DSE, UDSM zasaini makubaliano kurahisisha wanafunzi kufanya tafiti

Dar es Salaam. Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) limesaini mkataba wa makubaliano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kupitia Shule ya Biashara, wenye lengo la kurahisisha upatikanaji wa data kwa ajili ya tafiti za soko la mitaji na dhamana pamoja na kuimarisha elimu kwa umma.

Mkataba huo wa miaka mitatu ambao utakuwa ukihuishwa kila unapofikia ukomo, unalenga kupunguza changamoto za upatikanaji wa taarifa kwa wanafunzi na wahadhiri wa UDSM wanaofanya tafiti katika sekta ya fedha, hali iliyokuwa ikiwalazimu kufuata huduma hizo moja kwa moja katika ofisi za DSE.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumatatu Machi 30, 2026, Mwanasheria Mkuu wa DSE, Mery Mniwasa amesema ushirikiano huo utafungua fursa mpya za kielimu na kitaaluma kwa wanafunzi, ikiwamo kujifunza kwa vitendo kupitia kuanzishwa kwa maabara ya soko la mitaji chuoni hapo.

Amesema maabara hiyo itakuwa na vitabu, tafiti na mifumo mbalimbali itakayowawezesha wanafunzi kupata uelewa mpana wa masoko ya fedha kwa vitendo.

“Mkataba huu utadumu kwa miaka mitatu na baada ya hapo tutakuwa tukiuhuisha huku tukiboresha maeneo mbalimbali kulingana na mahitaji,” amesema Mniwasa.

Amesema kabla ya makubaliano hayo, DSE na UDSM tayari zilikuwa na ushirikiano wa muda mrefu usio rasmi, wanafunzi na wataalamu kutoka chuo hicho wamekuwa wakipata data kwa ajili ya tafiti zao.

“Si wanafunzi pekee, hata wataalamu kutoka chuo hicho wamekuwa wakihitaji data kwa ajili ya tafiti. Pia tumekuwa tukiendesha mashindano ya elimu ya juu ambapo wanafunzi wa UDSM hushiriki pamoja na vyuo vingine nchini,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Biashara ya UDSM, Profesa Omari Mbura amesema mkataba huo unatekeleza azma ya muda mrefu ya kuunganisha ujuzi na rasilimali kati ya taasisi hizo mbili za umma.

“Mkataba huu utanufaisha maeneo matatu makuu ambayo ni utafiti, ufundishaji na utoaji wa huduma kwa jamii,” amesema Profesa Mbura.

Ameongeza kuwa kupitia ushirikiano huo, chuo kitapata fursa ya kupata data na taarifa za kifedha zinazohusiana na masoko ya mitaji na dhamana, hatua itakayochochea ubunifu na kuongeza uwezo wa kuchambua taarifa hizo kwa manufaa ya jamii.

Mkuu wa Idara ya Fedha wa UDSM, Tobias Swai amesema tafiti nyingi hutegemea upatikanaji wa data sahihi, hivyo makubaliano hayo yatafungua wigo mpana zaidi kwa wanafunzi na watafiti kupata taarifa muhimu kwa wakati.

“Data ni rasilimali muhimu na si rahisi kuzipata bure. Kupitia makubaliano haya, tutapata si tu data za DSE bali pia taarifa za masoko ya kimataifa ambako DSE ina uhusiano,” amesema Swai.

Amesema hatua hiyo itachochea ubunifu katika soko la mitaji kwa kusaidia kuibua bidhaa mpya, kuboresha mitalaa ya masomo na hata kuanzisha programu mpya za kitaaluma zinazokidhi mahitaji ya soko.