TLS kujadili utekelezaji Dira 2050, lishe bora na maisha nje ya mahakama

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikijiandaa kwa mabadiliko ya kimaendeleo kufikia dira ya Taifa 2050, wanasheria wabobezi wameitana kujadili utekelezaji wa dira hiyo na nafasi ya mawakili katika kusimamia maadili ya kazi, haki za binadamu na uwajibikaji unaohitajika.

Wanasheria hao watakutana katika mkutano mkuu utakaofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) kuanzia Aprili 27 hadi Mei 2, 2026. Pia, mawakili watajadiliana maisha ya wakili nje ya mahakama, ikiwemo usimamizi wa fedha, lishe bora na uwiano kati ya kazi na maisha binafsi.

Katika mkutano huo wenye kauli mbiu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 na nafasi ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) katika kuimarisha maadili ya taaluma, utawala bora, haki za binadamu na utawala wa sheria ili kukuza haki na uwajibikaji,  Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju ndiye atakuwa mgeni rasmi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumatatu, Machi 30, 2026, rais wa TLS,  Boniface Mwabukusi, amesema umuhimu wa mkutano wa mwaka huu, ni pamoja na kuzindua mpango mkakati wa miaka mitano ambao TLS  wameuoanisha na Dira ya Taifa 2050 katika kuweka mkazo wa uadilifu, utawala bora na uwajibikaji.

Amesema mkutano huu unaokwenda kutoa wito kwa kila wakili kuongoza kwa uadilifu na kubaki kuwa ngao imara ya utawala wa sheria katika Taifa, utajadili namna bora kwa TLS kutekeleza kifungu cha nne ikiwamo kuishauri Serikali na kuwasaidia wananchi.

“Mkutano huu utajadili nafasi ya mawakili katika kusimamia maadili ya kazi, haki za binadamu, na uwajibikaji unaohitajika ili kujenga jamii ya kisasa na yenye usawa,” amesema Mwabukusi.

Amesema moja ya tukio muhimu katika mkutano huo ni kuwa na jukwaa la mawakili waandamizi na kujadiliana namna ya kuwajibika kama taasisi na kubainisha wanapoelekeza fani yao kwenye Dira ya Taifa 2050, wajibu wao kama mawakili unavuka mipaka ya mahakamani.

Akitoa mchanganuo wa majadiliano ya mkutano huo utakaoanza Aprili 27, Mwabukusi amesema: “Aprili 29, 2026 kutakuwa na jukwaa la “Multi-Dimension forum beyond Legal Practice 2026” ambalo litaangazia maisha ya wakili nje ya Mahakama, ikiwemo usimamizi wa fedha, lishe bora na uwiano kati ya kazi na maisha binafsi.

Hii itafuatiwa na Jukwaa la ‘Senior Lawyers Forum 2026’ litakalofanyika Aprili 30 lenye kaulimbiu ya “Kutoka Uzoefu hadi Ubora,” ambapo wakongwe wa fani hiyo watatoa dira na miongozo kuhusu mustakabali wa utoaji haki nchini Tanzania, sambamba na hayo pia watajadili namna bora ya TLS kuweza kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.

Amesema wataalamu wa sheria wenye ushawishi mkubwa nchini watajadili kwa kina na kutoa fursa kwa chama kutekeleza kifungu cha nne katika kuwasaidia wananchi.

“Tumeandaa wiki yenye mafunzo muhimu ya kisheria (CLE) pamoja na fursa adhimu za kujuana na kubadilishana uzoefu,” amesema Mwabukusi akiwakaribisha wanachama wao zaidi ya 3,000 ili kujifunza, kuungana, na kuweka misingi ya ubora wa kisheria itakayodumu kwa miongo mingi ijayo.