RIPOTI ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), Charles Kichere imebaini makadirio yasiyo sahihi ya gharama ya ujenzi wa Uwanja wa AFCON Arusha pamoja na pia udhaifu katika majadiliano ya zabuni ya ujenzi wa Uwanja huo.
Kichere amesema kuwa kiwango cha fedha kilichotarajiwa kutumika katika ujenzi wa Uwanja huo ni kidogo kulinganisha na kile kilichosainiwa katika mkataba wa ujenzi huo.
“Nilibaini mapungufu katika ununuzi wa mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Arusha wenye thamani ya Sh338.54 bilioni hali inayoashiria kukosekana kwa thamani hali ya fedha katika matumizi ya rasilimali za umma. Kwanza kulikuwa na tofauti kubwa kati ya makadirio na thamani ya mkataba.
“Ambapo mradi ulikadiriwa kugharimu Sh187 bilioni lakini ulisainiwa kwa Sh338.54 bilioni sawa na ongezeko la asilimia 81. Hali hii inaonyesha kuwa makadirio hayakuwa sahihi na yaliathiri maamuzi ya kibajeti pamoja na utekelezaji wa mradi.
“Pia mkandarasi alipatikana kwa njia ya mzabuni mmoja kwa kisingizio cha dharura bila kuwepo ushahidi wa hali hiyo. Hii iliondoa ushindani ambapo ungeweza kuhakikisha upatikanaji wa bei nafuu na kulinda maslahi ya serikali.
“Tatu majadiliano ya zabuni yalifanyika kwa udhaifu ambapo sehemu kubwa ya vipengele vilivyojadiliwa havikuwa vimeidhinishwa kwenye mpango wa majadiliano na wigo wa kazi ulipunguzwa bila kupunguza gharama ipasavyo. Aidha gharama zisizo halali ikiwemo Sh3.27 bilioni za gharama za zabuni zilijumuishwa katika mkataba na kubebwa na serikali,” amesema Kichere.
Rais Samia Suluhu Hassan akipokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 kutoka kwa Charles Kichere, leo Machi 30, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Kichere amesema kuwa hali hiyo inaonyesha udhaifu katika upangaji wa miradi.
Ujenzi wa Uwanja wa AFCON Arusha ulianza Machi 2024 ukitarajiwa kuingiza mashabiki 30,000 na kutumika kwa fainali za AFCON 2027 zitakazofanyika Tanzania, Kenya na Uganda.
Uwanja huo uliopewajina la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan unajengwa na Kampuni ya China Railway Construction Engineering Group Limited (CRCEG) kutoka China.
