Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu ameagiza kuchukuliwa hatua kwa watendaji wa mamlaka za Serikali waliopata hati zenye mashaka kufuatia ukaguzi wa usimamizi na matumizi ya fedha za umma nchini.
Rais Samia ameyasema hayo katika hafla ya kupokea taarifa za Mamlaka za ukaguzi; Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), leo Jumatatu Machi 30, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hizo kwa pamoja, Rais Samia amesema amefanya hivyo kutimiza sheria ya ununuzi wa umma akitaja kuwa ni hatua inayolenga kuongeza uwajibikaji wa taasisi za Serikali na kuwapa haki wananchi kufahamu taarifa za matumizi yanayofanyika.
Amesema taasisi hizo tatu zinafanana kwa kuwa zote zinachunguza manunuzi na matumizi ya fedha ili kuhakikisha thamani ya fedha inafanana na matumizi ya umma kwa mustakabali wa Taifa na manufaa ya wananchi kwa ujumla.
Akizungumzia taarifa zilizowasilishwa ambazo zimeibua kasoro na mafanikio kadhaa, Rais Samia amewapongeza viongozi wa taasisi hizo akisema taarifa zao zimeibua maeneo ambayo yanahitaji hatua madhubuti ili kufikia mafanikio yanayotakiwa, huku akioneshwa kuridhishwa na ongezeko la hati safi kwa mujibu wa taarifa ya CAG.
“Kwenye ripoti hii, CAG amebainisha mapungufu na hatua za kuchukua. Niseme tu Serikali itachukua hatua kwa mujibu wa Sheria na kama ilivyopendekezwa na CAG,” amesema, akimwelekeza Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Crispin Chalamila kusimamia kikamilifu majukumu ya taasisi hiyo.
Rais Samia amesisitiza ili kuhakikisha fedha za wananchi zinalindwa, taasisi zinazokutwa na hati chafu zitajwe hadharani bila kufichwa ili ziweze kuimarisha uwajibikaji na kupunguzia mianya ya ubadhirifu wa mali za Serikali.
“Uwajibikaji si chaguo, ni lazima, na uwajibikaji huu si kwa taasisi hizi tatu pekee bali kwetu sote. Hatutasita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria zetu,” amesema akimwagiza Katibu Mkuu Kiongozi kusimamia kikamilifu utekelezwaji wa mapendekezo yaliyotolewa na taasisi hizo.
Katika hatua za utekelezaji wake, Rais amesema ripoti ya CAG itawasilishwa bungeni kama inavyoelekezwa kwa mujibu wa sheria kwa ajili ya hatua stahiki akisisitiza utekelezwaji wa mapendekezo yaliyotolewa na viongozi wa taasisi hizo.
