Kuna ishu ya Yanga na Ibrahimovich

YANGA inaendelea na mpango wake wa kusaka vijana wa kujiunga na Shule yake ya soka lakini uko mpango mwingine ambao Yanga imeupanga kupitia program hiyo.

Mpango huo ni kushiriki mashindano maalum ya vijana Barani Ulaya ya Kombe la Gothia ambayo huwa maalum kwa maskauti wa soka Sweden na kwingineko Ulaya kutazama na kuchukua wachezaji wenye vipaji vya soka wanaoweza kujiunga na timu mbalimbali barani humo.

Historia ya mashindano hayo ya Gothia ndio inaonekana kuchangia kuishawishi Yanga kujipanga vilivyo kwa ajili ya kuhakikisha inafanya vyema katika mashindano hayo.

Nyota 12 waliowahi kutamba katika soka duniani walionekana kupitia mashindano hayo ambayo Yanga itashiriki yakipangwa kuchezwa kuanzia Julai 12 hadi 18 mwaka huu huko  Gothenbur, Sweden yakishirikisha timu kutoka mataifa 80 tofauti.

Mastaa 12 ambao wameibukia kupitia mashindano hayo ni Zlatan Ibrahimovic, Alan Shearer, Andrea Pirlo, Xabi Alonso, Emmanuel Adebayor, Dejan Kulusevski, Kim Källstrom, Júlio Baptista, Kosovare Asllani, Ze Roberto, Yassine Bounou na  Fridolina Rolfo.

Yanga inaamini kwamba ushiriki wake katika mashindano hayo utaiwezesha kuwaweka sokoni baadhi ya wachezaji na hivyo kuiwezesha klabu kuigiza kipato kupitia mauzo ya wachezaji hao. “Mpango mkubwa kwa sasa ni kuandaa timu yenye ubora wa hali ya juu ambao watatuwezesha kufanya vizuri katika mashindano ya Gothia ambayo tutashiriki mwaka huu. Tutashiriki kwa mara ya kwanza hivyo tunataka tuanze kwa gia na mafanikio makubwa,” kilifichua chanzo ndani ya Yanga.