Masasi. Simanzi, hofu na maswali mengi yamegubika Kijiji cha Mdenga, kata ya Nangoo wilayani Masasi mkoani Mtwara, kufuatia mauaji ya mwalimu wa Shule ya Msingi Mwongozo, Hidaya Chiwembi (51), anayedaiwa kuuawa baada ya kushambuliwa na kisha kunyongwa hadi kufa, tukio linalohusishwa na mgogoro wa mpaka wa shamba.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Machi 28, 2026, na kuacha majonzi kwa familia, ndugu, walimu wenzake pamoja na wakazi wa eneo hilo.
Akisimulia namna tukio hilo lilivyotokea katika mazingira ya kawaida kabla ya kugeuka kuwa mauaji alipozungumza na Mwananchi, Nasri Rajabu mtoto wa mwalimu huyo amesema siku ya tukio aliongozana na mama yake kwenda shambani saa tatu asubuhi kwa ajili ya shughuli za kilimo kama ilivyokuwa kawaida yao.
Amesema walilima hadi saa 9 alasiri, mama yake alimruhusu arejee nyumbani huku akisalia shambani.
Hata hivyo, mtoto huyo anasema walishangaa kuona mpaka saa 3 usiku mama yao hajarudi nyumbani, wakaanza kushikwa na wasiwasi.
“Ilikuwa siyo kawaida yake kuchelewa vile kutoka shambani, mpaka saa 3 usiku mama alikua hajarudi nyumbani, tukaanza kuingiwa na hofu. Bibi akanituma nikamtafute shambani, lakini sikufanikiwa kumuona,” amesema Nasri kwa masikitiko.
Amesema alipofika shambani alijaribu kumtafuta mama yake kwa kuzunguka maeneo mbalimbali, lakini hakumuona.
Hata hivyo, amesema wakati anazunguka na kumulika kwa tochi shambani hapo, aliona kipande cha kitenge ambacho mama yake alikuwa amekiviringishia simu asubuhi walipoondoka nyumbani kwenda shambani hapo.
“Tochi niliyokuwa namulikia kumtafuta mama ilikuwa na mwanga mdogo, nikashindwa kuendelea kumtafuta nikaamua kurudi nyumbani kutoa taarifa,” amesema Rajabu.
Amesema familia kwa kushirikiana na baadhi ya walimu wa shule hiyo na wananchi, walianza msako wa kumtafuta usiku huo, lakini jitihada hizo hazikuzaa matunda.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nangoo, Edwin Mchopa akizungumzia tukio hilo, amesema walirejea tena shambani jana Jumapili Machi 29, saa 12 asubuhi kuendelea na utafutaji.
Amesema baada ya muda mfupi wa msako, waliliona kapu lililokuwa na baadhi ya vifaa vya marehemu, likiwamo dumu la maji ya kunywa.
“Baada ya kulisogelea eneo hilo, mwalimu mmoja aliyekuwa rafiki yake wa karibu aliuona mwili wake akapiga kelele tuliposogea tukaona ni yeye lakini ameshakufa,” amesema Mchopa.
Anasema mwili wake ulikuwa umetapakaa damu ukiwa umelala chini, lakini eneo hilo lilionekana limevurugika kuashiria kulikuwa na mapigano na simu yake ilikuwa pembeni imevunjwa.
“Tunasikitika sana kwa kumpoteza mwalimu mwenzetu katika mazingira haya ya kikatili. Tunaomba vyombo vya dola vifanye uchunguzi wa kina ili wahusika wakamatwe na kufikishwa mbele ya sheria,” amesema Mchopa.
Mwalimu Mchopa amesema walitoa taarifa Kituo cha Polisi Ndanda na askari walifika eneo la tukio kufanya uchunguzi wa awali na kuuchukua mwili wa marehemu na kwenda kuuhifadhi Hospitali ya Mtakatifu Benedict Ndanda kwa ajili ya uchunguzi.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Issa Suleimani amesema uchunguzi wa awali wa madaktari umebaini marehemu alipata majeraha makubwa yaliyosababishwa na kunyongwa shingo na kupigwa na kitu butu kichwani, hali iliyosababisha kupoteza damu nyingi na kufariki dunia.
Hata hivyo, amesema chanzo cha mauaji hayo ni mgogoro wa mpaka wa shambani ulioibuka kati ya marehemu na mtuhumiwa ambaye hajamtaja jina.
Amedai kuwa mtuhumiwa alikuwa amechimba udongo wa kufyatulia tofali za kuchoma kwenye mpaka huo bila ridhaa ya Mwalimu Chiwembi.
Amesema Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka mtuhumiwa huyo ambaye kwa sasa ametoroka.
“Tumeshamfahamu aliyefanya mauaji hayo kwa sababu baada ya kutenda alitoroka, sisi Kama Jeshi la Polisi tunaendelea na uchunguzi na mara tu baada ya kumkamata tutamfikisha mahakamani,” amesema kamanda huyo.
Amewataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi huku akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kufanya vitendo hivyo.
