Mwanza. Watendaji wa sekta ya madini, hususan maofisa madini wakazi wa mikoa, wametakiwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo ya migodi ili kubaini mapema hatari zinazoweza kusababisha ajali, kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha nchini.
Wito huo umetolewa leo Jumatatu Machi 30, 2026 jijini Mwanza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Yahya Samamba wakati akifungua kikao cha pili cha Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Madini.
Samamba amesema mvua zinazoendelea kunyesha zimeongeza hatari ya ajali migodini, hali inayoweza kusababisha majeruhi na vifo, iwapo hatua za tahadhari hazitachukuliwa mapema.
Amesisitiza umuhimu wa watumishi wa sekta hiyo kuongeza juhudi katika ukaguzi na usimamizi wa usalama migodini ili kupunguza hatari zinazoweza kuepukika.
Amesema ni wajibu wa watumishi kuhakikisha wanatoa elimu kwa wachimbaji na kusisitiza ukaguzi wa mara kwa mara wa miundombinu ya migodi, hususan katika kipindi hiki cha mvua.
“Nimelielekeza Baraza la Wafanyakazi kuhakikisha wanapokwenda katika mikoa na ofisi zao wawasisitize wenzao kufanya ukaguzi wa misingi ya migodi ili kuepusha madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizi, ikiwemo vifo na majeruhi. Thamani ya uhai wa mtu mmoja ni kubwa kuliko madini tunayozalisha,” amesema Samamba.
Aidha, amewataka watumishi hao kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano katika kusimamia shughuli za madini, hatua itakayosaidia kudhibiti utoroshaji wa madini na kuongeza mapato ya Serikali.
Amesema matumizi ya mifumo ya kisasa yataongeza uwazi na ufanisi katika usimamizi wa rasilimali za madini.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Ramadhani Lwamo amezungumzia umuhimu wa baraza hilo, akisema ni jukwaa linalokutanisha menejimenti na wawakilishi wa wafanyakazi kwa lengo la kupitia na kutathmini utekelezaji wa mpango kazi na bajeti ya mwaka 2025/2026.
Amesema pia huweka mikakati ya kuboresha utendaji kazi na kuimarisha mahusiano kazini.
Amesema katika utekelezaji wa maelekezo ya kikao kilichopita, baraza limefanikiwa kushughulikia masilahi ya watumishi, ikiwemo ongezeko la mishahara kwa asilimia tano pamoja na kuanza kwa utekelezaji wa mfumo wa motisha, hatua inayotarajiwa kuongeza ari ya kazi.
Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dk Janet Lekashingo amesema tume inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, ambapo hadi Machi 24, 2026 imekusanya Sh1 trilioni, sawa na asilimia 111.2 ya lengo la miezi tisa.
Amesema mafanikio hayo yametokana na usimamizi mzuri wa sheria na kanuni za sekta ya madini pamoja na kuimarishwa kwa ukaguzi wa usalama, afya na mazingira migodini.
Amesisitiza kuwa juhudi hizo zinalenga kuhakikisha shughuli za uchimbaji madini zinafanyika kwa kuzingatia usalama wa wachimbaji na uendelevu wa mazingira.
