Stamico, Planet One wasaini mkataba uchimbaji madini ya kinywe 

Mirerani. Naibu Waziri wa Madini, Dk Stephen Kiruswa amesimamia utiaji saini wa mkataba wa utafiti, uchimbaji na uchakataji madini ya kinywe ndani ya ukuta wa madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.

Mkataba huo wa leseni tatu za uchimbaji madini mkakati ya kinywe umesainiwa leo Jumatatu Machi 30, 2026 mji mdogo wa Mirerani na Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico), Dk Venance Mwase na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Planet One, Ramakrishna Chinnamsetty.

Dk Kiruswa akizungumza kwenye hafla hiyo amewaagiza viongozi wa wilaya hiyo kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kampuni hiyo ili iweze kufanya kazi yao ipasavyo.

“Madini ya kimkakati ya kinywe yanatumika katika mambo mbalimbali ikiwemo kutengeneza betri za magari yanayotumia umeme,” amesema Dk Kiruswa.

Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa akizungumza baada ya utiaji saini wa mkataba wa utiaji saini wa hatua ya awali ya utafiti wa kina, uchimbaji na uchakataji wa madini ya Kinywe leo Jumatatu Machi 30, 2026 katika mji mmdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo

Amesema mkataba huo wa leseni tatu za utafiti wa madini ya kinywe unapaswa kuanza mara moja ili waendeleze uchimbaji na uchakataji wake kwa kiwanda chake kujengwa Mirerani.

Dk Mwase amesema wataendelea kuwa mashine ya kuwezesha wachimbaji madini katika utendaji kazi wao na wana Mirerani waupokee mradi huo mkubwa.

Mwase amesema wana Mirerani wasitegemee madini ya Tanzanite pekee kwani mradi huo wa madini ya kimkakati ya kinywe pia utatoa ajira kwa wana Simanjiro na mapato kwa halmashauri ya wilaya hiyo.

Katibu Tawala wa wilaya ya Simanjiro, Warda Abeid Maulid amewahakikishia viongozi wa Planet One ushirikiano wa kutosha ili waweze kufanya kazi zao inavyopaswa.

Chinnamsetty amesema baada ya kutia saini mkataba huo hivi sasa wapo tayari kuanza rasmi shughuli zao.

Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico), Dk Venance Mwase (kulia) na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya PlanetOne, Ramakrishna Chinnamsetty wakati wakisaini mikataba ya uchimbaji wa madini ya Kinywe leo Jumatatu Machi 30, 2026 katika mji mmdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo

Amesema watashirikiana na Serikali, viongozi na jamii kwa ujumla inayozunguka eneo hilo katika utafiti, uchimbaji na uchakata madini hayo ya kimkakati ya kinywe.

Katibu wa Chama cha Wachimbaji Madini mkoani Manyara (Marema) Tawi la Mirerani, Rachel Njau ameipongeza kampuni hiyo kwa kupata fursa ya kutafiti, kuchimba na kuchakata madini ya kinywe.

Njau amesema anatarajia watachochea uchumi wa wakazi wa mji mdogo wa Mirerani na Simanjiro kwa ujumla.

Mchimbaji wa madini ya Tanzanite katika mji mdogo wa Mirerani, Shabani Hamis amesema utiaji saini huo utakuwa fursa nzuri ya kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo.