Dar es Salaam. Mamlaka Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) imeibua kasoro mbalimbali za manunuzi ikiwemo asilimia 30 ya taasisi hazikutenga fedha kwa ajili ya makundi maalumu huku miradi 65 ya manunuzi ikibainika kutelekezwa katika taasisi 33 za umma.
Pia, taasisi 10 za ununuzi hazikufanyia kazi ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) katika mikataba ya thamani ya Sh143.1 bilioni na mingine ya Sh101.3 bilioni ilitolewa kama tuzo na taasisi mbalimbali bila kufuata utaratibu.
Licha ya dosari hizo, kiwango cha zabuni nchini kimekua kwa asilimia 14 katika kipindi cha miaka mitano mfululizo kati ya mwaka 2022 hadi 2025.
Hayo yamebainishwa leo Jumatatu, Machi 30, 2026 na Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba wakati akisoma muhtasari wa taarifa yake ya mwaka wa utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais Samia Suluhu Hassan akipokea taarifa ya mwaka ya utendaji kazi wa Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) kutoka kwa Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Dennis Simba, leo Machi 30, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Amesema mwaka 2022/23 zabuni ziliongezeka kwa asilimia 11 kutoka asilimia 65 hadi 76 na mwaka 2024/25 zikiongezeka kwa asilimia 3 kutoka asilimi 76 hadi 79.
“Zabuni zimeongezeka kwa asilimia 82 na idadi ya wazabuni wanaoshiriki imeongezeka kwa asilimia 98 kwa mwaka 2023/24 na 2024/25 huku asilimia 62 ya manunuzi yote yaliofanyika, ikitolewa kwa wazabuni wazawa,” amesema.
Ameongeza, PPRA imeokoa takribani Sh13.3 bilioni ambazo zingetumika kununua karatasi na vifaa vya ofisi na kupunguza zaidi ya tani 54 elfu za hewa ukaa, hivyo kuchangia katika uhifadhi wa mazingira nchini, kutokana na matumizi ya teknolojia ya Nesti katika uchakataji taarifa.
“PPRA imeweka malengo ya kuhakikisha uwazi kupitia teknolojia ya kisasa ikiwemo akili unde (AI), kukomesha upendeleo ili kuvutia makundi maalumu na kuvutia wazabuni wazawa ili kufikia malengo yake,” amesema.
Simba amesema pamoja na mafanikio yaliyofikiwa, asilimia 30 ya taasisi hazikutenga fedha kwa ajili ya makundi maalumu, yaani wanawake, vijana na wenye ulemavu.
Amesisitiza kuwa PPRA imedhamiria kuimarisha ufuatiliaji wa uzingatiaji wa sharia, ili kuhakikisha ununuzi wa umma unazingatia sharia, kanuni na taratibu za ununuzi umma.
Mbali hiyo, amesema taasisi 10 za ununuzi hazikufanyia kazi ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) katika mikataba ya thamani ya Sh143.1 bilioni.
Ili kudhubiti changamoto hiyo, amesema PPRA imeandaa moduli ya mfumo wa kuwezesha AG kuona na kujiridhisha na utekelezaji wa sheria.
“Mikataba 481 yenye thamani ya Sh2.8 trilioni ilifikia thamani halisi ya fedha, mikataba 70.7 yenye thamani ya Sh1.7 trilioni ilifikia kiwango cha thamani kwa wastani huku mikataba 87 yenye thamani ya Sh374.1 bilioni haikufikia kabisa thamani ya fedha,” ameongeza.
Ameibua udhaifu mwingine kuwa Sh101.3 bilioni zilitolewa kama tuzo na taasisi mbalimbali bila kufuata utaratibu, huku tuzo za juu zikitotolewa kwa upendeleo na kupelekea ongezeko la gharama kwa Sh5.1 bilioni.
Amesema zilitolewa tuzo kwa wazabuni wasiokidhi vigezo, zenye thamani ya Sh685.2 bilioni huku taasisi za ununuzi 21 zikibainika kuchelewa kuanza manunuzi yenye thamani ya Sh154.7 bilioni.
“Miradi 65 katika taasisi za nunuzi 33 iliitelekezwa. Pia taasisi nunuzi 24 zilifanya malipo ya Sh112.6 bilioni katika mikataba 39 kwa kazi ambazo hazikutekelezwa,” amesema akiongeza kuwa mamlaka hiyo pia imebaini mikataba 68 yenye thamani ya Sh32.3 bilioni haikuwasilishwa dhamana zake.
Simba amesema kupitiaa uchunguzi maalumu uliofanywa na mamlaka hiyo, umebainika ukiukwaji wa sheria za ununuzi wa umma na PPRA imechukua hatua ambazo zimeokoa Sh634.1 bilioni.
Pia imechukua hatua kwa wazabuni 34 ambazo zimekutwa na makosa mbalimbali yakiwemo kushindwa kutekeleza sheria, kugushi nyaraka na kushindwa kusaini mikataba iliyotolewa.
Katika suluhu ya kudumu ya matatizo hayo, Simba amesema, PPRA imewekeza katika mifumo yake ya kiteknolojia kuhakikisha mifumo ya manunuzi ya umma inadhibitiwa na inatoa nafasi kwa AG kuona na kutoa ushauri kwa taasisi inayofanya manunuzi ili kuhakikisha sheria na taratibu za manunuzi ya umma zinazingatiwa ipasavyo.
Amesisitiza PPRA imejiwekea malengo ya kuhakikisha makundi maalumu wakiwemo vijana yanawezeshwa kikamilifu huku wazabuni wazawa wakipewa kipaumbele katika sekta hiyo.