WIZI WA MTOTO WAMPONZA, AFUNGWA MWAKA MMOJA

**

Mahakama ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza imemhukumu Novina Yoel Kuboja (23), ambaye ni mkulima na mkazi wa Buchosa wilayani humo, kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuiba mtoto wa kiume mwenye umri wa miezi mitatu (jina limehifadhiwa kwa sababu za kisheria).

Hukumu hiyo imesomwa leo Machi 30, 2026, na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Mhe. Evod Kisoka, ambapo mshtakiwa hakutaka kuisumbua mahakama kwa kukiri kutenda kosa hilo na kupatikana na hatia ya kuiba mtoto kinyume na kifungu cha 169 (1)(a) cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, marejeo ya 2023.

Kwa mara ya kwanza, Novina amefikishwa mahakamani leo tarehe 30 Machi, 2026, na kusomewa shtaka linalomkabili na Wakili wa Serikali, Rivana Kasinisala, katika kesi ya jinai namba 6895/2026. 

Inadaiwa alitenda kosa hilo mnamo Machi 11, 2026, katika kijiji cha Nyamatemele, kata ya Nyehunge, wilaya ya Sengerema.

Katika utetezi wake, mshtakiwa alieleza mahakama kuwa aliiba mtoto huyo kwa lengo la kwenda kumlea kwani yeye hana uwezo wa kupata mtoto.

“Mheshimiwa Hakimu, ninaomba nipunguziwe adhabu kwani ni mara yangu ya kwanza kutenda kosa hili. Lengo langu halikuwa baya, ni changamoto tu ya kutopata mtoto,” aliomba Novina.

Kauli hiyo ilipingwa vikali na upande wa mashtaka ambapo Wakili Kasinisala alisisitiza kuwa kitendo kilichofanywa na mshtakiwa ni cha kikatili na kinyume cha sheria, hivyo akaiomba mahakama itumie mamlaka yake kutoa adhabu kali ili kukomesha vitendo vya wizi wa watoto.

Akitoa hukumu hiyo, Mhe. Kisoka amesema mahakama haina mbadala wa kutoa adhabu nyingine kwani kifungu husika kinatoa adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela, hivyo akaamuru mshtakiwa kutumikia kifungo hicho gerezani.