CAG Dkt. Kichere Aibua Kasoro Kwenye Mradi wa Uwanja wa Arusha – Video

Global Publishers
March 31, 2026
0 Comments

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, Machi 30, 2026 amewasilisha ripoti kuu ya mwaka wa fedha 2024/2025 kwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika Ikulu jijini Dar es Salaam, akibainisha mapungufu katika baadhi ya miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa uwanja wa mpira wa Arusha.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mradi wa ujenzi wa uwanja huo ulikadiriwa awali kugharimu takribani Shilingi bilioni 187, lakini hatimaye mkataba wa ujenzi ulisainiwa kwa kiasi cha Shilingi bilioni 338.54, ikiwa ni ongezeko la takribani asilimia 81.

Dkt. Kichere amesema uchunguzi wake ulibaini mapungufu katika mchakato wa ununuzi wa mradi huo, hali inayoweza kuashiria kutokuwepo kwa thamani halisi ya fedha katika matumizi ya rasilimali za umma.

“Nilibaini tofauti kubwa kati ya makadirio na thamani ya mkataba. Mradi ulikadiriwa kugharimu Shilingi bilioni 187 lakini ulisainiwa kwa Shilingi bilioni 338.54, ongezeko la asilimia 81. Hali hii inaonyesha kuwa makadirio hayakuwa sahihi na yaliathiri maamuzi ya kibajeti pamoja na utekelezaji wa mradi,” amesema Dkt. Kichere.

Ripoti hiyo inaendelea kuainisha maeneo mbalimbali yenye changamoto katika usimamizi wa fedha za umma, huku ikisisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya upangaji, manunuzi na usimamizi wa miradi ya serikali ili kuhakikisha uwazi na ufanisi katika matumizi ya rasilimali za nchi.

Taarifa hiyo imewasilishwa katika kipindi ambacho serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini, huku ripoti za CAG zikitumika kama nyenzo muhimu ya kuboresha uwajibikaji na kuongeza ufanisi katika matumizi ya fedha za umma.