Dar es Salaam. Katika maeneo mbalimbali, kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wazazi kuhusu vitendo vya baadhi ya wasaidizi wa nyumbani, wakiwemo wanaotuhumiwa kwa uzembe, wizi hata ukatili dhidi ya watoto
Kilio cha muda mrefu cha akina mama ni kimoja kukosa dada wa kazi wa kuwaaminika.
Asubuhi zimekuwa na presha, mama akijiandaa kuwahi kazini, mtoto mchanga mikononi, huku mawazo yakigawanyika kati ya kazi na usalama wa mtoto.
Kutokana na hali hiyo, wanawake wa mtaa wa Amani, Ubungo External jijini Dar es Salaam wamelazimika kutafuta suluhisho lao wenyewe, haikuwa sera, wala mradi rasmi ilikuwa ni hatua ya dharura ya kusaidiana.
Ilianza pale mama mmoja alipomwomba jirani yake amshikie mtoto kwa muda mfupi na kadri siku zilivyopita, maombi kama hayo yaliongezeka.
Ndani ya muda mfupi, nyumba moja ikawa kituo kisicho rasmi cha kulelea watoto.
Leo hii, wanawake watatu wa familia moja wanashirikiana kulea watoto wa wazazi wanaokwenda kazini, wakifanya kazi ambayo wengi wanaiita ya mama wa wote.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Machi 30, 2026, Amina Ngwache amesema wazo la kulea watoto alikuwa nalo dada yao ambapo alikuwa anaachiwa mtoto mmoja na mfanyakazi wa kiwandani na huyo aliwaeleza wengine.
“Yule dada baada ya kuona mtoto wake analelewa vizuri aliwaambia na wenziwe wenye shida ya wadada wa kazi hivyo wakaanza kuleta,” amesema Amina.
Amesema hadi sasa wanajumla ya watoto 17 na mdogo zaidi ya wote ana miezi saba na mkubwa anamiaka miwili na idadi hiyo imegawanywa watu watatu kwa kuwa na watoto sita kwa watano.
Amesema sababu ya kupelekewa watoto hao ni changamoto ya wadada wa kazi ambapo mmoja ya wazazi aliyepeleka mtoto wake hapo ni baada ya mwanawe kupigwa na binti kisha kuvunjwa mguu.
“Kuna mtoto tumeletewa hapa mama yake alisema alipigwa na binti wa kazi hadi kumvunja mguu jambo ambalo limekuwa tishio kwa wazazi wengui huku wengine wakiugulia nauli wanzotumia kuagiza wasichana kisha wanatoroka,” amesema Amina.
Tofauti na ilivyotarajiwa, huduma hiyo haijabaki kwa wakazi wa Ubungo External pekee.
Amesema watoto wanaolelewa kwenye nyumba hiyo wanatoka maeneo mbalimbali ya Jiji, ikiwemo Mbagala, Tandika na Buza.
Amina amesema wazazi wao hulazimika kusafiri umbali mrefu kila siku ili kuwafikisha watoto wao kabla ya kuelekea kazini.
“Wengi wao wanafanya kazi viwandani wanaingia asubuhi na mapema, ndiyo maana wanawaleta huku mapema,” amesema.
Mlezi huyo amesema watoto hupokelewa kuanzia saa 1:30 asubuhi na hukaa hadi saa 1:00 jioni, muda ambao wazazi wao hurudi kuwachukua.
Gharama nafuu, msaada mkubwa
Amesema huduma hiyo hulipiwa Sh2,000 kwa siku kwa mtoto mmoja, kwa baadhi ya wazazi waliomba kutokana na kipato na wengine hulipa Sh40,000 kwa mwezi.
Amesema kwa wazazi wengi, hii ni nafuu ikilinganishwa na gharama za kuajiri dada wa kazi wa kudumu.
Katika kuhudumu watoto kwa weledi amesema wazazi wanapowapeleka watoto wao, huacha mahitaji muhimu kama taulo za watoto (Pampas), uji, chakula na wakati mwingine dawa.
“Hakuna kitu kingine kikubwa wanachotuachia, zaidi ya mahitaji ya mtoto na sisi kazi yetu ni moja ya kuwalisha na kuwaangalia mienendo yao,”
Pamoja na umuhimu wa huduma hiyo, Amina amesema mazingira ya kulelea watoto bado ni changamoto kubwa.
Amesema nyumba inayotumika ni ya familia na ni ndogo, hali inayosababisha msongamano wa watoto kwani hulala kwenye mikeka, wakitumia kanga zao.
Walezi hulazimika kupanga ratiba ya kuwahudumia ili kuhakikisha kila mmoja anapata nafasi na uangalizi.
“Tunafanya kwa kujitahidi sana, lakini ukweli ni kwamba sehemu ni ndogo hivyo tulikuwa tunahitaji eneo kubwa na magodoro ili kuwasaidia watoto tunaowalea,” amesema.
Kutokana na watoto wadogo huwa na changamoto nyingi za kiafya, na hapa hali si tofauti, Amina amesema mtoto anaweza kuletwa akiwa mzima, lakini baadaye akaanza kuugua au kulia kwa muda mrefu.
Amesema kukabilianana hali hiyo, walezi hulazimika kuchukua hatua za awali za hudumaya kwanza kwa kuwapa Panado pamoja na kumjulisha mzazi.
“Tunawahudumia kwa uwezo wetu, lakini tukiona hali si nzuri,tunampa dawa kushusha homa na tunamjulisha mzazi,” anaeleza.
Amesema hii inaongeza uzito wa jukumu lao, hasa kwa kuwa hawana mafunzo rasmi ya afya ya watoto na wanalea kwa uzoefu wa watoto wao na wajukuu zao na si watu baki.
Mlezi mwingine, Sharifa Makuka amesema kunapotokea shughuli yoyote kwenye nyumba hiyo hutoa taarifa kwa wazazi kwa kuwahi kuchukua watto siku hiyo na kuchukua mapumziko kwa siku nne hadi tano.
“Mwezi uliopita tulikuwa na msiba tuliwaambia wazazi wasilete watoto siku ya Jumamosi ulipotea msiba na tutaendlea na ulezi Jumatano,”amesema Sharifa.
Amesema msiba huo umeisha rasmi Machi 29, 2026 amabpo hawakupokea watoto hao na hivyo kuendelea na kazi leo machi 30 mwaka huu.
Amesema wamefanya hivyo kutokana na hekaheka za kwenye shughuli ni ngumu kuwa makini na watoto kani kuna kuwa na umati wa watu wengi.
Amesema inaponyesha mvua wanakuwa makini zaidi na kutoruhusu watoto kutoka nje ilikutotokea hatari za watoto kucheza kwenye maji.
“Mvua ikinyesha kwa kweli ni shida tunakuwa makini na watoto kuliko kitu chochote maana ndiyo kazi tuliochagua hivyo tunajikuta tunabeba watoto wawili wawili,”amesema.
Kutokana na kusambaa kwa video ikionyesha walezi hao na watoto wao Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake, Jinsia na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima kupitia kurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram amesema maofisa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii watafika eneo hilo haraka.
“Ahsanteni sana wote mlionitumia video hii inayowahusu akina mama kadhaa huko eneo la External, Kazamoyo, jijini Dar es Salaam ambao, wamejianzishia shughuli binafsi ya kulea watoto kutwa wanaoachwa na wazazi wao wanapoenda kwenye shughuli zao za kutafuta riziki.
Maofisa Maendeleo na Ustawi wa Jamii watafika eneo hilo haraka kesho ili kuwaona na kuwapa ushirikiano kuhusu miongozo na taratibu ili huduma yao iwe njema zaidi katika kuijenga vema zaidi sekta yao binafsi,”.
Aidha, ametoa wito kwa wote wanaopenda kufanya shughuli za malezi na makuzi kama sekta binafsi, wasisite kujitokeza na kuwaona maofisa ustawi wa jamii na maendeleo ya jamii ili, waifanye vema zaidi kwa tija zaidi.