Uwajibikaji duni wasababisha hifadhi ya Tazama kuvamiwa

Dar es Salaam. Katika sehemu ya pili ya uchunguzi maalumu wa Mwananchi linakuleta kuhusu hatari zinazolikumba eneo la ukanda wa bomba la mafuta la Tazama, tunakuletea mvutano wa kauli kati ya Serikali na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), huku kila upande ukieleza msimamo wake kuhusu matumizi ya eneo hilo nyeti.

Katika uchunguzi huo, Mwananchi imebainika licha ya marufuku ya kufanya shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya miundombinu hatarishi, bado kuna uwepo wa shughuli mbalimbali, ikiwamo uwekaji nyaya za umeme zenye msongo mkubwa karibu na bomba hilo.

Akizungumza na Mwananchi, Meneja Uendeshaji wa Kanda ya Tanzania wa Tazama, Saimon Salu, anadai kuwa hata Tanesco wamevamia eneo hilo, hali inayoongeza hatari kwa wananchi na wafanyabiashara wanaoendelea na shughuli zao katika ukanda huo.

Alipotafutwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange, kwa ajili ya ufafanuzi wa suala hilo, alijibu kwa kifupi, “Siwezi kuzungumzia suala hili kwa wakati huu.”

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, James Mataragio, alisema mamlaka husika zinatarajia kufanya ziara ya ukaguzi katika eneo hilo ili kubaini hali halisi ya uvamizi wa miundombinu hiyo na kuchukua hatua stahiki kukabiliana na tatizo hilo.

“Pia, Tazama kuna wakaguzi wao watakaofuatilia na kutathmini hali iliyopo ili kutafuta ufumbuzi,” anasema Dk Mataragio.

Hata hivyo, Salu anaendelea kufafanua kuwa imekuwa changamoto kudhibiti miundombinu yao na wamekuwa kwenye mjadala na Tanesco kuangalia uwezekano wa kuondoa nguzo zao kwenye miundombinu ya bomba hilo.

Wakati Salu akieleza hayo, gazeti hili lilizungumza na Shadrack Kitobero, mwajiriwa wa Tazama mwenye jukumu la kulinda na kukagua miundombinu hiyo kila siku kuanzia Kigamboni hadi Mbagala Rangi Tatu, ambaye anasema wanakumbana na changamoto katika ulinzi.

Anasema wanapowabana baadhi ya wananchi wanaovamia maeneo hayo, hujibu wamepewa ruhusa na viongozi wa serikali za mitaa.

“Tumejiridhisha kuwa mara nyingi wanashirikiana na baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa, hulipa fedha na maeneo hayo hukodishwa kwao kwa malipo ya kila mwezi,” anasema.

Anasema kila mwenye kibanda katika eneo lililovamiwa huwa na mtu nyuma yake anayenufaika na kodi ya pango ya kila mwezi, na pia hulipa ushuru.

Anafafanua kuwa baadhi ya watu wamejenga nyumba zao hadi kufika ndani ya hifadhi ya bomba hilo, huku mbele yake wakijenga vibanda vya biashara wanavyovikodisha kwa wafanyabiashara kwa malipo ya mwisho wa mwezi.

Kwa mujibu wake, jukumu lao kubwa ni kutoa taarifa kwa wanaovamia hifadhi hizo.

Anatoa mfano wa eneo la Uwokovu Chemchem, Mbagala, ambako mkazi mmoja amejenga hadi ndani ya hifadhi hiyo. Baada ya taarifa kutolewa, mamlaka zilifika na kuweka alama za mipaka, hali iliyozua taharuki.

“Tulimwambia avunje sehemu ya nyumba yake pamoja na bustani ya maua aliyoijenga, lakini amekuwa mgumu. Tayari alishapewa notisi ya kuondoka; kilichobaki ni kwa uongozi kuchukua hatua ya kubomoa, pamoja na vibanda vingine,” anasema.

Shadrack anasema baadhi ya wavamizi huwadharau kwa sababu hawana sare wala vitambulisho vinavyoonyesha kazi zao.

“Hatuna vitambulisho; ukijaribu kuwaeleza, mara nyingi hawaelewi na hudhani labda tumekuja kwa nia nyingine. Mazingira ya mjini yana changamoto zake kila mtu anajiona anajua, hivyo wanatuchukulia poa,” anasema.

Anaeleza pia kuwa wakati mwingine hulazimika kutumia muda mwingi kujieleza na kuwashawishi wananchi waelewe, hasa wanapoulizwa maswali mengi. Hata hivyo, wanapokutana na watu wanaowafahamu, hali huwa rahisi zaidi.

“Eneo la Zakhem (Mbagala) ni gumu, tunapata shida kwa sababu linategemea maisha ya watu wengi mama lishe na wauzaji wa pombe. Ukizungumza nao, wanakuambia hapa ndipo wanaposomesha watoto wao na kujiuliza wataenda wapi wakiondolewa,” anasema.

Anasema baadhi yao wamechukua mikopo mikubwa kwa ajili ya shughuli hizo za ujasiriamali ndani ya hifadhi ya miundombinu, licha ya kufahamu hatari iliyopo. 

Wakati hali ikiwa hivyo, wadau wamependekeza mambo matano ya kuzingatiwa ili kulinda miundombinu ya Bomba la Tazama, ikiwemo wananchi kujenga utamaduni wa kuheshimu taratibu na sheria zilizopo.

Wakili wa kujitegemea, Edson Kilatu, anasema kinachoendelea katika hifadhi hiyo ni uvamizi wa maeneo ya wazi, unaosababishwa na kukosekana kwa utamaduni wa kuheshimu sheria pamoja na kukithiri kwa vitendo vya rushwa vinavyohusisha baadhi ya wasimamizi.

 “Eneo la wazi linalindwa na sheria. Inashangaza kuona mtu anaanza kujenga au kufanya biashara hapo bila kuchukuliwa hatua. Hapa kuna mtu ananufaika.”

 “Sheria hazipo kama urembo. Hata kama adhabu haijatajwa wazi, lazima zitekelezwe. Ila kwa sababu ya ujanja, watu wanazipindisha na kufanya wanavyotaka,” anasema.

Kilatu pia anahoji wajibu wa halmashauri, akisema zinapaswa kusimamia kikamilifu matumizi sahihi ya ardhi. Anasema uvamizi huanza taratibu, kisha baadaye watu hujenga majengo ya kudumu, hata ya ghorofa, bila kuchukuliwa hatua.

Anaeleza kuwa kuna tatizo kubwa la uwajibikaji, akidai wakurugenzi na maofisa mipango miji wanafahamu uvunjwaji wa sheria unaoendelea lakini hawachukui hatua stahiki.

Kilatu anasema ujenzi holela umesababisha hasara kwa Serikali na wananchi.

“Mtu mgeni akiingia Dar es Salaam anaweza kudanganywa na kununua eneo la wazi akiamini muuzaji ni mmiliki halali. Ndicho kilichowakuta baadhi ya wananchi katika maeneo kama Kimara na Jangwani,” anasema.

Anasema hali hiyo ikiachwa iendelee husababisha migogoro na mateso kwa wananchi pale uongozi mpya wa Serikali unapoamua kutekeleza sheria kwa kuvunja majengo, kama ilivyowahi kutokea katika maeneo ya Kimara.

Wataalamu wa masuala ya majanga wameonya kuwa kuendelea kwa shughuli za kibinadamu karibu na miundombinu nyeti kunaweza kuhatarisha usalama wa wananchi na mali zao.

Akizungumzia hilo, mtaalamu wa masuala ya majanga, James Mbatia anasema majanga mengi duniani husababishwa na binadamu, ambapo karibu asilimia 99 hutokana na uzembe au makusudi ya kibinadamu.

Mbatia anasema shughuli zinazoendelea kufanyika karibu na miundombinu hiyo muhimu ni janga linalojitengeneza lenyewe.

“Hili si janga la asili bali linalotengenezwa na binadamu. Likitokea, haiwezi kusemwa ni bahati mbaya bali ni mauaji ya kukusudia,” anasema Mbatia.

Anasema uhai wa binadamu una thamani kubwa kuliko kitu chochote. Endapo vifo vitatokea kutokana na uzembe huo, wahusika wanapaswa kuwajibishwa kisheria kwa kuwa sheria zipo na zinaeleza wazi.

Kwa mujibu wa Mbatia, changamoto kubwa ipo kwa watendaji wa mipango miji na katika utoaji wa vibali vya ujenzi, ambao mara nyingi hushindwa kufuata sheria zilizopo.

“Sheria zipo, lakini hazifuatwi. Udhaifu huu unahitaji mamlaka kuchukua hatua za kinga sasa kabla janga halijatokea,” anasema.

Amesema kuwa ni muhimu mamlaka kujikita zaidi katika hatua za kinga badala ya kusubiri majanga yatokee ndipo zichukuliwe hatua. Anaonya kuwa athari za majanga ni kubwa na zinaacha majeraha ya kudumu kwa jamii.

“Kinga ni bora kuliko tiba. Elimu itolewe kwa wakazi wa maeneo hayo pamoja na wale walioweka miundombinu kwa kuzingatia sheria. Tukifuata sheria, suluhisho linapatikana badala ya kusubiri vifo vitokee,” anasema Mbatia.

Kwa upande wake, Profesa Amos Majule kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ameishauri Tazama kujenga uzio kama ilivyo katika miundombinu ya reli ya kisasa (SGR). Anasema ingawa ujenzi wa uzio huo ni wa gharama kubwa, ni njia bora zaidi ya kuhakikisha usalama.

“Wajenge uzio kwa usalama zaidi ili watu wasiingie kufanya shughuli katika maeneo hayo. Pili, watu wasiruhusiwe kufanya shughuli za kilimo katika maeneo hayo, na kuwe na alama zinazoonekana wazi ili kuwakumbusha kuwa katika eneo hilo imepita miundombinu ya kusafirisha nishati,” amesema.

Katika maelezo yake, Profesa Majule amesema ni lazima umma uelimishwe mara kwa mara kupitia serikali za mitaa ili kuepusha baadhi ya wananchi kujenga katika maeneo hayo kwa kisingizio kwamba hawakuwa na taarifa.

“Wananchi wasijenge karibu na miundombinu hiyo. Ikiwa tayari wamejenga, ni bora wakahamishwa. Najua ni gharama kubwa, lakini Serikali lazima ibebe mzigo huo,” amesema.

Profesa Majule ameongeza kuwa ikiwa wananchi wataendelea kufanya shughuli zao katika maeneo hayo, kwanza wanaweka hatarini miundombinu kuharibiwa. Aidha, ikitokea milipuko, vifo vinaweza kutokea.

“Itaharibu makazi na mali zao, na kama mafuta yatavuja yatasababisha ardhi kuchakaa au kuharibika, ikiwemo misitu, huku viumbe hai vingine vitaathirika katika mfumo mzima wa ikolojia,” anasema.