Dar City, Al Ahly kukiwasha tena leo BAL

WAKATI mashabiki wa mpira wa kikapu barani Afrika wakielekeza macho yao huko Afrika Kusini kwenye michuano ya Basketball Africa League (BAL), timu ya Dar City iko katika nafasi nzuri ya kuendeleza rekodi yake itakaposhuka dimbani leo, Jumanne kuvaana na Al Ahly Ly katika mchezo wa tatu.

Dar City inaingia Kalahari Conference, Pretoria saa 10:00 jioni ikiwa na ari kubwa baada ya kushinda mechi mbili za mwanzo (2-0).

Ushindi wa pointi 100-70 dhidi ya Johannesburg Giants ulionyesha uwezo mkubwa wa timu hiyo kushambulia na kumaliza mechi mapema na pia ilionyesha uimara wa kikosi kufuatia kutoka nyuma kwa zaidi ya pointi 10 na kuibuka na ushindi wa 90-85 dhidi ya Nairobi City Thunder.

Kinachoifanya Dar City kuwa tishio kwa wapinzani ni uwezo wa kufunga kwa kasi kwa wachezaji tofauti.

Nyota David Michineau ameibuka kuwa mhimili wa ushambuliaji baada ya kuongoza kwa pointi 39 katika mchezo uliopita huku pia akichangia pasi za mwisho na ‘rebounds’. Sambamba na hilo, Nisre Zouzoua ambaye ni fundi wa mitupio ya mbali ameongeza nguvu eneo la pembeni kwa uwezo wa kubadili mchezo.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, benchi la ufundi la Dar City linaloongozwa na Mamadou Gueye ‘Pabi’ lina kazi ya kuboresha upande wa ulinzi.

Unajua kwanini? katika mchezo dhidi ya Thunder, waliruhusu wapinzani kufika zaidi katika eneo lao hasa kipindi cha kwanza, hali iliyowalazimu kutumia nguvu kurudi mchezoni changamoto inayoweza kuwa hatari wanapokutana na Al Ahly ya Libya.

Upande wa Al Ahly Ly unaingia ukiwa katika presha baada ya kupoteza mechi mbili za mwanzo. Hata hivyo, Dar City haipaswi kuichukulia poa timu hiyo kwani wapinzani wao  wana wachezaji hatari kama  Jo Lual Acuil aliyeonyesha uwezo wa kufunga na kupora mipira.

Mchezo wa leo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, huku Dar City ikilenga kuibuka na ushindi ili kujihakikishia nafasi nzuri ya kusonga mbele, wakati Al Ahly ikisaka ushindi wake wa kwanza ili kufufua matumaini ya kusalia kwenye mashindano.

Kwa mtazamo wa jumla, Dar City inaonekana kuwa na makali zaidi kuelekea pambano hili, lakini mafanikio yao yatategemea uwezo wa kudhibiti kasi ya mchezo mapema na kuzuia makosa ya kiulinzi. Ikiwa watafanikiwa kufanya hivyo, wana nafasi kubwa ya kuendeleza rekodi yao ya ushindi na kujiweka karibu zaidi na hatua inayofuata.