SIMBA inaendelea kuonyesha ubabe wake kwenye usajili wa Ligi Kuu Bara kimyakimya ili kuhakikisha inapunguza presha wakati dirisha la usajili litakapofunguliwa.
Simba imeandaa mkakati mpya wa usajili kwa ajili ya msimu ujao ambapo uongozi wa timu hiyo unataka kuhakikisha unamaliza usajili wake mapema ikiamini kuwa kufanya hivyo kutawafanya wazizidi ujanja timu nyingine ambazo zitakuwa zinataka mastaa hao.
Tayari taarifa ambazo Mwanaspoti inazo timu hiyo imeshamalizana na kiungo mzawa Kelvin Nashoni kutoka kwenye kikosi cha Pamba ambacho alikuwa akikichezea kwa mkopo akitokea Singida BS ambayo anamaliza nayo mkataba mwishoni mwa msimu huu.
Uongozi wa timu hiyo umesema kuwa umekuwa na wakati mgumu kila inapowania mchezaji na klabu nyingine kubwa hapa nchini wakati dirisha linapofunguliwa hivyo kwa sasa hawataki kukutana tena na hali hiyo.
“Tuna nafasi chache sana za kujaza, baada ya kuwaongezea mikataba wachezaji wetu akiwemo Rushine De Reuck na Yusuph Kagoma tulianza kazi ya kuingiza sura mpya ambapo mpaka sasa tumesajili mchezaji mmoja tu ambaye ni Nashon, lakini tunataka kuhakikisha kuwa kabla dirisha halijafunguliwa tayari tuwe tumekamisha usajili wetu kwa kuwa tayari majina yapo kilisema chanzo kutoka Simba.
Chanzo hicho kilisema kuwa uongozi wao unataka hadi fainali za Kombe la Dunia zitakapoanza basi wawe wameshamalizana na suala la usajili na kazi iwe ni kuweka ratiba yao vizuri kuelekea maandalizi ya msimu mpya 2026/2027.
“Hatuna mpango wowote wa kusajili mchezaji kutoka kwenye fainali za Kombe la Dunia ingekuwa AFCON au CHAN sawa lakini huku wala hatufikiri, hivyo tunataka kumaliza kazi ya usajili mapema kwa kuwa tunataka pia timu iingie kambini mapema.”
Chanzo kimesema kuwa Simba inataka kusajili mshambuliaji mmoja kutoka nje, lakini itamrudisha kiungo wao Saleh Karabaka ambaye anacheza JKT Tanzania kwa mkopo huku ikiendelea kufanya tathimini kwa upande wa kipa wao namba moja Djibrilla Kassali ambaye alipewa mkataba mfupi na timu hiyo na bado hajaongezewa, huku Moussa Camara pamoja na kwamba yupo nje ya kikosi hicho lakini anahudumiwa na timu hiyo kwa kila kitu ikiwemo malazi, chakula, posho za mechi hadi mwishoni mwa msimu huu ambapo mkataba wake utamalizika.
“Camara bado anahudumiwa na timu, kila kitu anafanyiwa na timu hivyo naona kama ni mtego kwa Kassali kwa kuwa kwenye vikao kama vile bado uongozi unaona kama Camara akiwa fiti anaweza kuwa bora kuliko yeye, lakini ni suala la muda kwa kuwa mwishoni mwa msimu anamaliza mkataba na inawezekana ameshaanza mazungumzo sehemu nyingine.
“Mchezaji mwingine ambaye yupo na hajaondolewa kwenye kikosi na bado ni mali ya Simba ni Mohamed Bajaber mwisho wa msimu atarudi sasa mwalimu ndiye ataamua kama aondoke moja kwa moja au akatwe nani yeye aingie.’’
Hata hivyo, inelezwa kuwa mwishoni mwa msimu Simba inaweza kuachana na wachezaji watatu wa kigeni ambapo mmoja amekuwa akipata nafasi mara kwa mara na wengine wawili hawana nafasi ya kudumu kwenye kikosi hicho
Wachezaji wa kigeni waliopo Simba ni: Kassali, De Reuck, Ismael Touré, Alassane Kanté, Naby, Elie Mpanzu, Libasse Gueye,Clatous Chama, Jonathan Sowah,Anicet Oura, Bajaber, Neo Maema.
