Ligi ya Wanawake (WPL) inatarajiwa kurejea Aprili 03 kwa mechi za mzunguko wa pili, huku Simba Queens ikianza kampeni yao kwa kuvaana na Bilo Queens.
Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya kikosi cha Simba Queens zinaeleza kuwa kiungo mkabaji mpya, Alexandra Mbitounou Nke raia wa Cameroon, hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachocheza kutokana na majeraha yanayomsumbua kabla ya kutua klabuni hapo.
Chanzo hicho kimeeleza kuwa hali ya mchezaji huyo bado haijawa imara kiasi cha kuruhusiwa kucheza mechi za ushindani na wanasubiri ripoti ya daktari kujua ni muda gani atakaa nje.
“Ni kweli hatakuwa tayari kwa mechi ijayo. Bado anahitaji muda zaidi ili kupona kabisa, hatutaki kuhatarisha afya yake, ndiyo maana hatujamtambulisha tunafanya maamuzi kwanza,” kilisema chanzo hicho.
Dirisha dogo Simba Queens walifanya maboresho kwa kusajili wachezaji wawili muhimu wakilenga kuongeza nguvu katika kikosi hicho kinachowania ubingwa msimu huu.
Miongoni mwa waliosajiliwa ni mshambuliaji Ernestine Heutchou, ambaye tayari ametambulishwa rasmi na ameanza mazoezi na Nke ambaye bado hajatambulishwa.
Simba ilimsajili Nke baada ya beki wake Ester Mayala kufanyiwa upasuaji msimu uliopita uliomfanya akae nje miezi sita na kiungo Brice Zanga kuamishiwa nafasi hiyo.
Hivyo Nke alisajiliwa ili aweze kuziba nafasi ya Zanga ambaye alihamishiwa beki wa kati, lakini kurejea kwa Mayala kunahatarisha nafasi ya Mcameroon huyo.
Inaelezwa kama jeraha la Nke litakuwa kubwa kuna uwezekano mkubwa Simba ikavunja mkataba wake.
