Bunge laahirishwa, bajeti kusubiri kusomwa rasmi

Dodoma. Kikao cha kwanza cha mkutano wa tatu wa Bunge la 13 kimeahirishwa hatua inayosogeza mbele rasmi mchakato wa kuanza kusomwa kwa bajeti ya Serikali.

Hayo yamebainishwa leo Jumanne Machi 31, 2026 na Naibu Spika wa Bunge, Daniel Sillo, ambapo ametangaza kuahirishwa kwa kikao hicho bila kueleza sababu za moja kwa moja.

Bunge leo Machi 31,2026 limeonekana kuwa na idadi ndogo ya wabunge na mawaziri waliohudhuria.

Katika kikao hicho, Sillo amesoma taarifa ya Spika wa Bunge akiwajulisha wabunge kuhusu msiba wa Mbunge wa Ismani, William Lukuvi na kueleza kuwa maziko ya Lukuvi yanafanyika leo katika kijiji cha Idodi, mkoani Iringa, yakiongozwa na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba.

Lukuvi alifariki dunia Machi 25, 2026 katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Dodoma alikokuwa akipatiwa matibabu.

Naibu Spika aliwaomba wabunge kusimama kwa dakika moja kwa ajili ya kumkumbuka Lukuvi na walipokaa akamwomba Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi, Profesa Riziki Shemdoe kusoma hati za kuwasilisha mezani kwa niaba ya Waziri Mkuu ambaye hakuwepo.

Kwa sasa, macho yote yanaelekezwa kesho Jumatano Aprili Mosi, 2026, ambapo Waziri Mkuu atafungua pazia la kuanza usomaji wa bajeti yake.