Tel aviv. Iran imeshambulia na kuchoma moto tanki kubwa la mafuta ghafi karibu na pwani ya Dubai Jumatatu Machi 30, 2026, huku Rais Donald Trump akionya kuwa Marekani itaharibu kabisa mitambo ya nishati na visima vya mafuta vya Iran ikiwa nchi hiyo haitafungua Mlango-bahari wa Hormuz.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Machi 31, 2026 na Reuters zinaeleza shambulio hilo ni mfululizo wa mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara kwa kutumia makombora au ndege zisizo na rubani (drones) tangu Marekani na Israel zilipoishambulia Iran mnamo Februari 28, 2026.
Pia shambulio hilo linakuja baada ya msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kuelezea mapendekezo ya amani ya Marekani kuwa hayana mantiki.
Kupitia mitandao ya kijamii, Trump ametoa onyo jipya akisema ikiwa makubaliano hayatofikiwa hivi karibuni na Mlango-bahari wa Hormuz kutofunguliwa, Marekani itamalizia ‘ziara’ yake nchini Iran kwa kulipua na kuharibu kabisa vituo vyote vya kuzalisha umeme, visima vya mafuta, na Kisiwa cha Kharg.
Shirika la Mafuta la Kuwait (KPC), ambalo ndilo mmiliki wa tanki hilo, limesema shambulio limetokea mapema Jumanne na kusababisha moto na uharibifu wa ganda la meli, lakini hakuna majeruhi wala vifo vilivyoripotiwa. Mamlaka nchini Dubai baadaye zilisema zimefanikiwa kuudhibiti moto huo.
Mgogoro huu wa mwezi mmoja umeenea kote Mashariki ya Kati, ukiua maelfu ya watu, kuvuruga usambazaji wa nishati, na kutishia kuingiza uchumi wa dunia katika msukosuko mkubwa. Bei ya mafuta ghafi ilipanda kwa muda mfupi baada ya shambulio dhidi ya tenki hilo lenye uwezo wa kubeba mapipa milioni mbili ya mafuta yenye thamani ya zaidi ya dola milioni 200.
Kupanda kwa bei ya mafuta kumeanza kuathiri uchumi wa kaya nchini Marekani, ambapo wastani wa bei ya petroli nchini humo ulivuka dola 4 kwa galoni siku ya Jumatatu kwa mara ya kwanza kwa zaidi ya miaka mitatu.
Hata hivyo, ripoti za gazeti la Wall Street Journal inaeleza, Trump amewaambia wasaidizi wake kuwa yupo tayari kusitisha kampeni ya kijeshi hata kama mlango-bahari utabaki umefungwa kwa kiasi fulani, jambo ambalo lilisaidia kwa kiasi kidogo kutuliza soko la mafuta.
Endelea kufuatilia Mwananchi
