Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi, Hassan Saidy amewataka Watumishi wa Wakala kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kuhakikisha ndani ya muda uliopangwa wanafikisha umeme kwenye vitongoji vyote vya Tanzania Bara.
Ametoa maelekezo hayo Makao Makuu ya REA, Jijini Dodoma wakati wa kikao kazi na Watumishi wote, ambapo amesema baada ya kusaini Mradi mkubwa wa HEP II (B); Mradi wa kusambaza umeme kwenye vitongoji 9,009 tarehe 17 Januari, 2026 na kuongeza kuwa kazi iliyombele ya kila Mtumishi ni kuhakikisha vitongoji hivyo vinafikishiwa umeme katika kipindi cha miaka mitatu yaani hadi 2029.
Mhandisi Saidy amesema kukamilika kwa Mradi huo wa HEP II (B) pamoja na miradi mingine inayoendelea kutafanya jumla ya vitongoji ambavyo tayari vitakuwa vimefikishiwa umeme kuwa takriban 51,000 kufanya vitongoji vitakavyobakia bila umeme na bila kuwa katika mradi wowote kuwa taklibani 13,000 ambavyo vimepangwa kuanza kusambaziwa umeme ifikapo mwaka 2030 kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2025 – 2030.
Awali ilielezwa kuwa Mradi huo wa HEP II (B) ni muendelezo wa jitihada za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) za kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya umeme kwa Wananchi wote wa Tanzania Bara.
Mradi huo unatarajiwa kutoa manufaa ya moja kwa moja kwa Wananchi kwa kuongeza upatikanaji wa huduma ya umeme vitongojini; kuboresha huduma za kijamii hususan katika sekta za afya, elimu na maji; kuwezesha matumizi ya umeme katika shughuli za uzalishaji na kuongeza kipato cha Wananchi pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi wa maeneo ya vitogojini pamoja na kuimarisha ustawi wa jamii.
Aidha; Mhandisi, Saidy aliongoza Watumishi wa REA katika zoezi la kuchagua Viongozi wa TUGHE tawini hapo ambapo kwa kauli moja Watumishi waliwachagua Viongozi wao katika ngazi tofauti kama ifuatavyo: – Mwenyekiti wa Tawi ni Swalehe Kiloza, Katibu wa Tawi ni Mhandisi, Annet Malingumu; Mjumbe wa Halmashauri ya Tawi ni Bwana Issa Sabuni na Mwakilishi wa Kundi la Vijana, Mhandisi, Issac Sanga.
Viongozi wengine ni pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Wanawake ya Tawi la TUGHE REA ni kama ifuatavyo: – Mwenyekiti ni Wilhelmina Cheyo; Katibu ni Ruth Emmanuel; Mweka Hazina ni Bi. Aveline Wilfred; Wajumbe Kamati ya Wanawake ni Bi. Happiness Ndunguru na Mhandisi, Bertha Mwaituka.
Vilevile Watumishi wa REA pia walichagua Viongozi kwa upande wa Klabu ya Michezo ya REA ambapo itaongozwa na Bwana Selemani Mtunzy kama Mwenyekiti na Mwenyekiti Msaidizi ni Bwana Samwel Sumwa; Katibu ni Bwana Praygod Ng’hunda; Mweka Hazina ni Bwana Daniel Kisaka wakati Wajumbe wa Kamati Tendaji kwa upande wa Wanaume atakuwa Mhandisi, Thomas Mmbaga na kwa upande wa Wanawake atakuwa Bi. Beatrice Shelukindo.
.jpeg)
.jpeg)

