Ngorongoro kutumia AFCON kutangaza utalii

MAMLAKA ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), imesema imejipanga kutumia fursa ya mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2027), kutangaza vivutio vya utalii na historia ya kipekee ya eneo hilo, ikiwemo chimbuko la mwanadamu katika eneo la Laetoli mkoani Arusha.

Akizungumzia msimu wa 11 wa shindano la Safari Field Chalenji linalohusisha waongoza watalii, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Huduma na Masoko wa NCAA, Mariamu Kobelo amesema mamlaka hiyo imeanza maandalizi ya kutumia mashindano hayo makubwa ya soka kama jukwaa la kuitangaza Tanzania kwa wageni wa ndani na nje ya nchi watakaofika kushuhudia michuano hiyo.

Amesema NCAA inalenga kuunganisha hamasa ya mpira wa miguu wa kisasa na historia ya kale ya mwanadamu ili wageni watakaokuja kwa ajili ya AFCON wapate pia fursa ya kufahamu urithi wa kipekee uliopo Ngorongoro.

Kwa mujibu wa Kobelo, eneo la Laetoli lina umuhimu mkubwa wa kihistoria duniani kutokana na kuwa na ushahidi wa mwanadamu wa kwanza kutembea kwa miguu miwili, jambo linalolifanya kuwa moja ya maeneo muhimu ya urithi wa dunia.

“Tunataka watu watambue kuwa mbali na soka, Tanzania pia ina historia kubwa ya mwanadamu na vivutio vya kipekee vya utalii vinavyopatikana Ngorongoro,” amesema.

Amesema AFCON ni nafasi muhimu kwa taasisi za utalii nchini kujitangaza kwa kiwango kikubwa zaidi kutokana na idadi ya wageni na wadau mbalimbali wanaotarajiwa kufika nchini wakati wa mashindano hayo.

Kobelo ameongeza kuwa NCAA imejipanga kuhakikisha wageni watakaotembelea eneo la Ngorongoro wanapata uzoefu wa kipekee wa kuona kwa pamoja wanyamapori, mandhari ya asili, historia ya mwanadamu na urithi wa utamaduni wa Tanzania.