Arusha. Mahakama ya Rufani imebariki adhabu ya kunyongwa hadi kufa iliyotolewa dhidi ya watu wanne waliokutwa na hatia ya kumuua Rashid Hassan, kisha kuutelekeza mwili wake kwenye mto Kyarano.
Uamuzi uliotupilia mbali rufaa hiyo ulitolewa Machi 26, 2026 ambapo Mahakama baada ya kuchambua hoja za pande zote ilibaini nyingi za warufani zilikuwa na mapungufu ya kisheria na hazikuwa na athari kwa msingi wa kesi ya upande wa mashtaka.
Warufani hao waliokuwa wakipinga hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, iliyotolewa Oktoba 10, 2023 ni John Mbatira, Sadick Shaban, Manga Mgonoki na Steven Augustino.
Majaji waliotoa uamuzi huo ni Dk Gerald Ndika, Patricia Fikirini na Mustafa Ismail ambapo Mahakama hiyo iliridhika kuwa upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi wa kutosha kuthibitisha hatia ya warufani hao bila kuacha shaka yoyote.
Miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na hoja kuwa ushahidi wa shahidi mmoja wa upande wa mashtaka uliwasilishwa kinyume cha sheria kwa madai kuwa hakutajwa katika hatua za awali za kesi, ambapo Mahakama hiyo ilibaini upande wa mashtaka ulitoa taarifa kuhusu shahidi huyo kabla ya kuwasilishwa mahakamani hivyo alikidhi matakwa ya kisheria.
Sababu nyingine iliyowasilishwa ilikuwa ni baadhi ya vielelezo vilikamatwa kinyume cha sheria ambapo Mahakama hiyo iliona hoja hiyo haina umuhimu baada ya kuondoa kielelezo husika katika ushahidi, hivyo hakukuwa na athari katika uamuzi wa mwisho.
Mauaji hayo yalitokea Juni 30, 2022 katika kijiji cha Mwanzaburiga, Wilaya ya Butiama mkoani Mara ambapo mwili wa marehemu ulipatikana ukielea katika Mto Kyarano.
Uchunguzi wa kitabibu uliofanywa na daktari ulithibitisha kuwa marehemu alikufa kutokana na majeraha makubwa kichwani yaliyosababishwa na kupigwa kwa vitu butu, hali iliyopelekea kuvuja kwa damu nyingi na kuharibu ubongo.
Kumbukumbu za Mahakama zinaonyesha upande wa mashtaka katika kuthibitisha kesi yake ulitegemea nguzo tatu kuu za ushahidi, ambazo ni ushahidi wa kimazingira unaoonyesha marehemu mara ya mwisho alikuwa na warufani usiku kabla ya mwili wake kukutwa ukielea kwenye mto kesho yake.
Pia, mrufani wa kwanza, pili na nne walikiri kosa hilo na kumuhusisha mrufani wa tatu na kuwa mrufani wa tatu alikutwa na mkanda unaoaminika kuibiwa kutoka kwa marehemu wakati wa kifo chake.
Mashahidi wawili, waliotambulika kama shahidi wa tatu na nne, waliieleza Mahakama kuwa waliwaona warufani wakiwa pamoja na marehemu wakitembea na baadaye wakinywa pombe katika eneo moja kabla ya tukio.
Shahidi mmoja alieleza kuwa alimwona marehemu akiingia nyumbani kwa mmoja wa warufani na baadaye akiwa katika kundi la watu waliokuwa wakinywa pombe.
Shahidi mwingine alieleza kuwa aliwaona wote wakiwa pamoja barabarani usiku huo, wakielekea upande wa mpaka wa Buturi na Mwanzaburiga.
Nguzo ya pili ya ushahidi ilikuwa ni maungamo yaliyotolewa na warufani watatu kati ya wanne, ambao walikiri kushiriki katika mauaji hayo na kutoa maelezo ya jinsi walivyopanga na kutekeleza tukio hilo.
Katika maungamo hayo, waliieleza polisi kuwa walimshambulia marehemu kwa kutumia rungu na mawe kabla ya kutupa mwili wake mtoni.
Mahakama ilieleza kuwa maungamo hayo, licha ya warufani kuyakana baadaye wakidai yalipatikana kwa mateso, yalithibitishwa na ushahidi huru uliotolewa mahakamani, ukiwemo wa mashahidi na ripoti ya daktari.
Nguzo ya tatu ilikuwa ni kielelezo cha mkanda uliodaiwa kupatikana kwa mmoja wa warufani, ambao ulitambuliwa kuwa ni mali ya marehemu.
Hata hivyo, Mahakama ya Rufaa ilibaini kuwa ushahidi huo haukukamilika ipasavyo kwa kuwa shahidi muhimu aliyepaswa kuthibitisha umiliki wa mkanda huo hakuwasilishwa mahakamani. Kutokana na upungufu huo, mahakama iliamua kupuuza kielelezo hicho.
Katika rufaa hiyo warufani walikuwa na sababu kadhaa ambapo mrufani wa kwanza hadi wa tatu, ambao waliwakilishwa na wakili mmoja, sababu zao ilikuwa ni Mahakama ilitegemea vibaya ushahidi uliotolewa na shahidi wa tano na kielelezo cha pili alichotoa, kwani hakutajwa awali wakati wa kuhamisha kesi kuwa atakuwa miongoni mwa mashahidi.
Nyingine ni upande wa mashtaka ulishindwa au ulipuuza kwa kiasi fulani kutoa mashahidi muhimu na shtaka dhidi yao halikuthibitishwa kwa kiwango kinachohitajika.
Mrufani wa nne aliyewakilishwa na wakili wake, alikuwa na sababu mbili ambazo ni maelezo ya onyo hayakuwa kamili na shtaka dhidi yake halikuthibitishwa.
Mahakama ilieleza kuwa ushahidi wa “kuonekana mara ya mwisho” ukiunganishwa na maungamo ya warufani uliunda mnyororo kamili wa ushahidi unaoonyesha bila shaka kuwa walihusika katika mauaji hayo.
Kuhusu hoja ya baadhi ya mashahidi muhimu kutokuitwa mahakamani, ushahidi fulani uliwasilishwa kinyume cha sheria, na kuwa hatia yao haikuthibitishwa kwa kiwango kinachotakiwa kisheria. Hata hivyo, mahakama ilitupilia mbali hoja hizo zote.
Jaji Ndika amesema mahakama ilikubaliana kuwa kulikuwa na upungufu, lakini ikaona haukuathiri msingi wa kesi ya upande wa mashtaka kwa kuwa ushahidi mwingine uliwasilishwa kwa kina na kwa kuaminika.
Aidha, mahakama ilikubaliana na Mahakama Kuu kwamba mauaji hayo yalifanyika kwa kukusudia, ikizingatia namna yalivyotekelezwa walivyotumia nguvu kubwa kumpiga sehemu nyeti za mwili wake, na baadaye kutupa mwili wake mtoni ili kuficha ushahidi.
Kwa msingi huo, Mahakama ilihitimisha kuwa kosa la mauaji lilithibitishwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria na ushahidi uliotolewa.
“Tumejiridhisha kwamba rufaa hii haina msingi wowote wa kisheria, na hivyo tunaikataa ,” ilieleza sehemu ya uamuzi wa Mahakama.
