Global Publishers
March 31, 2026
0 Comments
Serikali imeeleza sababu za kuongezeka kwa gharama za ujenzi wa uwanja wa mpira unaojengwa mkoani Arusha, ambapo sasa zimefikia shilingi bilioni 338.54 kutoka makadirio ya awali ya shilingi bilioni 187.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema kuwa ongezeko hilo linatokana na maboresho yaliyolazimika kufanyika ili kukidhi viwango vya kimataifa vilivyowekwa na Confederation of African Football (CAF).
Amefafanua kuwa mabadiliko hayo yalihusisha kuboresha miundombinu ya uwanja huo, ikiwemo huduma za kisasa, usalama, pamoja na uwezo wa kuhimili mashindano makubwa ya kimataifa.
Msigwa alibainisha kuwa awali mradi wa ujenzi wa uwanja huo ulianza mwaka 2021, kabla ya Tanzania kuteuliwa kuwa mmoja wa waandaaji wa michuano ya Africa Cup of Nations 2027 (AFCON 2027). Hivyo, uteuzi huo umeongeza mahitaji mapya ya kiufundi na ubora wa miundombinu inayojengwa.

Amesisitiza kuwa licha ya ongezeko hilo la gharama, lengo kuu la Serikali ni kuhakikisha uwanja huo unakidhi viwango vya juu vya kimataifa na kuwa tayari kwa matumizi ya mashindano makubwa, ikiwa ni pamoja na AFCON 2027.
Mradi huo unatarajiwa kuwa miongoni mwa viwanja muhimu vitakavyotumika katika mashindano hayo, huku ukichangia kukuza sekta ya michezo na utalii katika mkoa wa Arusha na Tanzania kwa ujumla.
Ujenzi wa uwanja huo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali kuboresha miundombinu ya michezo nchini ili kuiweka Tanzania katika ramani ya kimataifa ya soka na matukio makubwa ya michezo.