Dodoma. Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amezuia kutangazwa kwa bei ya makaa ya mawe bila kushirikisha wadau, akisisitiza hatua hiyo inalenga kuongeza uwazi na kulinda masilahi ya wachimbaji na wasafirishaji wa rasilimali hiyo.
Mavunde ametoa maagizo hayo Machi 30, 2026, alipokuwa akizungumza katika mkutano wa kwanza wa wadau wa biashara ya makaa ya mawe uliofanyika jijini Dodoma, uliolenga kujadili changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
Hatua hiyo, imekuja kufuatia malalamiko ya wadau waliolalamikia ongezeko la gharama za uendeshaji wa biashara hiyo, hususan tozo mbalimbali zikiwemo gharama za usafirishaji kutoka migodini hadi mipakani.
Tozo zingine ni ada za ukaguzi wa madini, pamoja na tozo za barabara na bandari zinazotozwa kulingana na uzito wa mzigo.
Katika maelekezo yake, Mavunde ameagiza Tume ya Madini Tanzania kufanya uchambuzi wa kina kuhusu mfumo wa tozo, ikiwemo mrabaha, na kuwasilisha mapendekezo haraka kwa ajili ya hatua zaidi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa majadiliano kati ya Wizara ya Madini na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kupitia upya tozo za usafirishaji kabla ya kufikia uamuzi wa mwisho, hatua inayolenga kupunguza malalamiko na kuimarisha ufanisi wa sekta hiyo.
Akizungumzia mwenendo wa baadhi ya wafanyabiashara kubadilisha bei kiholela, Mavunde amesema tabia hiyo inavuruga ushindani wa soko na kuathiri utulivu wa bei.
“Kuanzia sasa, hakuna bei itakayotangazwa bila kuwashirikisha wadau. Ni muhimu kwa kila mdau kufahamu bei halisi ya soko ili kuepusha migongano isiyo ya lazima, kwa kuwa kila mmoja anamtegemea mwenzake,” amesema.
Awali, mshauri wa Chama cha wauzaji na wasafirishaji wa makaa ya mawe nchini, Rahim Bhanj, aliitaka Serikali kuingilia kati ili kupunguza mzigo wa tozo unaowakabili wafanyabiashara, akisema hali hiyo inaathiri ufanisi wa biashara.
Bhanj, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Bhanj Transport Ltd, alipendekeza kufanyika marekebisho ya mfumo wa tozo ili zipunguzwe na kubaki katika vituo vya mipakani, hatua itakayopunguza gharama katika mnyororo mzima wa biashara.
Aidha, alieleza kuwa bado kuna changamoto ya kutotambulika kwa mrabaha wa asilimia tatu ya mauzo ya makaa ya mawe kama sehemu ya kodi, akisisitiza umuhimu wa utambuzi huo ili kuleta uwiano katika mfumo wa kodi.
Wadau hao pia wamesisitiza umuhimu wa uwazi wa taarifa za bei, wakieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza hasara zisizo za lazima na kuwezesha wafanyabiashara kufanya maamuzi sahihi kwa kuzingatia hali halisi ya soko.
