Miundombinu chakavu, mivujo yatikisa upatikanaji wa maji

Dar es Salaam. Kwa baadhi ya wakazi kupata maji mikoa mbalimbali nchini imekuwa kama bahati nasibu, leo yanatoka kwa shida, kesho mabomba yanavuja bila msaada wa haraka.

Changamoto hii imebainishwa kupitia ripoti mpya ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), inayoonyesha kati ya malalamiko 463,740 yaliyowasilishwa, asilimia 58.6 yanatokana na mivujo na presha hafifu ya maji.

Malalamiko hayo yapo kwenye Ripoti ya Utendaji wa Mamlaka za Maji Safi na Usafi wa Mazingira kwa mwaka wa Fedha 2024/25 iliyozinduliwa Machi 19, 2026 mkoani Morogoro na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.

Katika ripoti hiyo, ilionyesha asilimia 12.6 ya malalamiko yote  yalihusu majitaka, asilimia 11.5 ankara na dira za maji, asilimia 4.5 maunganisho ya maji na asilimia 12.8  mambo mengineyo.

Wakati ripoti ikibaini hayo, Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Maji kwa Mwaka 2025/26 Serikali ilieleza hatua za kukabiliana na changamoto hizo.

Hatua hizo ni kupunguza malalamiko ya wateja kwenye ankara za maji, kuongeza ufanisi kwenye ukusanyaji wa maduhuli ni kuhakikisha wateja wa maji wanafungiwa dira za maji za malipo kabla ya matumizi.

Dira hizo zitasaidia kuongeza ufanisi wa matumizi ya maji pamoja na kudhibiti mivujo inayosababisha hasara kwa mteja.

“Hadi Aprili 2025, jumla ya wateja 16,809 wamefungiwa dira za maji za malipo kabla ya matumizi kati ya wateja 2,019,951 wa vijijini na mijini.

“Kwa upande wa Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira jumla ya wateja 13,282 wamefungiwa dira hizo na kwa upande wa vijijini, Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa)  imefunga jumla ya dira 3,527 kwenye mikoa mbalimbali,” taarifa hiyo ya bajeti ilieleza.

Katika kutatua malalamiko ya wananchi kuhusu maji, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) 2025-2030, imepanga kuondoa adha ya upatikanaji wa maji kwa kuhakikisha angalau asilimia 90 ya kaya nchini zinafikiwa na maji safi na salama.

Hii itafanyika kupitia Mpango Kabambe wa Taifa wa Maji na ujenzi wa Mtandao wa Taifa wa Maji (National Water Grid) utakaotumia vyanzo vikubwa kama Ziwa Victoria kupeleka maji mikoa yenye ukame kama Singida na Dodoma.

Akitoa suluhu ya malalamiko kwenye sekta ya maji, mchambuzi wa masuala ya uchumi, Tumaini Munale anasema, Serikali inapaswa kufanya uwekezaji wa kimkakati katika ukarabati na uboreshaji wa mabomba chakavu (pipe replacement programs) na matumizi ya teknolojia za kisasa za kugundua mivujo.

Anasema hatua hiyo itapunguza upotevu wa maji na kuongeza ufanisi wa usambazaji.

“Mamlaka za maji zinapaswa kuimarisha mifumo ya usimamizi wa shinikizo la maji, maeneo mengi hupata msukumo hafifu kutokana na upangaji usio sahihi wa mitandao au matumizi makubwa yasiyodhibitiwa,”anasema.

Munale anataja jambo lingine ni kuimarisha huduma kwa wateja kupunguza malalamiko yanayohusu ankara, dira na majitaka.

Anasema matumizi ya dira za malipo kabla ya matumizi mifumo ya kidijitali ya kutoa bili sahihi na majibu ya haraka kwa malalamiko ni suluhisho muhimu.

Pia, elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya maji na namna ya kusoma dira itasaidia kupunguza migogoro.

“Serikali inapaswa kuimarisha ukaguzi wa mara kwa mara, kuweka viwango vya utendaji (performance benchmarks) na kuhakikisha mamlaka za maji zinawajibika kwa matokeo na sisi maneno,” anasema.

Kwa upande wake, Dk Reubeni Lumbagala anasema ili kupunguza malalamiko kwenye upotevu wa maji miundombinu yote mibovu iondolewe.

“Kuna umuhimu wa kuanzisha mifumo jumuishi ya usimamizi wa rasilimali za maji inayounganisha vyanzo vya maji, miundombinu na mahitaji ya watumiaji,”anasema

Kwenye sekta ya maji, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere juzi alipokuwa akiwasilisha ripoti yake ya ukaguzi kwa Rais Samia Suluhu Hassan ya mwaka 2024/25, alisema upotevu wa maji umeendelea kuisababishia Serikali hasara.

Amesema kwa mwaka 2024/25 upotevu wa maji umeongezeka kufikia asilimia 35 kutoka asilimia 32.

Kiwango hicho kipo juu ya lengo la kitaifa la kutozidi asilimia 20 hali iliyosababisha hasara ya Sh248.78 bilioni huku baadhi ya mamlaka zikiwa na kiwango kikubwa cha upotevu wa maji.

“Same-Mwanga kama anazalisha asilimia 100 ya maji asilimia 70 yanapotea, Dar es Salaam asilimia 53 ya maji yanayozalisha yanapotea, Morogoro  asilimia 50 yanapotea kwa maana hiyo asilimia kubwa hayafikii wananchi  au yanayowafikia hayatozwi,”alisema CAG Kichere.

Alisema chanzo kikubwa cha tatizo ni miundombinu chakavu na wizi wa maji, hali inayoathiri uendelevu wa mapato mamlaka za maji na kupunguza upatikanaji wa huduma na kutegemea ruzuku Serikalini.

“Napendekeza Serikali iimarishe uwekezaji katika ukarabati na uboreshaji wa  miundombinu ya maji, mifumo ya upotevu wa maji na kuchukua hatua ya miunganisho haramu kupunguza hasara na kuongeza ufanisi wa sekta.”

Undani wa ripoti ya Ewura

Kulingana na ripoti ya Ewura, malalamiko 306,156 sawa na asilimia 66 yalitatuliwa kikamilifu ikilinganishwa na asilimia 61 kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Aidha, kati ya malalamiko hayo yaliyotatuliwa, asilimia 82 yalitatuliwa ndani ya siku tano za kazi kwa mujibu wa kanuni za Ewura za Maji na Usafi wa Mazingira (Leseni na Ubora wa Huduma) za Mwaka 2020.

“Uchambuzi unaonesha kuwa kumekuwa na maboresho katika kushughulikia na utoaji wa huduma kwa wateja.

“Maendeleo zaidi yatategemea uimarishaji wa mifumo ya ufuatiliaji wa malalamiko kwa wakati, upatikanaji wa rasilimali na watumishi wa kutosha katika vitengo vya huduma kwa wateja, pamoja na kuimarisha mifumo ya uwajibikaji kupitia ukaguzi wa utendaji na tathmini za mrejesho wa wateja,”taarifa hiyo ilionyesha.

Ewura inapendekeza ili kuimarisha huduma kwa wateja, mamlaka za maji zinapaswa kuwa na mikataba ya huduma kwa wateja, pamoja kupokea na kushughulikia malalamiko yao.

Uchambuzi wa vigezo vyao unaonyesha kuwa ni mamlaka za maji 73 sawa na asilimia 88 zilikuwa na mikataba ya huduma kwa wateja iliyoidhinishwa.