Dar/Mikoani. Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na viongozi wa waendesha bodaboda limeanza operesheni maalumu ya kukamata vyombo vya moto vinavyofunga taa kali kupita kiwango na kuhatarisha watumiaji wengine wa barabara.
Barabara kuu na za pembezoni mwa miji zimekumbwa na kadhia hiyo ya taa zisizo na viwango, baada ya baadhi ya madereva kuongeza taa za ziada mbele ya magari yao au kubadilisha mfumo wa taa za kiwandani kwa madai ya urembo au kuongeza mwanga.
Baadhi ya madereva wa pikipiki, bajaji na magari wanasema mwanga huo mkali unapokutana nao hupunguza uwezo wa kuona kwa sekunde kadhaa na unaweza kusababisha ajali.
Mara kadhaa Mwananchi imeandika kuhusu kadhia ya ufungaji wa taa hizo, ambapo wadau mbalimbali walikemea hali hiyo. Mambo mengine yanayolalamikiwa ni ufungaji wa honi zenye sauti kubwa na kelele za muziki kwenye pikipiki na bajaji.
Kutokana na malalamiko hayo, Polisi wameanza operesheni katika baadhi ya mikoa ikiwemo Arusha, ambako tayari wamekamata taa 248 za aina mbalimbali zisizokidhi viwango.
Machi 29, 2026, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, William Mkonda aliiambia Mwananchi kuwa tayari ametoa maelekezo kwa vikosi vya usalama barabarani kote nchini kuchukua hatua.
“Tayari nimemwagiza RTO wa Kilimanjaro kushughulikia suala hili, na zoezi linaendelea sambamba na utoaji elimu kwa watumiaji wa barabara kwa kushirikiana na vyama vyao,” amesema Mkonda.
Amesema lengo si kuchukua hatua za kisheria pekee, bali pia kuhakikisha madereva na waendesha vyombo vya moto wanaelewa madhara ya kutumia taa zisizokidhi viwango.
Maelekezo hayo yametolewa mahsusi kwa mkoa wa Kilimanjaro baada ya baadhi ya madereva kuonekana kwenye mitandao ya kijamii wakipinga operesheni hiyo.
Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Bodaboda Wilaya ya Arusha, Shaibu Hamis amesema wamekuwa wakikamata pikipiki zinazosababisha kero za taa na kelele, huku wakitoa elimu kwa waendesha.
“Hakuna anayependezwa na jambo hili. Ukichunguza, asilimia kubwa wanaofanya hivyo ni vijana wa miaka 25 kushuka chini, na wengi hawana elimu ya madhara yake. Pia wahusika wengi hawapo kwenye vituo rasmi vya bodaboda,” amesema.
Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Bodaboda jijini Mbeya, Aliko Fwano amesema pamoja na juhudi za uhamasishaji, mamlaka za Serikali zina jukumu kubwa zaidi la kukomesha tatizo hilo.
“Hawa vijana wanaona ni fursa ya biashara. Kama zinakera, Serikali inapaswa kudhibiti kuingizwa na kuuzwa kwa vifaa hivyo,” amesema.
Kwa upande wake, dereva wa gari dogo mjini Morogoro, Juma Ng’ondavi, amesema amenusurika ajali mara kadhaa kutokana na taa kali za bodaboda na hivyo anaomba Serikali idhibiti biashara na matumizi ya taa hizo.
Hata hivyo, dereva bodaboda Onesmo Barton amesema taa hizo zinawasaidia kuonekana barabarani na kuongeza usalama wao.
“Pikipiki mara nyingi hudharaulika barabarani. Hizi taa zinasaidia tuonekane kirahisi. Pia maeneo ya nje ya mji zinasaidia kuona hatari mapema,” amesema.
Mkazi wa Mbeya, Oliver Mwakipesile, amesema taa hizo huwapa hofu watumiaji wa barabara hasa usiku, wakidhani ni wahalifu.
Msemaji wa Chama cha Waendesha Bodaboda Zanzibar, Mohamed Mahmoud Khamis, amesema hawaruhusu matumizi ya taa hizo, lakini baadhi ya madereva wamekuwa wakikaidi.
“Sio matakwa ya chama, bali ni vijana wanaoendeshwa na mihemko. Ni vigumu kufuatilia kila chombo, lakini hakuna sheria inayoruhusu kufanya hivyo,” amesema.
Dereva na mkazi wa Mwanza, Abdulrahim Mkewa, amesema taa hizo ni hatari hasa kwa madereva wasio na uzoefu.
“Ukikutana na gari lenye taa hizi unaona kama giza. Akiwasha mara mbili unapoteza kabisa mwelekeo na unaweza kupata ajali,” amesema.
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha, Georgina Matagi, amesema operesheni hiyo inalenga kuimarisha usalama barabarani.
Amesema baadhi ya taa hizo zina mwanga mkali unaofanana na ule wa magari makubwa, hali inayoweza kuwapotosha madereva wengine.
“Zipo taa tunaziita ‘macho ya bundi’. Pikipiki ikifunga taa mbili za aina hiyo, dereva wa gari anaweza kudhani ni gari linakuja, kumbe ni pikipiki. Hii imechangia ajali nyingi,” amesema.
Matagi amesema pia wamebaini baadhi ya waendesha bodaboda wanaficha namba za usajili kwa kuweka majina ya utani au alama zisizoeleweka, hali inayochochea uhalifu.
“Unakuta pikipiki imehusika na uhalifu, lakini namba imefichwa. Inakuwa vigumu kuitambua na ni hatari kwa jamii,” amesema.
Ameongeza kuwa operesheni hiyo pia inalenga kudhibiti kelele zinazotokana na mifumo ya honi iliyofanyiwa mabadiliko kinyume cha sheria.
Katika operesheni hiyo, madereva wanaokamatwa hulazimika kuondoa vifaa visivyokubalika kabla ya kuruhusiwa kuondoka, huku wanaokiuka sheria wakitozwa faini kulingana na makosa yao.
Matagi amesema licha ya baadhi ya madereva kutumia hadi Sh80,000 kununua taa hizo, wengi wao hawana hata leseni halali ya udereva yenye thamani ya takribani Sh70,000.
“Unakuta bodaboda zaidi ya 200, lakini wenye leseni ni wachache. Badala ya kuwekeza kwenye usalama, wanawekeza kwenye vifaa hatarishi,” amesema.
Kwa upande mwingine, Kamanda wa Usalama Barabarani Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Hamis Mwakanolo, amesema operesheni hiyo inaendeshwa nchi nzima kwa maagizo ya Mkuu wa Jeshi la Polisi.
“Nasi tunaendelea na operesheni kila siku. Wapo wanaotukimbia, lakini tukiwakamata tunawachukulia hatua,” amesema.
“Tumekuwa tukipokea malalamiko mengi kuhusu taa hizi zisizo salama. Tunawasihi madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani,” amesema.
Kilio cha wafanyabiashara
Wakati operesheni hiyo ikiendelea, wafanyabiashara wa vifaa vya pikipiki, wamesema hatua hiyo ingeanzia kwenye uingizaji wa mizigo, wakidai wameingiza bidhaa hizo kihalali na kulipia kodi zote stahiki.
Mfanyabiashara wa jumla na rejareja wa vifaa vya pikipiki katika soko la Kariakoo, Salum Mussa amesema kuwakamata waliofunga si tatizo, lakini wangeanzia ukaguzi kwa waagizaji kabla ya wafanyabiashara kupata hasara.
“Sisi tunaingiza mzigo kihalali kabisa, tunalipia kodi, Serikali imeruhusu bidhaa ziingie, lakini baadaye zinapigwa marufuku mtaani, hii inakuja kutuumiza sisi kiuchumi na kutupa hasara,” amesema Mussa.
“Wateja wetu wakuu ni bodaboda na bajaj kwa magari sio sana kwa sababu asilimia kubwa yanajulikana, sasa wanapoambiwa wazitoe au wanakamatwa wanarudi kwetu kwamba kwa sasa hazitauzika kama awali, hivyo tutajikuta tunabaki na mzigo sokoni,” amesema.
Fundi pikipiki eneo la Tabata, jijini Dar es Salaam, Hassan Said amesema kuna haja ya mamlaka kutoa elimu mapema kabla ya kuchukua hatua ili kuepusha hasara kwa wafanyabiashara .
Amesema hata Serikali inatakiwa kutoa mwongozo wa bidhaa zinazoruhusiwa ili wafanyabiashara wasiagize zisizoruhusiwa na kuishia kupata hasara.
“Tatizo kubwa si kila dereva amepitia mafunzo au darasani kujua matumizi sahihi ya taa, ndiyo maana unaona wengi hawana leseni na wanatumia taa hizo bila kuelewa madhara yake,” amesema.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusupu Mwenda amesema kila muagiza mzigo lazima awe na kibali na hakuna kibali kinachotolewa kwa bidhaa zisizoruhusiwa nchini.
Amesema kwa wale wenye ushahidi mzigo wao uliingia kihalali wawasilishe kwenye mamlaka zinazohusika, kama waliingiza kwa njia ya magendo hilo jambo halikubaliki.
“Hata hivyo na sisi tutaendelea kusimamia kuhakikisha bidhaa zisizoruhusiwa haziingizwi sokoni,” amesema Mwenda.
(Imeandikwa na Devotha Kihwelo (Dar), Janeth Mushi (Arusha), Saada Amir (Mwanza), Jesse Mikofu (Zanzibar),Hamida Sharif (Morogoro), Saddam Sadick (Mbeya) na Samwel Mwanga (Simiyu).
