Dk Mwigulu awaweka matumbo joto watendaji Iringa, atangaza ziara

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba ametangaza mpango wa kufanya ziara mkoani Iringa huku akieleza kutoridhishwa na sheria ya maegesho iliyotungwa katika maeneo ya mkoa huo, akisema inaleta mzigo kwa wananchi na inaweza kuwaumiza kiuchumi.

Dk Mwigulu  ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Machi 31,2026 katika kijiji cha Idodi,  wakati wa misa ya kumuaga aliyekuwa mbunge wa Ismani, William Lukuvi, akisema katika ziara hiyo atapita katika kila halmashauri na jimbo ili kuzungumza na viongozi pamoja na wananchi kuhusu changamoto mbalimbali za maendeleo.

“Nitapanga ziara kuja Mkoa wa Iringa, hapo ndipo nitakuja tuongee kwa kirefu. Nitapita kila halmashauri na kila jimbo. Mjiandae kwelikweli kwa sababu katika maandalizi ya ziara tayari nimeshaona maeneo ambayo tunatakiwa kuyafanyia kazi,” amesema Dk Mwigulu.

Katika maelezo yake, Waziri Mkuu amesema tayari amebaini baadhi ya mambo yanayohitaji kufanyiwa kazi, akitolea mfano sheria ya maegesho inayoruhusu mamlaka kukamata vyombo vya usafiri vinavyoegeshwa katika maeneo yasiyoruhusiwa na kuvihifadhi kwa muda kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa.

Amesema kwa mujibu wa sheria hiyo, chombo cha moto kinapokamatwa na mwenye nacho asipokichukua ndani ya mwezi mmoja, kinaweza kuuzwa huku mmiliki akitakiwa pia kulipa faini ya muda wote kilichohifadhiwa.

“Nimeona mmetunga sheria ya maegesho kwamba mtu akiegesha chombo chake cha moto katika maeneo fulani mnakikamata na ikifika mwezi mzima hajakichukua mnakiuza. Katika hicho kipindi cha mwezi anatakiwa pia alipe faini ya chombo chake kuhifadhiwa,” amesema.

Hata hivyo, amesema utaratibu huo unapingana na msimamo aliowahi kuutoa wa kulinda mitaji midogo ya wananchi.

“Yaani nyie mnaongelea kushika magari, bajaji na baiskeli wakati mimi nilisema ni marufuku kushika hata sahani ya mama lishe. Inakuwaje mnatunga sheria mshike hivyo vyombo vya usafiri?”

Dk Mwigulu amesema vyombo hivyo ni vitendea kazi muhimu kwa Watanzania wengi wanaojitafutia kipato, hivyo hatua ya kuvishikilia au kuviuza inaweza kuwaumiza kiuchumi, hasa kwa wale waliovinunua kwa mikopo.

“Unashikaje kitendea kazi ya Mtanzania ambacho inawezekana amekipata kwa kukopa, anadaiwa na benki, mshike kwa hiari yenu wenyewe halafu akikosa fedha ya kukigomboa mnasema awalipe na muda ambao mmekishika,” amehoji.

Ameongeza kama lengo ni kudhibiti maegesho, basi sheria hizo zinapaswa kuzingatia haki na uwezo wa wananchi, akitoa mfano wa magari ya Serikali.

“Sasa kama mnapenda kushika magari, mbona hamjaweka magari ya Serikali,” amehoji.

Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu amewapa pole kwa mara nyingine wananchi wa Ismani na Iringa kwa kumpoteza mpendwa wao na Serikali itaendelea kuyaenzi mema yote aliyoyatenda na kuahidi kuyafanyia kazi ikiwemo ya jimboni humo.