Dar es Salaam. Licha ya Serikali kuruhusu wanafunzi walioacha shule kutokana na ujauzito au changamoto nyingine kurejea katika mfumo rasmi wa elimu, bado baadhi ya wasichana wanaokumbatia fursa hiyo wanakabiliwa na changamoto ya unyanyapaa kutoka kwa jamii, walimu na wanafunzi wenzao.
Mwongozo huo unatolewa kupitia Waraka wa Elimu Na. 2 wa mwaka 2021, unaoruhusu wanafunzi walioacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwamo ujauzito kurejea na kuendelea na masomo yao, ukiwa sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya elimu bila ubaguzi.
Hata hivyo, changamoto ya unyanyapaa inaendelea kuwakatisha tamaa baadhi ya wanafunzi waliorejea shuleni, hali inayosababisha wengine kushindwa kuendelea na masomo licha ya fursa hiyo kuwapo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana Jumatatu, Machi 30,2026 wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kukabiliana na unyanyapaa kwa wanafunzi wanaorejea shuleni iliyoandaliwa na Taasisi ya Msichana Initiative, Ofisa Mwandamizi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Gladness Kirei amewataka wadau wa elimu kuwasaidia wanafunzi hao ili waweze kuendelea na masomo yao.
Kampeni hiyo inakwenda kutekelezwa katika mikoa ya Dodoma na Tabora walengwa watapewa mafunzo ya kukabiliana na unyanyapaa huo huku watendaji wengine wakielimishwa kuhusu umuhimu wa kuzingatia maelekezo ya mwongozo uliotolewa na Serikali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Msichana Initiative Consolata Chikoti akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya BCC inayolenga kuhamasisha jamii kuondoa unyanyapaa kwa wasichana wanaorejea shuleni baada ya kujifungua.
Amesema baadhi ya wanafunzi waliorudi shuleni baada ya kuruhusiwa kupitia waraka huo wanajikuta wakiacha tena masomo kutokana na kukumbana na unyanyapaa katika mazingira yao.
“Wapo wanafunzi wanaoshindwa kuendelea na masomo kwa sababu wananyanyapaliwa na jamii, walimu au hata wanafunzi wenzao. Hii inawafanya wajisikie kutengwa na kukata tamaa,” amesema.
Dk Kirei amefafanua mwongozo wa Serikali unaruhusu mwanafunzi kuhama shule endapo atahisi ananyanyapaliwa katika shule aliyopo.
“Mwongozo unaeleza wazi mwanafunzi anapoona shule moja inamnyanyapaa au kuna watu wanaomfanya ajisikie vibaya, anaruhusiwa kuhama kwenda shule nyingine ili apate mazingira rafiki ya kujifunza.
“Tunawapongeza kwa kuwapambania wasichana hadi kuona wale waliopata ujauzito wanapata fursa ya kurudi shuleni. Kampeni hii inaendelea kuhamasisha jamii kuona kundi hili kama wanafunzi wengine na kuwapa nafasi ya kusoma ili watimize ndoto zao,” amesema Dk Kirei.
Ameongeza kuna umuhimu wa kuwasaidia wanafunzi hao kwa njia mbalimbali ikiwamo kuwapatia mahitaji muhimu ya shule, vifaa vya kujifunzia na kuwapa moyo ili waendelee na masomo bila kukata tamaa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Msichana Initiative, Consolata Chikoti amesema shirika hilo linaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto zinazowakabili wasichana ili kuhakikisha wanapata haki yao ya elimu.
Amesema utekelezaji wa Waraka wa Elimu Na. 2 wa mwaka 2021 unakabiliwa na changamoto kadhaa hasa katika jamii ambako baadhi ya wanafunzi wanaorejea shuleni hukumbana na unyanyapaa.
“Takwimu za Wizara ya Elimu zinaonesha wanafunzi waliorejea katika mfumo wa elimu baada ya kuacha shule ni takribani 58, huku tafiti za Global Women Institute zikionesha takribani wasichana milioni 60 duniani wamekumbana na ukatili wa kijinsia,” amesema Consolata.
Consolata amesema takwimu pia zinaonesha msichana mmoja kati ya watatu anaolewa kabla ya kufikisha miaka 18, huku mmoja kati ya wanne pekee akiwa na uwezekano wa kumaliza elimu ya sekondari.
Ameitaja changamoto nyingine inayowakabili wasichana ni kukosa masomo kwa siku nne hadi tano kila mwezi kutokana na changamoto za hedhi.
Consolata amesema kupitia mradi wa “Rudi Shule”, shirika hilo tayari linafikia zaidi ya wasichana 500 waliokuwa wameacha shule, huku mwaka huu wakitarajia kuwafikia wanafunzi 250 zaidi.
“Hata hivyo, katika utekelezaji wa mradi huu tunagundua kuwa changamoto kubwa wanayokumbana nayo wasichana wanaorejea shuleni ni unyanyapaa kutoka kwa wanafunzi wenzao, jamii na wakati mwingine hata walimu,” amesema.
Mmoja wa wanafunzi walioshiriki katika uzinduzi wa kampeni hiyo, Theresa Juma (21), amesema licha ya changamoto alizopitia baada ya kupata ujauzito akiwa na umri wa miaka 18, bado ana ndoto ya kuendelea na elimu.
Baadhi ya wanafunzi walioshiriki uzinduzi wa kampeni ya BCC inayolenga kukabiliana na unyanyapaa dhidi ya wasichana wanaorejea shuleni baada ya kujifungua.
Theresa ambaye alipata ujauzito akiwa kidato cha kwanza na baadaye alilazimika kuacha shule na hata kufukuzwa nyumbani.
“Nakumbuka nilikuwa naingia kidato cha pili baada ya kufaulu kwa daraja la kwanza, lakini nilipopata ujauzito maisha yangu yanabadilika kabisa. Nafukuzwa nyumbani na napitia wakati mgumu sana,”amesema Theresa.
Hata hivyo, Theresa amesema changamoto hizo hazimfanyi akate tamaa na anaamua kujitafutia kipato ili kuweza kuendelea na masomo huku akimlea mtoto wake.
“Kwa sasa ninaendelea na masomo yangu. Ninalipa ada mwenyewe huku nikijitafutia kipato cha kuendesha maisha yangu na kumlea mtoto wangu,” amesema.
Amesema matamanio yake ni kuona jamii inawasaidia na kuwapa moyo wasichana wanaopitia changamoto kama yake ili waweze kutimiza ndoto zao za elimu na maisha bora.
