Mwanza. Katika juhudi za kuimarisha ulinzi wa kifedha na uwezo wa wananchi kukabiliana na changamoto zisizotarajiwa benki ya Stanbic Tanzania imetoa elimu ya bima kwa wananchi jijini Mwanza.
Elimu hiyo imetolewa nje ya tawi la benki hiyo lililopo Barabara ya Nyerere. Wananchi wa kada mbalimbali, wamiliki wa biashara ndogo na za kati pamoja na wafanyabiashara, waliopata nafasi ya kuelimishwa masuala mbalimbali yanayohusu bima na nafasi yake katika kulinda afya, biashara, mali pamoja na ustawi wa kifedha.
Hatua hiyo inaendelea kuiweka Stanbic kama mdau anayechochea mjadala mpana kuhusu umuhimu wa bima na namna wananchi na biashara wanavyoweza kujijengea kinga dhidi ya misukosuko ya maisha na biashara.
Akizungumza hafla hiyo, Meneja wa Benki Bima wa benki hiyo, Janeth Mbaruku, amesema bado kuna pengo kubwa la uelewa kuhusu bima miongoni mwa wananchi, licha ya umuhimu wake katika kusaidia watu binafsi na biashara kukabiliana na athari za matukio yasiyotegemewa.
“Watu wengi bado wanaichukulia bima kama jambo gumu, la gharama kubwa au huduma inayotafutwa pale tatizo linapotokea tayari. Kupitia shughuli hii, tunalenga kuifikisha elimu hii karibu zaidi na watu ili waelewe kuwa bima ni sehemu muhimu ya maandalizi ya kifedha na ulinzi wa yale wanayoyathamini,” amesema Janeth.
Amesema shughuli iliyofanyika Mwanza ni mwendelezo wa jitihada pana zaidi ambazo benki hiyo imeanza kuzifanya katika maeneo mbalimbali ya nchi, kufuatia mwitikio chanya uliopatikana katika hatua kama hiyo ililofanyika Tanga mwaka jana.
“Huu ni mwendelezo wa safari tuliyoianza. Tuliona mwitikio mzuri Tanga, na sasa Mwanza pia imeonesha wazi kuwa wananchi wanahitaji majukwaa ya namna hii ili kupata elimu sahihi, kwa lugha rahisi na inayogusa maisha yao ya kila siku. Ndiyo maana tunaona umuhimu wa kuendelea kuyapeleka mazungumzo haya karibu zaidi na jamii,” aliongeza.
Amebainisha kuwa shughuli hiyo imefanyika kwa ushirikiano na washirika wa bima wa Stanbic ambao ni Britam Insurance Tanzania Limited, Newtan Insurance Company Limited, Alliance Insurance Corporation Limited, Sanlam Allianz General Insurance Tanzania Limited, pamoja na Heritage Insurance Company Tanzania Limited, kwa lengo la kusaidia wananchi wengi zaidi kufanya maamuzi sahihi kuhusu kinga ya kifedha kabla ya kukumbwa na changamoto au hasara.
Miongoni mwa walioshiriki ni mfanyabiashara wa Mwanza, Florence Lugobi, ambaye amesema elimu hiyo imempa mtazamo mpya kuhusu bima, hasa kwa watu wanaojihusisha na biashara na kukutana na changamoto mbalimbali kila siku.
“Kama wafanyabiashara, mara nyingi tunajikita zaidi kwenye mauzo, bidhaa na uendeshaji wa kila siku wa biashara, lakini huwa hatupati muda wa kufikiria nini kinaweza kutokea endapo changamoto isiyotarajiwa itajitokeza. Leo nimeelewa vizuri zaidi kuwa bima si jambo la ziada, bali ni kinga na utulivu wa mawazo,” amesema Florence.
Ameongeza kuwa elimu ya aina hiyo inahitajika kuwafikia watu wengi zaidi, hasa wafanyabiashara wadogo na wa kati ambao mara nyingi hukabiliwa na hatari mbalimbali bila kuwa na uelewa wa kutosha juu ya namna ya kujilinda.
“Watu wengi wanahitaji kupewa elimu hii kwa lugha rahisi na inayoeleweka. Ukielewa vizuri, unagundua kuwa bima si kwa watu wachache tu, bali ni huduma muhimu kwa yeyote anayejenga biashara, familia au maisha yake kwa ujumla,” amesema.
Shughuli ya utoaji elimu iliyofanyika Mwanza linaakisi mwelekeo mpana zaidi wa namna taasisi za kifedha zinavyoanza kuifikia jamii kwa njia inayozidi huduma za kawaida za kifedha, kwa kuwekeza pia katika elimu ya vitendo inayosaidia wananchi kuwa na maandalizi bora, uthabiti wa kifedha na uwezo wa kulinda mafanikio wanayoyajenga.
Wakati matumizi ya bima yakiendelea kuwa chini ikilinganishwa na ukubwa wa hatari zinazokabili kaya na biashara nyingi nchini, wadau wa sekta hiyo wameendelea kuonesha kuwa elimu, uelewa na kuaminika kwa huduma ni miongoni mwa mambo muhimu yatakayosaidia kuongeza mwamko na matumizi ya bima kwa upana zaidi.
