Serikali yatinga kuokoa maisha ukanda bomba la Tazama Dar

Dar es Salaam. Kufuatia uchunguzi wa Gazeti la Mwananchi ulioibua hatari ya wafanyabiashara kuendelea kufanya shughuli zao katika ukanda wa bomba la mafuta la Tazama, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke imeanza kuchukua hatua.

Hatua hizo kutekeleza mpango wa kimkakati wa kujenga soko la kisasa la ghorofa pamoja na stendi mpya ya daladala, hatua inayolenga kuwaondoa wafanyabiashara katika maeneo hilo hatarishi na kuwapeleka kwenye mazingira salama zaidi.

Akizungumza kuhusu mpango huo, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda amesema hali ya sasa katika baadhi ya maeneo imekuwa ikiweka rehani usalama wa maisha ya wananchi na mali zao, ndiyo maana Serikali imeamua kuchukua hatua za haraka na za kudumu.

Mapunda ameeleza kuwa kupitia ushirikiano kati ya Serikali na halmashauri, ujenzi wa miundombinu hiyo mipya utatoa suluhisho la kudumu kwa wafanyabiashara waliokuwa wakifanya kazi katika maeneo yasiyo rasmi na yenye vihatarishi.

Amesisitiza kuwa lengo la mradi huo si tu kuwaondoa wafanyabiashara katika hatari, bali pia kuboresha mazingira ya biashara kwa kuwapatia miundombinu ya kisasa, salama na inayokidhi mahitaji ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika jiji hilo.

Mapunda amesema utekelezaji wa mpango huo tayari umeanza katika baadhi ya maeneo ya jirani, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa shughuli za biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wilaya ya Temeke.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kuwanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.

“Maeneo haya ni hatarishi, hivyo kwa kushirikiana na halmashauri tunajenga masoko ya ghorofa ili kuwahamisha wafanyabiashara na kuwawezesha kufanya shughuli zao katika maeneo salama,” anasema.

Anasema bado hakuna muda maalumu uliopangwa wa kukamilisha shughuli ya kuwahamisha wafanyabiashara hao, lakini mipango inaendelea ili kuhakikisha wanaondoka katika maeneo hatarishi na kuhamia maeneo rasmi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Jomary Satura, anasema halmashauri tayari imetangaza zabuni ya ujenzi wa stendi kubwa ya kisasa ya Mbagala, itakayokuwa na vyumba vingi kwa ajili ya wafanyabiashara mbalimbali, wakiwemo wamachinga.

Satura anasema stendi hiyo inalenga kuongeza fursa za kiuchumi kwa vijana wa eneo hilo, akibainisha kuwa ukubwa wa mradi utawezesha kuhudumia wafanyabiashara wengi kwa wakati mmoja.

Hata hivyo, anasema bado kuna changamoto ya baadhi ya wafanyabiashara kutopenda kufanya kazi katika maeneo rasmi, licha ya kuwepo kwa masoko yaliyojengwa.

“Tuna masoko matatu ya Zakheim, Mbagala na Kambochea yenye vyumba vingi, lakini baadhi ya maeneo hayo yameachwa wazi kutokana na wafanyabiashara kuhamia katika maeneo hatarishi, hali inayochangiwa pia na tabia za wateja,” anasema.

Anasema ujenzi wa stendi hiyo mpya unaaminiwa kuwa suluhisho la kuwakusanya wafanyabiashara wengi katika eneo salama na rasmi. Mradi huo unatarajiwa kujengwa katika eneo la kona kuelekea Chamazi, kwenye kiwanja chenye ukubwa wa hekta tatu.

Kwa upande wake, Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Nurdin Bilal ‘Shetta’ anasema anafahamu jambo hilo isipokuwa wanalishughulikia ikiwemo kutafuta maeneo yanayofaa wafanye shughuli zao.

“Jambo hili tunalifuatilia na kwa kushirikiana na halmashauri, kulishughulikia kwa kuwatafutia maeneo sahihi wanayoweza kufanya shughuli zao kwa usalama,” anasema.

Mbunge wa Ukonga, Bakari Shingo, amesema kuwa wajibu wa Serikali ni kutengeneza ajira na kuweka mazingira rafiki kwa wananchi, huku akisema katika eneo lake vijana wengi wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ajira.

“Wajibu wa Serikali ni kutengeneza ajira na mazingira rafiki kwa wananchi. Katika eneo langu vijana wengi wanakabiliwa na changamoto ya ajira,” amesema.

Akizungumzia suala la wafanyabiashara wanaofanyia shughuli katika eneo hatarishi, amesema tatizo hilo si la kubeza kwani wahusika wanafahamu hatari iliyopo.

“Shida haina adabu. Wote waliokaa katika hifadhi hiyo wanajua hatari yake, lakini ukiwagusa kuhusu hoja hiyo wanakuuliza unawapeleka wapi? Najua ni hatari, lakini tayari nimekaa na Mkurugenzi pamoja na Mkuu wa Wilaya kutafuta eneo la soko Gongo  la Mboto,” amesema.

Amesema Gongo la Mboto ina idadi kubwa ya wamachinga, hivyo kuna haja ya kutafuta suluhisho la kudumu kwa kujenga soko rasmi.

“Gongo la Mboto kuna wamachinga wengi. Lazima tutafakari na kupata eneo la kujenga soko ili kuondokana na hatari inayoweza kuleta hasara kubwa kwa jamii,” amesema.

Amesema anatambua hatari ya wananchi kuendelea kufanya shughuli zao katika eneo hilo, lakini tayari kuna makubaliano na watendaji wa halmashauri kutafuta suluhisho.

“Ni kweli najua hatari ya kufanya shughuli katika eneo hilo, na kwa makubaliano yetu na watendaji wa halmashauri tumekubaliana kufikiria na kupata eneo la soko Gongo la Mboto,” amesema.

Hata hivyo, amekanusha kuwa wanasiasa ndio chanzo cha wananchi kufanya shughuli katika maeneo hayo, akidai kuwa baadhi ya watendaji hawatekelezi wajibu wao ipasavyo.

“Kuna miradi mingi unashindwa kwenda kwa sababu ya wataalamu. Cha msingi tuache tabia ya kutupiana mpira; kikubwa ni kuwajibika kwa kusimamia sheria,” amesema.

Kwa kumalizia, amesema hata kama wanasiasa wamechangia changamoto hizo, hilo haliwaondolei wataalamu wajibu wao wa kutekeleza sheria.

“Inawezekana kweli wanasiasa wamechangia kukwamisha baadhi ya mambo, lakini hiyo haiondoi wajibu wa wataalamu kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia miongozo na taratibu za sheria za nchi,” amesema.

Alipoulizwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk James Mataragio, kuhusu hali ya uvamizi wa miundombinu hiyo, anajibu kuwa mamlaka itafanya ziara ya ukaguzi ili kubaini hali halisi na kuchukua hatua stahiki kuondoa tatizo hilo.

“Pia, Tazama kuna wakaguzi wao watakaofuatilia na kutathmini hali iliyopo ili kutafuta ufumbuzi,” anasema Dk Mataragio.

Hata hivyo, Mwananchi ilizungumza na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Mhite kutaka kujua kama anafahamu changamoto hiyo na hatari inayowakabili wanaofanya biashara maeneo hayo.

“Nitafuatilia na kujua namna ya kufanya kazi,“ Mhite.

Bomba la mafuta la Tazama ni mradi uliounganisha Tanzania na Zambia kwa lengo la kuvunja minyororo ya utegemezi na ukandamizaji wa kikoloni.

Miaka ya 1960, Zambia ilijikuta katika hali ngumu ya kijiografia. Ikiwa ni nchi isiyo na bandari, kila shughuli ya biashara ya kimataifa ililazimika kupita katika nchi jirani.

Hali hiyo ilikuwa ya hatari zaidi kutokana na mazingira ya kisiasa ya wakati huo. Nchi kama Rhodesia (sasa Zimbabwe), Afrika Kusini na Msumbiji zilikuwa chini ya tawala za kibaguzi au kikoloni, ambazo mara nyingi zilitumia miundombinu yao kama silaha ya kisiasa.

Ndipo zilipojitokeza dhamira na uongozi wa kipekee kutoka kwa marais Mwalimu Nyerere (Tanzania) na Kenneth Kaunda (Zambia).

Viongozi hawa waliamua kuchukua hatua ya kihistoria kwa kuanzisha mradi wa bomba la mafuta ambalo lingeunganisha Bandari ya Dar es Salaam na Zambia, bila kutegemea njia za nchi zenye misimamo hasimu.

Mwaka 1966, makubaliano rasmi ya ujenzi wa bomba hilo yalitiwa saini, yakifungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kikanda.

Kufikia mwaka 1968, bomba hilo lenye urefu wa takriban kilomita 1,710 lilianza kufanya kazi, likisafirisha mafuta kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Ndola nchini Zambia.

Umuhimu wa bomba la Tazama haukuishia katika usafirishaji wa mafuta pekee. Kimsingi, lilikuwa ni chombo cha ukombozi wa kiuchumi.

Aidha, bomba hilo lilipunguza kwa kiasi kikubwa gharama za usafirishaji wa mafuta. Kabla yake, mafuta yalisafirishwa kwa malori kupitia barabara zisizo na ubora, hali iliyokuwa ghali na hatarishi.

Kwa Tanzania, mradi huu uliimarisha nafasi yake kama lango la biashara kwa nchi zisizo na bandari katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.

Awali, bomba hili lilikuwa likisafirisha mafuta ghafi (crude oil) kwa ajili ya kusafishwa katika kiwanda cha Indeni nchini Zambia.

Hata hivyo, katika jitihada za kuongeza ufanisi, serikali za Tanzania na Zambia zimeanza kuliboresha ili liweze kusafirisha mafuta yaliyosafishwa kama dizeli moja kwa moja.

Leo hii, bomba la Tazama linaendelea kuwa alama ya mafanikio ya ushirikiano wa kikanda barani Afrika. Ni ushahidi kuwa changamoto za kijiografia kama ukosefu wa bandari zinaweza kushindwa kupitia mshikamano na maono ya pamoja ya viongozi.