Ajali ya basi yaua sita, manusura  wasimulia ilivyokuwa

Dodoma. Ajali za barabarani zimeendelea kugharimu maisha ya watu baada ya watu sita kufariki dunia na wengine 55 kujeruhiwa katika ajali iliyotokea Kijiji cha Mkiwa, Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.

Ajali hiyo imehusisha basi la kampuni ya Green Line ambalo lilikuwa linatoka Dar es Salaam kwenda mkoani Mwanza.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Amon Kakwale amesema chanzo cha ajali hiyo ni gurudumu la mbele la basi kupasuka baada ya kukita kwenye shimo

“Ni kweli kuna ajali inayohusisha basi ulilolitaja, mpaka sasa tumepoteza wenzetu sita lakini tunao majeruhi 14 waliopelekwa hospitali kwa matibabu zaidi,” amesema Kakwale.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, ajali hiyo iliyotokea saa nne asubuhi Machi 31, 2026 na uchunguzi zaidi unaendelea, ikiwemo kubainisha majina ya majeruhi na waliopoteza maisha, huku juhudi za kuwapeleka hospitali waliopatwa na madhara zikiendelea.

Hata hivyo, taarifa kutoka eneo la tukio zimedai idadi ya majeruhi inatajwa kuwa zaidi ya 50, wakiwemo watoto na kwamba waliokuwa katika hali ya kuhitaji uangalizi zaidi walikuwa 16.

“Dereva wetu tangu mwanzo wa safari hakuwa na mwendo wa kuogopesha, lakini tulipofika kijiji hicho, ambacho hakionyeshi kuwa na changamoto, ndipo akakita kwenye shimo na hapo tukasikia kishindo kilichokwenda sambamba na gari kupinduka,” amesema mmoja wa abiria aliyejitambulisha kwa jina moja la Celina.

Majeruhi huyo, ambaye alitaja kuumia mkono wa kulia na kupata maumivu makali kwenye mbavu za upande huo, amesema kama ajali hiyo ingetokea wakiwa kwenye mwendo mkali, huenda ingesababisha maafa makubwa zaidi.

“Mimi ndiyo nilikuwa kwenye gari na abiria aliyekuwa kwenye kiti cha mbele yangu naamini amepoteza maisha. Wasimsingizie dereva, ila haya mashimo barabarani ni hatari jamani. Tumepoteza abiria wenzetu na sisi wengine hatujui maumivu yetu yamefikia wapi,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson basi hilo limepata ajali katika eneo la Njiri katika Kijiji cha Mkiwa, Wilaya ya Ikungi na kuwa Serikali ilishachukua hatua zote stahiki kwa ajili ya kuwasaidia majeruhi na kuhifadhi miili ya waliopoteza maisha.

Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Manyoni, Dk Bwire James amesema hospitali hiyo ilipokea miili sita na majeruhi 55, kati yao wanaume 34 na wanawake 21, baadhi walitibiwa na kuruhusiwa huku wengine wakiendelea na matibabu.