Askofu Bagonza atoa wito kurejea kwenye ukweli

Dar es Salaam. Katika ujumbe wake wa Pasaka mwaka 2026, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza, amewataka waumini na jamii kwa ujumla kurejea katika msingi wa ukweli, akisisitiza kuwa ufufuko wa Yesu Kristo ni ushuhuda wa ushindi wa ukweli dhidi ya uongo.

Kwa mujibu wa kalenda ya Kikristo, Wakristo wataadhimisha Sikukuu ya Pasaka Aprili 5, 2026, siku ambayo katika imani hiyo huadhimisha ufufuko wa Yesu Kristo kutoka kwa wafu, tukio linalochukuliwa kuwa kiini cha imani ya Kikristo na ishara ya ushindi wa uzima dhidi ya mauti, haki dhidi ya dhambi na ukweli dhidi ya uongo.

Akitoa salamu hizo kwa waumini wa dayosisi hiyo, Askofu Bagonza amenukuu maandiko matakatifu ya Biblia akisema, “Ni kweli Bwana amefufuka! Amemtokea Simoni” (Luka 24:34), akieleza kuwa ushuhuda huo uliotolewa na mitume ni msingi wa imani ya Kikristo na uthibitisho usio na shaka wa ufufuko wa Kristo.

Amefafanua mitume waliotoa ushuhuda huo walikuwa na dhamira ya kuondoa mashaka kwa watu wote ili waamini ukweli huo, huku akisisitiza kuwa hata wale waliomtesa na kumuua Yesu walipaswa kujua kuwa ukweli hauwezi kufichika milele.

“Tabia ya watu kukwepa ukweli haikuanza leo,” amesema Askofu huyo, akiongeza kuwa tofauti na zamani ambapo watu waliogopa kusema uongo, sasa hali imebadilika na wengi wanaogopa kusema ukweli.

Kwa mujibu wa ujumbe huo, Askofu Bagonza ameeleza, “zamani watu waliogopa kusema uongo ili wasife, lakini siku hizi watu wanaogopa kusema ukweli ili wasife,” akitahadharisha kuwa hali hiyo inaonesha kuporomoka kwa maadili ya jamii.

Akinukuu maandiko katika Biblia, Injili ya Yohana, amekumbusha juu ya asili ya uongo akisema, “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, yeye ni mwongo, na baba wa huo uongo” (Yohana 8:44), akisisitiza kuwa uongo ni silaha inayotumiwa kuharibu jamii na kupotosha haki.

Katika hatua nyingine, Askofu huyo ameweka wazi kuwa chanzo cha migogoro mingi katika familia, kanisa na Taifa ni kuendekeza uongo badala ya kusimamia ukweli.

Aidha, ametaja mifano ya imani potofu zinazotamalaki katika jamii, akisema ni uongo kuamini mtu anaweza kutajirika bila kufanya kazi, au kupata uongozi kwa hila na kutotenda haki.

“Ni uongo kuvuruga amani ili kuleta amani, na ni uongo kudai tunaweza kuwa na amani bila kutenda haki,” amesisitiza, akionya kuwa bila kurejea katika ukweli, hakuna usalama wa kweli kwa jamii.

Askofu Bagonza pia ameelezea wasiwasi wake kuhusu malezi ya vijana, akidai kuwa wameachwa katika mazingira yanayowafanya waige mienendo mibaya kutoka kwa viongozi na jamii huku akihoji kwa masikitiko…vijana wana nini cha kuiga iwapo wanachokiona ni rushwa, ubabe, wizi na dhuluma.

Hata hivyo, pamoja na changamoto hizo, ametoa tumaini kupitia ujumbe wa ufufuko, akisema kuwa Kristo aliyefufuka ni mwaliko kwa wanadamu wote kurejea katika njia ya kweli.

“Baba wa ukweli ameshafufuka. Yeye akituweka huru, tunakuwa huru kweli kweli” (Yohana 8:32), amenukuu, akisisitiza kuwa ufufuko wa Yesu Kristo ni wito wa maridhiano ya kweli yanayojengwa juu ya haki, ukweli na uwajibikaji bila kuogopa gharama zake.

Askofu Bagonza pia amewataka waumini na Watanzania kwa ujumla kufanya toba na kubadilika, akisema, “tujirudi tushike ukweli ili utuweke huru,” huku akiwatakia waumini Wakristo na Watanzania kwa ujumla Pasaka njema yenye baraka na furaha ya kufufuka kwa ukweli, akiweka msisitizo kuwa ushindi wa Kristo ni ushindi wa ukweli unaopaswa kuishi ndani ya kila mmoja.