DCEA yateketeza kilogramu 68 za mirungi Same

Same. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Kanda ya Kaskazini, imeteketeza dawa za kulevya aina ya mirungi zenye uzito wa kilogramu 68.3, ambazo zilikuwa zikitumika kama vielelezo kwenye kesi mbalimbali katika Mahakama ya Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro.

Dawa hizo za kulevya zimeteketezwa leo Jumanne, Machi 31, 2026 katika eneo la wazi la dampo la Jeshi la Polisi lilipo wilayani humo, ambapo wadau wa Mahakama, washtakiwa, vyombo vya ulinzi na usalama  pamoja na baadhi ya wananchi walishuhudia shughuli hiyo.

Kufuatia shughuli hiyo, wananchi wa wilayani humo wameishukuru mamlaka hiyo kwa juhudi kubwa wanazozifanya za kupambana na dawa za kulevya na kusema utumiaji na usafirishaji wa dawa za kulevya umekithiri wilayani humo huku wakidai kuwa, wahusika wakubwa ni vijana.

Dawa za kulevya aina ya mirungi ikiteketezwa katika eneo la wazi  katika  eneo la dampo la polisi wilayani  Same, mkoani Kilimanjaro.

Mmoja wa wananchi hao, Salmina Ramadhan amesema utumiaji wa dawa za kulevya aina ya mirungi umewaathiri vijana na baadhi yao wanashindwa kutekeleza majukumu ya kifamilia.

“Vijana wetu wameharibika sana kutokana na matumizi ya mirungi, tunawaomba  (DCEA) itusaidie. Hapa kwenye kata yetu, mirungi inauzwa waziwazi na vijana wengi wameathirika.”

“Hali ya mtaa wetu sasa haifai kabisa, mirungi imeshamiri na imekuwa ni janga. Tunaomba msaada ili kukomesha hali hii.”

Mwananchi mwingine, Amana Sabuni, ameipongeza DCEA kwa hatua hiyo nzuri na kusema vijana wengi ndoa zao zimevunjika kutokana na ulaji wa mirungi hivyo akaomba hatua zaidi zichukuliwe kukomesha hali hiyo.

Dawa za kulevya aina ya mirungi ikiteketezwa katika eneo la wazi  katika  eneo la dampo la polisi wilayani  Same, Mkoani Kilimanjaro.

“Jitihada hizi zisiishie tu hapa, leo tumeona dawa zikiteketezwa lakini sio hivyo tu ndoa nyingi zimevunjika, mtaani adabu hakuna, wazee hawaheshimiwi. Tumefurahi leo kwa  mara ya kwanza kushuhudia dawa hizi zikiteketezwa. Hizi dawa zimekuwa ni changamoto kutokana na vijana wetu kuharibika,” amesema Sabuni.