ENG. KASEKENYA AWATAKA WATUMISHI UJENZI KUFANYA KAZI KWA WELEDI

******

Naibu Waziri Eng. Godfrey Kasekenya amesisitiza umuhimu wa watumishi wa Wizara ya Ujenzi kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na weledi, huku wakiweka mbele maono ya Serikali ya awamu ya sita ya kuacha tabasamu kwa wananchi.

Akifunga Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Ujenzi jijini Dodoma leo Eng. Kasekenya amewataka watumishi kuepuka vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya ofisi.‎‎

“Fanyeni kazi kwa weledi ili kufikia malengo ya Serikali na kuleta tija kwa wananchi”, amesema Eng. Kasekenya.

Naibu Waziri Kasekenya amehimiza watumishi kufanya mazoezi na kuwa na vyanzo sahihi vya mapato ili kuepuka msongo wa mawazo na changamoto za afya ya akili.

Aidha, Eng. Kasekenya amesisitiza umuhimu wa watumishi kuwa na msukumo wa kufanya kazi ili kuongeza ujuzi na maarifa ambapo vinapelekea kufanya kazi kwa uhuru na kujituma.

‎Mapema akizungumza katika kikao hicho Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, amebainisha kuwa kikao cha Baraza la Wafanyakazi kililenga kusikiliza hoja mbalimbali za watumishi, kujadili kwa kina majukumu na maslahi ya watumishi na kutoa ufumbuzi kwa changamoto zinazowakabili watumishi.

Ameeleza kuwa Baraza hilo limepata faida kubwa kwa kujifunza mada muhimu ikiwemo uwekezaji na ujasiriamali kwa watumishi, ambapo hata mtumishi mwenye mshahara mdogo anaweza kuimarisha hali yake kifedha na kuwa mwekezaji mzuri.‎

‎Amebainisha kuwa Baraza limejadili lishe bora na afya ya mwili, kujua nini na wakati gani wa kula ili kuimarisha afya na mstakabali wa watumishi, pamoja na afya ya akili, ikiwemo kuepuka msongo wa mawazo ili kuwa na utumishi bora. 

Aidha, wajumbe wamejadili mikakati ya ujenzi wa barabara, madaraja, ukarabati wa miundombinu, na mbinu za kushirikisha sekta binafsi pamoja na kuimarisha mizani ili kulinda barabara.‎

‎Mkutano wa Baraza la wafanyakazi Wizara ya Ujenzi ulioanza jana umehitimishwa leo ambapo pamoja na mambo mengine umepitia mapendekezo ya bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027.

Wajumbe wa Baraza hilo pia wamekagua majengo ya ofisi za Wizara ya Ujenzi na la Wakala wa Barabara TANROADS yanayojegwa Mtumba na Njedengwa jijini Dodoma na kuridhishwa na kasi ya ujenzi huo.