Pedro: Yanga kuna shida! Amtaja Moallin

WAKATI baadhi ya mashabiki wa Yanga wakionekana kutofurahia kiwango cha timu hiyo, kocha mkuu Pedro Goncalves amesema baadhi ya watu wanalalamika bila kujali kwamba timu inafanya vizuri.

Vilevile amegusia ujio wa Abdihamid Moalin kwamba halikuwa pendekezo lake, lakini anaamini kuwa ataisaidia klabu hiyo kufika mbali.

Yanga ambayo ilianzishwa miaka 91 iliyopita, inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 38, ni kati ya timu mbili ambazo hadi sasa hazijapoteza mchezo wowote katika ligi sambamba na Azam ambayo itaivaa leo, Singida BS.

Kocha huyo raia wa Ureno, ameeleza kuwa alipotua Yanga mwishoni mwa Oktoba, 2025 timu hiyo inayosaka ubingwa wa 32 wa Ligi Kuu Bara ilikuwa imeuanza msimu huu wa mashindano huku ikiwa nyuma ya Simba na Azam, lakini sasa presha kwenye timu hiyo ni kubwa.

“Ingawa kuna kelele ni nyingi zinazotuzunguka lakini ukweli unabaki kuwa tulipofika (wakati anatambulishwa) hatukuwa juu ya msimamo. Tulikuwa nyuma ya Simba na timu nyingine lakini sasa tupo kileleni tukiwa na mabao mengi ya kufunga (32), machache ya kufungwa (3) na hatujapoteza mechi yoyote,” alisema Pedro.

“Hivyo tunaongoza ligi kwa sababu tunastahili, tumeonyesha hilo uwanjani. Kwa sasa tunajiandaa kwa nusu ya pili ya msimu, ambapo zimebaki takribani miezi miwili na nusu na itakuwa kipindi kigumu sana kwa kila mtu. Hata hivyo, kuwa juu ya msimamo ndilo lengo na si kufika tu juu bali kubaki juu, jambo ambalo linatupa kujiamini kuelekea mechi zilizobaki.”

Ndani ya mafanikio hayo, Pedro alisema kuna upande mwingine ambao mashabiki wengi hawaoni kirahisi ni uchovu na changamoto za ratiba ngumu ya mechi ambazo wamekuwa nazo mfululizo.

Kocha huyo alisema kuwa kwa muda mrefu wachezaji walikuwa wakicheza bila kupumzika, hali iliyowalazimu kutoa wiki maalumu ya mapumziko ili kurejesha nguvu za kikosi hicho.

Baadhi ya wachezaji wao ambao hawakuwa kwenye majukumu ya timu za taifa kama vile, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ walipata nafasi ya kupona huku wengine wakifanyiwa matibabu maalum ili kurejea katika ubora wao.

Alieleza kuwa kikosi hakijakamilika kwa asilimia mia moja, lakini anaamini kadri siku zinavyosonga, watazidi kuwa imara zaidi.

Kuhusu presha ya malalamiko ya mashabiki, hasa juu ya sare mfululizo ambazo walitoa dhidi ya Azam (0-0), TRA (0-0) na Mtibwa Sugar (1-1) na upungufu wa mabao katika baadhi ya mechi, kocha huyo hakukwepa kuzungumzia hilo;

“Presha ndani ya kikosi ni kweli ipo lakini presha ni sehemu ya maisha ya kila siku, tangu nifike hapa nimekuwa nikiihisi. Yanga ni klabu kubwa lakini siyo pekee Afrika wala nchini, hivyo kila timu kubwa inaishi na presha na ni lazima tujifunze kukabiliana nayo,” alisema.

“Hakuna anayefurahia sare, nasi hatufurahii kabisa. Lakini ukweli ni kwamba sehemu kubwa ya sare  zimetokea mechi za ugenini katika mazingira magumu sana, hasa kutokana na ubora mdogo wa viwanja.”

Kuhusu wanaoifananisha Yanga ya msimu huu na ile iliyopita chini ya makocha tofauti, kocha huyo alisema; “Tunachofanya msimu huu ni kushindana na wapinzani wa sasa, si wa zamani. Wapinzani wetu ni Simba, Azam na timu nyingine zote.”

“Hatuwezi kulinganisha hali ya sasa na misimu iliyopita kwa sababu mazingira ni tofauti. Ni lazima tukubaliane na hali halisi ya sasa na kujiandaa nayo. Tunachopambana nacho ni ushindani wa leo.”

Pedro ameiongoza Yanga katika michezo 12 ya Ligi Kuu Bara, ameshinda mechi tisa ambazo ni dhidi ya Tanzania Prisons, Singida BS, JKT Tanzania, Namungo, Dodoma Jiji, Mashujaa, Coastal Union, Fountain Gate, KMC huku akitoa sare nne dhidi ya Mtibwa Sugar, TRA United, Azam na Simba

Hivyo ameifanya Yanga kukusanya pointi 38, Wananchi chini ya kocha huyo wamedondosha pointi nane katika sare nne.

“Ni uongozi wa klabu ndio uliopendekeza wazo hilo la kumjumuisha, bila shaka tuna matarajio naye makubwa, tunaamini atatusaidia na kuongeza nguvu kwenye kikosi kwa sababu ni nyongeza muhimu kwetu,” alisema na kuongeza;

“Benchi letu halikuwa pana hivyo tuna majukumu mengi ya kutekeleza. Ndiyo maana tunaamini ni mtu sahihi atakayetusadia katika kazi hiyo kubwa tuliyonayo. Tunaamini ataongeza mchango chanya ndani ya timu.”

Hata hivyo mmoja wa viongozi wa timu hiyo aliwahi kusema kuwa ujio wa kocha huyo ni pendekezo la Pedro.

Kwa upande wake, Abdihamid Moalin ambaye amewahi kufanya kazi kwenye timu hiyo kama mkurugenzi wa ufundi na kocha msaidizi alisema; “Nimefurahi kwa mapokezi makubwa ambayo nimepata nipo tayari kutoa mchango wangu wote kwa ajili ya kuisaidia timu kufikia malengo yake.”