UCHAMBUZI WA MAYALA: Urais 2030: Ndoto halali, sio jinai

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kila Mtanzania mwenye sifa anaruhusiwa kugombea nafasi ya urais.

Ibara ya 39 ya Katiba hiyo inaeleza wazi vigezo vya msingi vinavyopaswa kutimizwa na mgombea wa kiti hicho cha juu kabisa nchini. Miongoni mwa vigezo hivyo ni pamoja na kuwa raia wa kuzaliwa wa Tanzania, kuwa na umri wa miaka 40 au zaidi, kuwa mwanachama wa chama cha siasa na kuteuliwa na chama hicho, pamoja na kuwa na sifa za kuwa mbunge au mjumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Msingi huu wa kikatiba unaweka wazi kuwa ndoto ya kuwa rais siyo kosa wala dhambi. Ni haki ya msingi ya kila Mtanzania anayekidhi masharti hayo. Ndoto hiyo ni sehemu ya uhuru wa kisiasa na kidemokrasia unaolindwa na Katiba yenyewe.

Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni, kumekuwepo na dalili zinazoashiria kujengeka kwa mazingira yasiyo rafiki kwa baadhi ya Watanzania wanaoonesha nia au ndoto ya kugombea urais mwaka 2030.

Baadhi ya viongozi wamekuwa wakitoa kauli zinazotafsiriwa na wengi kuwa ni vitisho au mikwara inayoweza kuwakatisha tamaa wale wanaotamani kushiriki katika mchakato huo wa kidemokrasia.

Ni muhimu kufahamu kuwa nafasi ya urais ni ya ushindani wa wazi, unaopaswa kuendeshwa kwa misingi ya haki, usawa na kuheshimu Katiba. Hakuna kundi la watu au watu wachache waliopewa haki ya kipekee ya kugombea nafasi hiyo. Mfumo wa vyama vingi vya siasa unaruhusu ushindani mpana, ambapo kila chama kina taratibu zake za kumpata mgombea, lakini pasipo kuzuia haki ya mtu kuwa na ndoto hiyo.

Kinachotia shaka ni kauli zinazodokeza kuwa kuna watu maalum pekee wanaostahili kugombea urais kupitia vyama fulani.

Hali hii si tu inapunguza wigo wa ushindani, bali pia inakinzana na roho ya demokrasia inayohimiza ushiriki mpana wa wananchi.

Aidha, zipo kauli zinazotolewa hadharani zikihusisha vitisho, kuhusisha dini au hata kutoa hukumu za mapema kuhusu nani atafanikiwa au kushindwa katika uchaguzi ujao.

Kauli za aina hii, hasa zinapotolewa na viongozi wa umma, zinaweza kuleta taswira isiyofaa kwa jamii na kudhoofisha imani ya wananchi katika mchakato wa kidemokrasia.

Kwa mfano, kauli zinazodai kuwa baadhi ya watu hawawezi kamwe kuwa marais, au kuwa ndoto zao hazitatimia, zinaweza kutafsiriwa kama kujaribu kufunga milango ya ushindani kabla ya wakati.

Hali kadhalika, matumizi ya lugha ya vitisho au kulinganisha wapinzani wa kisiasa na taswira hasi siyo afya kwa ustawi wa siasa za kistaarabu.

Swali la msingi linalopaswa kujiulizwa ni hili: Je, kuwa na ndoto ya kugombea urais mwaka 2030 ni kosa? Jibu ni hapana. Ndoto hiyo inapaswa kuheshimiwa na kulindwa kama sehemu ya haki za kikatiba za Mtanzania.

Ni kweli kwamba vyama vya siasa vina mamlaka ya ndani ya kuchuja wagombea wao. Hata hivyo, mchakato huo unapaswa kuwa wa haki, wazi na unaozingatia misingi ya demokrasia.

Pale ambapo watu wanahisi kunyimwa haki au kubaguliwa kwa misingi isiyo wazi, hali hiyo inaweza kusababisha baadhi yao kuhama vyama au hata kukata tamaa ya kushiriki kabisa katika siasa.

Katika muktadha wa uchaguzi wa mwaka 2030, ni wazi kuwa Tanzania itahitaji viongozi wapya watakaowania nafasi ya urais baada ya kipindi cha uongozi wa sasa kukamilika. Hivyo basi, ni muhimu kuanza kujenga mazingira yatakayowezesha ushindani wa haki na unaozingatia misingi ya Katiba.

Viongozi wa umma wanapaswa kuwa mstari wa mbele kulinda haki hizi. Wameapa kuitii na kuilinda Katiba, hivyo kauli au vitendo vinavyoonekana kuwanyima au kuwakatisha tamaa wengine haviendani na kiapo hicho. Badala yake, wanapaswa kuhimiza ushindani wa hoja, sera na uwezo wa uongozi.

Demokrasia yenye afya inahitaji mawazo tofauti, ushindani wa wazi na heshima kwa kila anayetamani kuongoza. Kuwazuia au kuwatisha watu wenye ndoto ya uongozi ni kudhoofisha misingi hiyo. Kwa mtazamo mpana, ni vyema Watanzania wakaachwa huru kujitokeza, kueleza nia zao na hatimaye kupimwa na wananchi kupitia sanduku la kura. Hapo ndipo taifa linaweza kupata viongozi bora, waliopatikana kwa ushindani wa haki na unaokubalika na wengi.

Mwisho wa yote, urais si mali ya mtu au kundi fulani, bali ni dhamana ya wananchi wote. Ndoto ya kuwania nafasi hiyo ni haki ya kila Mtanzania mwenye sifa, na inapaswa kuheshimiwa, siyo kubezwa au kuzimwa kwa vitisho.