Migogoro ya upinzani ni Ofisi ya Msajili au wenyewe?

Dar es Salaam. Migogoro ya uongozi ndani ya vyama vya upinzani nchini inaendelea kuibua mjadala, huku baadhi vikielekeza lawama kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, vikidai inaingilia maamuzi ya ndani.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya siasa, wanaeleza tatizo linaanzia kwenye mapungufu ya kimuundo katika sheria na udhaifu wa ndani wa vyama wenyewe, hali inayotia doa mustakabali wa ushindani wa kisiasa nchini.

Malalamiko ya vyama vya upinzani kuhusu kuingiliwa katika maamuzi yao ya ndani, yamewahi kuibuliwa na Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha NCCR Mageuzi.

Vyama hivyo vyote, kwa nyakati tofauti vimejikuta vikibadili uongozi ghafla, tofauti na ule ambao ulichaguliwa kupitia chaguzi zao za ndani.

Kwa CUF, hilo limetokea mapema mwaka huu, baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kubatilisha uchaguzi uliompa ushindi Profesa Lipumba, uliofanyika Desemba mwaka 2024.

Kwa mujibu wa barua ya msajili, alipokea malalamiko kutoka kwa wanachama wa chama hicho, wakilalamika ushindi wa Profesa Lipumba haukufika zaidi ya asilimia 50 ya kura, hivyo kwa Katiba ya CUF uchaguzi ulipaswa kurudiwa.

Hata hivyo, Profesa Lipumba mwenyewe amedai uamuzi huo wa kuondolewa kwake umetokana na kauli zake dhidi ya mamlaka akikemea matukio ya Oktoba 29, mwaka 2025 na kuukosoa uchaguzi kwa ujumla.

Alitaja sababu ya pili ya hilo ni chama chake kiligomea kutoa maoni yake kwenye Tume ya kuchunguza matukio yaliyojitokeza kabla na baada ya Oktoba 29, 2025.

Kwa upande wa Chadema, kilikutana na hali hiyo pale ambapo ofisi hiyo ya msajili ilipokiandikia barua kueleza baadhi ya viongozi wake hasa wajumbe wa sekretarieti walipatikana katika mazingira batili.

Ubatili huo, barua hiyo ilisema umetokana na viongozi hao kupigiwa kura na kikao ambacho kilihudhuriwa na wajumbe wasiokuwa halali.

Hata hivyo, barua hiyo ya msajili kwa Chadema, ilitokana na malalamiko ya aliyekuwa mwanachama wa chama hicho, Lembrone Mchome, aliyedai baadhi ya wajumbe hawakuwa halali.

Akizungumzia hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Aman Golugwa, amesema kumekuwapo hila nyingi ndani ya mifumo kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, zinazolenga kubagaza vyama vya siasa.

“Tuna ushahidi kuwa chama chetu kinapitia magumu kwa sababu ya mifumo. Vyama vya upinzani vinapitia changamoto, hasa vinapoonekana kutoa ushindani wa kweli dhidi ya serikali,” anasema.

Kuhusu yanayoendelea ndani ya CUF, anasema wanashindwa kumuonea huruma Profesa Ibrahim Lipumba kwa sababu hapo awali alikubali kutumika, jambo lililokiumiza chama hicho na kuongeza uadui.

“Kipindi hiki, alipojaribu kuwa mkweli huenda kutokana na utu uzima hali hiyo imekuwa kama dawa kwake. Hata hivyo, kusema ukweli katika kipindi hiki kumemgharimu,” anasema.

Anasema kuwa yote aliyoyazungumza katika hotuba zake yalikuwa ya kweli, lakini kwa sababu hapo awali alikuwa kikaragosi kilichotengenezwa na mfumo, ukweli huo umemgharimu, ingawa hakusema uongo.

“Alikuwa kikaragosi kilichotengenezwa na mfumo lakini mfumo umeamua kumpanda ponda. Chadema tuna uthibitisho kuwa Ofisi ya Msajili imekuwa ikiingilia na kuvuruga kabisa ukuaji wa vyama badala ya kuvilea,” anasema.

Anasema Msajili ameshindwa kusimamia na kulea vyama vya siasa, huku utashi wa baadhi ya waliopo katika ofisi hiyo ukilenga kudhoofisha demokrasia ya vyama vingi.

“Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa ni moja ya maeneo yanayohitaji mabadiliko ya kimfumo katika vyama vya siasa,” anasema.

Jambo, lililotokea kwa vyama hivyo, lilitokea pia kwa Chama cha NCCR Mageuzi na kusababisha kung’olewa kwa aliyekuwa mwenyekiti wake, James Mbatia.

Mbatia alisimamishwa katika nafasi hiyo na Halmashauri Kuu ya chama chake, ambayo hata hivyo alidai haikuwa na akidi iliyotimia. Hata hivyo, baadaye Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ilibariki uamuzi huo.

Kitendo hicho, kiliibua mjadala miongoni mwa wadau, kiasi kwamba ofisi ya msajili ililaumiwa kubariki jambo lililodaiwa kuwa batili.

Pamoja na malalamiko ya vyama vyote hivyo dhidi ya ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, lakini kila uamuzi wa ofisi hiyo ulikuwa ni utekelezaji wa ama dosari au malalamiko yaliyotokea ndani ya chama husika.

Lakini, wachambuzi wa masuala ya siasa, wanasema iwapo mambo hayo yangeshughulikiwa na mamlaka huru kama mahakama, pengine uamuzi ungekuwa mwingine, tofauti na ulioshuhudiwa kwa vyama kadhaa vya upinzani nchini.

Hata hivyo, Februari 23, 2026 Mwananchi ilizungumza na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, aliyekanusha madai hayo akisema tatizo la vyama vingi havizingatii katiba zao, sheria ya vyama vya siasa na kanuni walizojitengenezea wenyewe.

“Tatizo lingine baadhi ya watu wanataka uongozi bila kufuata utaratibu, lakini suala la msingi kufuata Katiba, Kanuni na Sheria ya Vyama vya siasa ingawa mivutano haiwezi kuisha kwa sabababu inasabishwa na vitu mbalimbali,”anasema

Alisema wakati mwingine zinatokana na mgongano wa mawazo lakini Ofisi ya Msajili huwa inasisitiza watu wazingatia Katiba, Kanuni na Sheria ya vyama vya siasa.

“Ofisi ya Msajili tunapotoa mwongozo huwa tunazingatia hayohayo, Katiba ya chama, kanuni na sheria ya vyama vya siasa,” alisema.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Said Majjid, amesema chanzo cha migogoro hiyo ni muundo wa kisheria unaoipa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa mamlaka makubwa kupita kiasi juu ya vyama vinavyopaswa kuwa huru.

Anafafanua Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992, pamoja na marekebisho yake ya 2022, imeweka mazingira ambayo msajili anaweza kuingilia masuala ya ndani ya chama kwa kigezo cha kusimamia utii wa sheria.

anasema katika mazingira ambayo chama tawala kina nguvu ya kisiasa na kiutawala, uwezekano wa ofisi kama ya msajili kutumika kisiasa huongezeka.

“Hata kama hakuna ushahidi wa moja kwa moja kila wakati, mtazamo wa upendeleo unajenga kutokuaminiana miongoni mwa wadau,” amesema Majjid.

Ametolea mfano Ghana na Afrika Kusini zilizoweka mipaka kati ya Serikali na taasisi zinazosimamia vyama vya siasa. Huko, msajili hana mamlaka ya kuamua migogoro ya uongozi wa chama bali mahakama ndiyo inafanya hilo.

Anasisitiza bila kufanya mageuzi ya kisheria yatakayopunguza mamlaka ya msajili na kuyapeleka kwenye vyombo huru kama mahakama, malalamiko kama hayo yataendelea kujirudia kila baada ya uchaguzi.

Udhaifu wa taasisi za vyama

Mchambuzi mwingine wa siasa, Dk Midard Maziku, amesema si sahihi kumlaumu msajili pekee, kwani vyama vya upinzani navyo vina udhaifu wa ndani unaovifanya kuwa rahisi kuingiliwa au kuyumbishwa.

Anaijenga hoja yake akirejea ripoti ya utafiti wa Uongozi wa Afrika ya Taasisi ya UNECA mwaka 2019, iliyoonyesha zaidi ya asilimia 60 ya vyama vya upinzani katika nchi zinazoendelea vina matatizo ya uongozi, ukosefu wa mifumo thabiti ya maamuzi na migogoro ya mara kwa mara ya Madaraka, hali inayotoa mwanya kwa taasisi za nje kuingilia kwa urahisi.

Anafafanua mara nyingi migogoro ya ndani inapozidi, wahusika hukimbilia kwa msajili au mahakamani, hivyo kuhalalisha kuingilia kwa taasisi hizo.

Kwa mtazamo wake, baadhi ya migogoro inayolalamikiwa sasa ilianza ndani ya vyama vyenyewe kabla ya kufikia hatua ya nje kuhusika.

Anasisitiza mageuzi ya kweli yanapaswa kuanzia ndani ya vyama vyenyewe. “Vyama lazima vijijenge kiutawala, viwe na mifumo ya uwajibikaji na demokrasia ya ndani. Vinginevyo vitaendelea kuwa dhaifu,” anasema.

Hata hivyo, anakiri kuwa hoja za kuingiliwa haziwezi kupuuzwa kabisa, bali zinapaswa kuangaliwa sambamba na udhaifu wa ndani wa vyama hivyo.

Dk Mziku, anasema kuingiliwa kwa vyama vya upinzani iwe ni kwa kiwango gani kunadhoofisha misingi ya ushindani wa kisiasa, ambao ni nguzo kuu ya demokrasia ya vyama vingi.

Kwa mujibu wa ripoti za taasisi za kimataifa kama Freedom House na Varieties of Democracy, nchi ambazo vyama vya upinzani vinakumbwa na vikwazo vya mara kwa mara huporomoka katika viwango vya uhuru wa kisiasa na uwajibikaji wa Serikali.

Anaongeza hali hiyo husababisha wananchi kupoteza imani na mchakato wa kidemokrasia.

“Wananchi wanapoona vyama haviko huru au vinaonekana kudhibitiwa, wanakata tamaa ya kushiriki siasa. Hii hupunguza ushiriki wa wapiga kura na kudhoofisha uhalali wa Serikali inayochaguliwa,” anasema.

Pia, anaonya hali hiyo inaweza kuchochea siasa za msuguano na hata migogoro ya kijamii. Historia ya nchi mbalimbali inaonyesha kukosekana kwa uwanja sawa wa kisiasa kunaweza kusababisha migogoro, hasa pale wananchi wanapohisi sauti zao hazisikiki.

Katika mtazamo wake, suluhisho linapaswa kuwa la kimfumo, kuimarisha uhuru wa taasisi, kuweka uwazi katika maamuzi ya msajili, na kuhakikisha kuwa migogoro ya vyama inatatuliwa na vyombo huru kama mahakama badala ya mamlaka ya kiutawala.

Anasisitiza umuhimu wa mazungumzo ya kitaifa kuhusu mustakabali wa demokrasia nchini, akisema bila makubaliano ya pamoja juu ya kanuni za uwanja sawa wa kisiasa, migogoro itaendelea kujirudia.

Kwa upande wa Majjid, anasema hali ya sasa si ya bahati mbaya, bali ni matokeo ya mfumo unaohitaji maboresho ya kina.

Miongoni mwa mapendekezo yake ni kufanya marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa ili kupunguza mamlaka ya msajili, kuimarisha demokrasia ya ndani ya vyama, na kuweka mifumo huru ya kutatua migogoro ya kisiasa.

Pia, anasisitiza umuhimu wa uwazi na uwajibikaji katika taasisi zote zinazohusika na siasa, pamoja na kujenga utamaduni wa kuheshimu tofauti za kisiasa.

Bila hatua hizo, anasema kila baada ya uchaguzi taifa litaendelea kusikia malalamiko yaleyale yakibadilika wahusika, lakini si kiini cha tatizo.

“Na hapo ndipo simulizi ya demokrasia ya Tanzania itabaki kudorora, haitakua,” anasema.