Na Said Mwishehe,Michuzi TV
JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limefanyika ziara ya kutembelea Kituo cha Kupoza Umeme cha Ifakara wilayani Kilombero mkoani Morogoro ambacho kimejengwa na Wakala wa Umeme Vijijini(REA) huku ikielezwa uwepo wa Kituo hicho umepeleka mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii.
Akizungumza katika ziara hiyo leo Machi 31,2026 , Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyoba, ameeleza kwamba kituo hicho kimemaliza changamoto ya kukatika kwa umeme iliyokuwa ikizorotesha shughuli za uzalishaji na huduma za kijamii.
Ameongeza Serikali inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kupitia REA imetoa Sh. bilioni 25 kugharamia ujenzi wa kituo hicho.Umeme unaozalishwa na kituo hicho ni megawati 18 na kati ya hizo saba ndio zinatimika.
Amefafanua umeme wa uhakika umefungua fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali ndani ya Wilaya hiyo.”Nitumie Jukwaa hili la Wahariri kuwakaribisha watu kuja kuwekeza.”
Kwa upande wakeMwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, amepongeza uwekezaji huo ambapo amefafanua unaonesha matumizi sahihi ya rasilimali za umma na mchango wa REA katika kusambaza umeme vijijini.
Amesisitiza REA wamefanya kazi kubwa ya kupeleka umeme vijijini na kwa sasa hakuna Mwananchi anayetoa rushwa kwa ajili ya kupatiwa nguzo TANESCO na hiyo imetokana na REA kuweka mikakati ya kuhakikisha nguzo za umeme zinapelekwa katika vijiji na sasa katika vitongoji.
Awali Meneja wa Usimamizi wa Miradi kutoka REA, Mhandisi Deogratius Nagu, amesema mradi huo umegharimu Sh.bilioni 25, ukihusisha pia ujenzi wa njia za kusafirisha umeme za msongo wa kilovolti 33 zenye urefu wa kilometa 70 pamoja na huduma za ushauri elekezi.
“Kituo hiki kimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Kilombero na Ulanga kwa kuondoa changamoto ya upatikanaji wa umeme na kuwezesha shughuli za kiuchumi kama kilimo na uchimbaji madini,” alisema.

