Kupungua kipaumbele cha lishe kunahatarisha afya ya watoto

Simiyu. Wakati juhudi za kuboresha afya ya jamii zikiendelea kufanyika nchini, wadau wa afya wameonya kuwa kupungua kwa uelewa na kipaumbele cha masuala ya lishe katika familia nyingi kunahatarisha afya ya watoto na kina mama, na kuongeza hatari ya matatizo ya utapiamlo.

Wakizungumza leo Aprili 1, 2026, wadau hao wamesema licha ya kuwepo kwa programu mbalimbali za kuboresha lishe nchini, bado jamii nyingi hazitoi uzito unaostahili kwa lishe bora kutokana na changamoto za kiuchumi, ukosefu wa elimu na mabadiliko ya mtindo wa maisha.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi Digital wanasema katika familia nyingi suala la lishe bora limekuwa halizingatiwi ipasavyo, huku wengi wakielekeza nguvu zaidi katika kuhakikisha familia inapata chakula cha kushibisha.

Mkazi wa Maswa, Maria Ndege, amesema mara nyingi watu huzingatia zaidi kushiba badala ya kula chakula chenye virutubisho muhimu kwa afya.

“Watu wengi wanajali kushiba tu. Ukipata ugali na mboga watu wanaona imetosha, lakini suala la lishe bora kama kula matunda, maziwa au vyakula vya protini halizingatiwi sana,” amesema.

Kwa upande wake, John Nyamhanga, mkazi wa Bariadi, amesema hali ngumu ya kiuchumi pia inachangia wananchi wengi kushindwa kuzingatia lishe bora katika familia zao.

“Watu wengi wanaelewa umuhimu wa lishe, lakini hali ya uchumi inafanya watu wale kile wanachokipata. Sio kila familia inaweza kumudu kununua vyakula vyenye virutubisho kila siku,” amesema.

Naye Aisha Majula amesema changamoto nyingine ni ukosefu wa elimu ya lishe katika jamii, hali inayosababisha baadhi ya wananchi kutofahamu namna ya kuandaa chakula bora hata kwa kutumia vyakula vinavyopatikana katika mazingira yao.

“Kama kungekuwa na elimu zaidi kuhusu lishe kwenye vijiji na mitaa, watu wengi wangeelewa namna ya kuandaa chakula bora hata kwa kutumia vyakula vinavyopatikana karibu nao,” amesema.

Akizungumzia hali hiyo, mtaalamu wa lishe kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu, Dk Chacha Magige, amesema kupungua kwa kipaumbele cha lishe katika jamii kunahatarisha afya ya watoto na kina mama.

Amesema lishe bora ni msingi muhimu wa afya njema, hasa kwa watoto katika miaka yao ya mwanzo ya maisha.

“Watoto wasipopata lishe sahihi katika miaka yao ya mwanzo wanaweza kupata udumavu, jambo linaloathiri ukuaji wa mwili na uwezo wa akili,” amesema.

Dk Magige amesema kuna umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu lishe bora na namna ya kutumia vyakula vinavyopatikana katika mazingira yao ili kuboresha afya.

Kwa upande wake, mtaalamu wa lishe na afya ya jamii, Peter Mathias, amesema changamoto nyingine ni kupungua kwa kampeni za uhamasishaji wa lishe katika ngazi ya jamii.

“Miaka iliyopita kulikuwa na kampeni nyingi za lishe katika vijiji na vituo vya afya, lakini sasa hazionekani sana. Tunahitaji kurudisha nguvu katika elimu ya lishe ili kupunguza matatizo ya utapiamlo,” amesema.

Amesema ushirikiano kati ya Serikali, wataalamu wa afya na viongozi wa jamii ni muhimu ili kuhakikisha elimu ya lishe inawafikia wananchi wengi zaidi.

“Bila kuimarisha afua za lishe katika ngazi ya familia na jamii, juhudi za kuboresha afya ya wananchi zinaweza kukwama,” amesema.