Dk Mwigulu atoa sababu kukatikatika kwa umeme

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesema kukatikakatika umeme kunakojitokeza ghafla hivi sasa, si upungufu wa nishati hiyo, bali uimarishaji wa Gridi ya Taifa.

Dk Mwigulu ameeleza hayo leo Jumatano Aprili mosi, 2026 wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya ofisi yake kwa mwaka 2026/27 bungeni jijini Dodoma, akiomba kuidhinishiwa Sh12.5 trilioni.

Ametoa maelezo hayo kipindi ambacho kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya hali hiyo ya umeme kukatika mara kwa mara ya kugeuka adha na wengine vifaa vyao kuunga.

Dk Mwigulu amesema nishati ya umeme ni injini ya kuimarisha na kurahisisha maendeleo ya kisasa hasa unapotumika katika shughuli za uendeshaji wa viwanda, teknolojia na matumizi ya nyumbani.

Amefafanua Serikali kwa kutambua hilo, imeendelea kutekeleza mikakati mahsusi ya kuhakikisha nishati ya umeme inayozalishwa nchini inakibidhi mahitaji yatokanayo na kasi kubwa ya ukuaji wa shughuli za uchumi na kijamii.

“Baada ya kukamilika kwa miradi mbalimbali ya uzalishaji wa umeme, ikiwemo ujenzi wa Bwawa la Julius Nyerere kwa kutumia fedha za ndani, hivi sasa nchi ina ziada ya megawati zaidi ya 2,000,” amesema.

Amesema Serikali itaendelea kujenga na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji wa umeme ili kuondoa changamoto ya kukatika katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na kuunganisha wilaya ambazo hazipo katika gridi ya Taifa.

“Mheshimiwa Spika, sasa hivi ukiona mahali umeme umekatika sio upungufu wa umeme, bali ni masuala ya uimara wa gridi. Serikali iweke zaidi ya Sh1 trilioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa gridi imara ili kutibu jambo la kukatika umeme,” ameeleza Dk Mwigulu.

Aidha, Dk Mwigulu amesema ili kuimarisha matumizi ya gesi asilia iliyoshindiliwa, amezielekeza Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Nishati, kushirikiana kuandaa viwango msawazo vitakavyoainisha mahitaji ya vyombo vya moto vya Serikali.

“Zijenge miundombinu ya kutosha kuwezesha vyombo hivyo kuanza kutumia gesi asilia iliyoshindiliwa,” amesema Dk Mwigulu.