Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba ameliomba Bunge kumuidhinishia Sh12.5 trilioni kwa mwaka 2026/27 huku akitoa maelekezo 11 likiwemo la kuanza kwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050.
Mengine ni pamoja na wakuu wa mikoa (RC) kusimamia mapokezi ya wanafunzi wapya wa elimu ya msingi, kuimarisha usimamizi wa makusanyo ya mapato kwa kutumia mfumo wa kielektroniki na mashine za POS.
Pia, taasisi na mamlaka zinazoshiriki katika uwezeshaji wananchi kiuchumi ziweke malengo yanayopimika na makandarasi wote wanaotekeleza na upatikanaji huduma ya uhakika.
Dk Mwigulu ameeleza hayo leo Jumatano Aprili Mosi, 2026 wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya ofisi yake kwa mwaka 2026/27 bungeni jijini Dodoma, akiomba kuidhinishiwa Sh12.5 trilioni.
Akiwa mwishoni kuhitimisha hotuba yake, Dk Mwigulu ameagiza kila sekta ihakikishe rasilimali za Taifa zinaelekezwa katika maeneo yenye tija na matokeo makubwa ili kupunguza utegemezi kutoka nje.
“Vilevile, kuendelea kuishirikisha sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika kuharakisha utekelezaji wa Dira 2050 ili kujenga uchumi jumuishi, shindani na unaotegemea uzalishaji wenye tija,”
Dk Mwigulu amewataka wakuu wa mikoa kusimamia kikamilifu maandalizi na mapokezi ya wanafunzi wa elimu msingi ya lazima ya miaka 10, watakaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2028 kwa kukamilisha miundombinu na huduma zote muhimu.
“Kuimarisha usimamizi wa makusanyo ya mapato kwa kutumia mfumo wa kielektroniki na mashine za POS, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma na kuendeleza rasilimali fedha katika miradi ya kimkakati na kielelezo,” amesema Mwigulu.
Aidha, Dk Mwigulu amezitaka wizara, taasisi na mamlaka zinazoshiriki katika uwezeshaji wananchi kiuchumi ziweke malengo yanayopimika, viashiria vya utendaji na ratiba za utekelezaji ili kuhakikisha mitaji hiyo inazalisha ajira, kipato na biashara endelevu hasa kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu.
Pia, amewataka makandarasi wote wanaotekeleza miradi ya Serikali kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa mikataba waliyoingia ikiwa ni pamoja na kuwalipa watoa huduma walioshiriki kwenye utekelezaji wa mradi husika.
“Maofisa masuhuli kuhakikisha wazabuni na watoa huduma wanalipwa kwa wakati kwa mujibu wa makubaliano na huduma iliyotolewa,”
“Wakuu wa mikoa, ndani ya miezi sita baada ya kuanza utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2026/27 kuhakikishe shule zote katika halmashauri zina matundu ya vyoo,” amesema.
Mbali na hilo, ametaka Wizara ya Maji ihakikishe huduma ya maji inapatikana kwenye shule na vituo vyote vya kutolea huduma ya afya ndani ya miezi sita baada ya kuanza utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2026/2027.
“Baada ya muda huo ni marufuku kwa wanafunzi kubeba maji na kupeleka shuleni. Pia ubora wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika sekta mbalimbali nchini uwiane na thamani ya fedha iliyotolewa.
“Fedha zinazoelekezwa na Serikali kwenye miradi hiyo zitumike kama ilivyokusudiwa na makandarasi wa ndani wawe wazalendo kwa kutumia ipasavyo fursa inayotolewa ya ushiriki wa kampuni zilizosajiliwa ndani, kutekeleza miradi mikubwa,” ameeleza Dk Mwigulu.
Sambamba na hilo, Dk Mwigulu amesisitiza wizara za kisekta, taasisi na mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha zinalipa fidia kwa wananchi wanaopisha maeneo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Serikali kabla ya kutwaliwa maeneo yao, kwa kuzingatia taratibu zilizopo.
Pia, taasisi zote za umma kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali ikiwemo mipango, programu na miradi ili kuongeza tija ya utendaji kazi na kuboresha huduma kwa wananchi.
Jambo jingine, Dk Mwigulu ameelekeza wizara, mikoa, mamlaka za serikali za mitaa, taasisi, wakala na idara zinazojitegemea kuanza kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi kama aliyoelekeza mkuu wa nchi.
