Dodoma. Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye amehoji iwapo Serikali itakuwa tayari kupitia upya mfumo wa bei kwenye minada ya korosho, kutokana na malalamiko ya namna bei zinavyopatikana.
Nape ameuliza swali hilo leo Jumatano, Aprili 1, 2026, alipouliza swali namba sita bungeni, ambapo katika swali la nyongeza ameeleza kuwa iwapo kutafanyika mapitio, itasaidia kubaini mambo mengi yanayosababisha wakulima kunyonywa.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema Wizara ya Kilimo, kupitia Bodi ya Korosho Tanzania, imeendelea kushirikiana na wadau kuendesha minada kwa njia ya kidijitali kupitia Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).
Kelele kuhusu bei ya korosho kwenye minada zimekuwa zikisikika karibu kila msimu, huku kukiwa na malalamiko kwamba Bodi ya Korosho haiwasaidii wakulima kupanga bei.
Mbali na hilo, wabunge wanaotoka katika mikoa inayolima korosho wamekuwa na vikao visivyo na mwisho kila inapoitishwa mikutano ya Bunge. Tukio linalokumbukwa zaidi ni pale aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli alipoliagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kusimamia ununuzi ili kudhibiti walanguzi.
Silinde amesema lengo la mfumo huo ni kuongeza uwazi, ushindani na kuimarisha bei kwa mkulima, na kuwa hatua hiyo imesaidia upatikanaji wa bei shindani kulingana na hali ya soko.
“Katika msimu wa 2025/26, korosho za Tanzania ziliuzwa kwa wastani wa Sh2,550 kwa kilo, ikilinganishwa na wastani wa Sh1,750 kwa kilo katika nchi za Msumbiji, Ivory Coast, Ghana, Nigeria na Benin,” amesema Silinde.
Amesema hali hiyo inaonyesha kuwa mfumo wa TMX una mchango mkubwa katika upatikanaji wa bei shindani kwa wakulima kulingana na hali ya soko la dunia.
Hata hivyo, Silinde amesema Serikali iko tayari kupokea maoni na ushauri ili kufanya maboresho zaidi pale inapobidi, kwa lengo la kuendelea kuimarisha mfumo wa uuzaji wa korosho kwa manufaa ya wakulima.
