Dar es Salaam. Hatimaye kilio cha maji kwa wakazi wa Magomeni Kota, jijini Dar es Salaam kipo karibu kupata jawabu, baada ya Serikali kuanza kufunga mifumo ya usambazaji wa huduma hiyo kwenye nyumba hizo.
Miundombinu hiyo kwa mujibu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), inatarajiwa kubadili mfumo wa uunganishaji wa huduma hiyo, kutoka mita moja kutumiwa na ‘block’ nzima, hadi kila mkazi kumiliki mita yake.
Marekebisho hayo, ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa maboresho ya makazi hayo, ambao Serikali ilitenga Sh2 bilioni kwa ajili hiyo ikiwamo kukarabati miundombinu iliyoharibiwa.
Uboreshaji huo unakwenda sambamba nyongeza ya matenki ya maji safi juu ya majengo hayo, hatua inayolenga kuhakikisha upatikanaji wa maji muda wote.
Hatua ya kila mkazi wa Kota kumiliki mita yake itarahisisha upatikanaji wa maji ya uhakika na kulipa ankara yake pasipo kama ilivyo sasa.
Ukarabati wa mradi huo wenye nyumba 644 unafanyika baada ya Mwananchi Julai 29, 2025, kuripoti taarifa ikielezea adha ya upatikanaji wa maji wanayokutana nayo wakazi wa nyumba hizo kwa kipindi cha miaka mitatu, ambapo kulikuwa na uharibifu wa miundombinu baada ya kukabidhiwa kwa wananchi.
Fundi akiendelea na shughuli ya uwekaji wa matenki ya nyongeza ya maji safi juu ya moja ya maghorofa ya Magomeni Kota.
Katika habari hiyo, ilifichuliwa kuwepo kwa wizi wa kinga radi katika majengo hayo pamoja na uchakavu wa majengo kwa ujumla, hali iliyosababisha Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), wanaosimamia mradi huo, kujitokeza na kueleza mipango ya kufanya maboresho.
Vilevile waliahidi kutenga Sh2 bilioni kwa ajili ya kuanza matengenezo na maboresho ya mifumo ya maji pamoja na lifti zinazotumika kupanda na kushuka.
Awali, wakazi hao walilazimika kuchangia mita moja, hatua iliyosababisha kusuasua kwenye malipo yaliyojumuishwa kwenye gharama ndogo ya Sh30,000 kila mwezi kwa ajili ya huduma mbalimbali ikiwamo usafi, maji, umeme na malipo ya walinzi.
Gharama ya Sh30,000 imekuwa kama mwiba kwa baadhi wakazi wa nyumba hizo ambao wamekuwa na tabia ya kutochangia kwa ufanisi, hali inayosababisha kuzorotesha utoaji wa huduma.
Kusuasua huko ndiko kulisababisha Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), kusitisha huduma ya maji, hata hivyo baadaye uongozi wa Magomeni Kota ulimaliza deni hilo.
Dawasa ilivyokata maji hayo wakazi wa nyumba hizo walilazimika kununua maji ya kwenye madumu na kutumia lifti kuyapandisha juu kwa wanaoishi ghorofani.
Ambapo hali hiyo ilichangia baadhi ya lifti kuharibika kutokana na maji kumwagika na kuathiri mashine zake. Hatua ya kuweka miundombinu ya mifumo hiyo, ili kurejesha huduma za maji itakata kiu ya wakazi hao na kuondokana na adha ya kununua maji ya madumu.
Katika ufuatiliaji wake, Mwananchi limebaini uwepo wa mafundi wakiweka miundombinu hiyo ya kuwezesha upatikanaji wa maji safi na kila mkazi awe na mita yake kwenye majengo yote matano ya Magomeni Kota.
Ambapo kabla ya kuanza kwa maboresho hayo wakazi wa nyumba hizo walitakiwa kupeleka nyaraka muhimu zilizohitajika kwenye ofisi za serikali za mitaa kwa ajili utambuzi wa kuwekewa mita za maji.
Walichokisema viongozi, wananchi wa Magomeni Kota
Mwenyekiti wa wakazi wa Magomeni Kota, George Abel, amesema ukarabati huo ulianza siku 10 zilizopita, ambapo kwa sasa wanaongeza matenki ya maji safi juu ya majengo yote.
“Pia wameanza kunyonya majitaka yaliyokuwa yanasumbua kwa muda mrefu, hali ambayo sasa imeimarika. Wamerudisha miundombinu ya umeme iliyokuwa imeibiwa, na kazi inaendelea kwa kasi,” amesema.
Amesema changamoto iliyobaki kwa sasa ni suala la malipo ya huduma, ambalo linawahusu wakazi wenyewe. Hivi sasa wanasubiri mwongozo au sheria inayotayarishwa na Serikali ili kuweka utaratibu utakaowahusisha wakazi wote.
Abel amesema hatua ya kila mkazi kutumia mita yake itaondoa ile changamoto ya kulimbikiza madeni kupitia mita moja kwa hiyo kila mmoja atawajibika kulingana na matumizi ya maji katika nyumba yake.
“Utalipia huduma ya maji kutokana na uwezo wako na usipolipia kama ni kukatiwa au vinginevyo itamuhusu muhusika wa mita husika na si wakazi wote, Serikali inafunga mita janja, pili tutaondoa adha ya kukaa kwa kipindi cha miaka miwili bila huduma ya maji,”amesema
Mmoja wa viongozi wa jengo katika makazi hayo amesema kuwa mabadiliko yaliyofanyika ni makubwa, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya maji na uwekaji wa kinga radi zilizokuwa zimeibiwa.
“Kwa sasa kinga radi zimewekwa katika majengo yote. Vilevile, wanaendelea kuongeza matenki ya maji safi, kunyonya majitaka na kusafisha chemba zote zilizokuwa zimejaa taka,” amesema.
Kwa upande wake, Mmoja wa Wakaazi wa eneo hilo, Salma Rashid ameishukuru Serikali kwa ukarabati huo unaoenda kujibu kilio chao cha upatikanaji wa maji maana hali ilikuwa mbaya.
“Tumeona hizo jitihada hii ni wiki ya pili mafundi wanaendelea kutengeneza mifumo tunaomba mchakato huo usichukue muda mrefu ili huduma ya maji ianze kupatikana.”
“Suala la wakazi kutoa Sh30,000 kwa ajili huduma jumuishi limekuwa changamoto licha ya viongozi wetu wa majengo kutoa elimu ya mara kwa mara, bado kuna shida tunaomba Serikali isimamie na iangalie kuwachukulia hatua wasiolipa kwani wanawaumiza wanaotoa,”amesema.
Katika maelezo yake, Salma amelishukuru gazeti la Mwananchi kwa kupaza sauti changamoto ambazo zimeanza kupatiwa ufumbuzi na Serikali.
Mkurugenzi wa Idara ya Miliki wa TBA, Said Mndeme, amesema wameanza ukarabati pamoja na ufungaji wa mifumo mipya ya maji itakayowezesha kila nyumba kuwa na mita yake ya huduma ya maji.
Amesema uwekaji wa mifumo hiyo ni utekelezaji wa mahitaji ya wakazi, kwani awali huduma ya maji ilikuwa ikishirikishwa kwa pamoja, hali iliyowalazimu kutegemea michango yao kulipia huduma hiyo, jambo ambalo lilionekana kuwa gumu.
Kutokana na changamoto hiyo, Mndeme amesema Serikali ilichukua hatua ya kuweka miundombinu mipya itakayosaidia kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na mita yake ya maji.
“Ni hatua inayohitaji gharama kubwa, lakini Serikali iliona umuhimu wa kubeba gharama hizo kwa lengo la kuwapatia wananchi huduma bora,” amesema Mndeme.
