Daraja latitia, lakata mawasiliano Kwamfipa-Msangani

Kibaha. Wananchi wa maeneo ya Msangani na Kwa Mfipa, wilayani Kibaha, mkoani Pwani wameeleza adha wanayopitia kufuatia kubomoka kwa daraja linalounganisha maeneo hayo na kukata mawasiliano na shughuli za kijamii na kiuchumi.

Kubomoka kwa daraja hilo kunaelezwa kusababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini ikiwamo Kibaha.

Wakizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Aprili 1, 2026 baadhi ya wakazi wa eneo hilo na maeneo jirani wameeleza adha wanayopitia, ikiwamo kulazimika kupita umbali mrefu na gharama za nauli kuongezeka mara mbili zaidi.

Halima Mussa amesema hali imekuwa ngumu hasa kwa watoto wanaokwenda shule na wagonjwa wanaohitaji huduma za haraka.

Mkazi mwingine, Seleman Mbegu amesema kubomoka kwa daraja hilo kumelazimu kupanda kwa gharama za usafiri kutoka Sh4,000 mpaka Sh5,000 hadi kufikia Sh8,000.

“Tunaomba mamlaka itusaidie kujenga daraja jipya mapema ili kurudisha mawasiliano,  hili lililobomoka lilikuwa limeanza kuonyesha dalili za kuchakaa kwa muda mrefu lakini hakuna hatua iliyochukuliwa hadi kuporomoka,” amesema.

Mkazi mwingine, Gaspar Raphael amesema barabara hiyo ilikuwa ndiyo tegemeo kwa wakazi wengi wa maeneo ya Simbani, Galagaza, Kumba, Kidenge hadi Msangani kufika kwa urahisi kwa Mathias.

“Hivi sasa tunatakiwa kuzungukia kwa Mfipa, ndipo tuanze kurudi, pia barabara imefungwa tangu mwaka jana kwamba inatakiwa kujengwa, hivyo nafuu kwetu ilikuwa ni hii ya Msangani ambako sasa daraja limeporomoka.

Daraja linalounganisha Msangani na Kwa Mfipa,  Kibaha mkoani Pwani likiwa limebomoka

Amesema kwa adha wanayopitia wakazi wa maeneo hayo, wanaiomba mamlaka ione namna gani itawasaidia kujenga daraja jipya, na si kuweka karavati kama ilivyokuwa kwenye hilo lililoporomoka.

Diwani wa Msangani, Frank Msimbe amesema tayari wamesharipoti kwa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura) kuhusu daraja hilo.

“Tunategemea litajengwa ndani ya miezi mitatu hadi minne ijayo, hivi sasa wananchi tumewaelekeza wazungukie Kwamfipa, Msangani gari hazipiti.

Tumeifunga hiyo barabara ingawa tumeweka kivuko kwa ajili ya dharura ili kupita wanafunzi maana eneo hilo lina shule pia,” amesema.

Meneja wa Wakala wa barabara mijini na Vijijini (Tarura) wilaya ya Kibaha, Samuel Ndoveni amesema tayari wameiandika bajeti, hela itakapotoka ujenzi utaanza.

“Siwezi kusema ni lini, lakini tunafahamu daraja hilo na tayari tumeshaliandikia bajeti, hela itakapotoka ujenzi utafanyika,” amesema.