………
Na Carlos Claudio, Dodoma
Jeshi la Polisi mkoani Dodoma linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kumuua dereva wa bodaboda, Omary Bakari (21), mkazi wa eneo la Michese jijini Dodoma.
Inadaiwa kuwa marehemu aliuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali katika maeneo ya shingoni na mgongoni, kwa lengo la kunyang’anywa pikipiki yake.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera, alisema tukio hilo lilitokea Machi 21 mwaka huu majira ya saa tatu na nusu usiku, katika mtaa wa Chinyoya, kata ya Kilimani jijini Dodoma.
Kamanda Hyera alieleza kuwa kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi lilifanya msako na doria kali, ambapo walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja, Sadick Jonathan (23), katika Kijiji cha Mazase, Wilaya ya Chamwino, akiwa na pikipiki ya marehemu yenye namba za usajili MC 556 FPE, aina ya Sinoray, rangi nyeusi
Alisema baada ya mahojiano, mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na tukio hilo akishirikiana na wenzake wawili, Paulo Abiel (26) na Ramadhani Hamidu (35), wote wakazi wa Dodoma. Watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa katika harakati za kutoroka kuelekea mikoa jirani.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi mkoani humo limefanikiwa kukamata watuhumiwa 12 wanaodaiwa kuhusika na mtandao wa wizi wa mifugo katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Miongoni mwa waliokamatwa ni Kedmon Steven pamoja na wenzake 11, ambao inadaiwa hujihusisha na uhalifu huo kwa kutumia silaha.
Baada ya kuiba mifugo, huichinja na kuisambaza katika maeneo ya biashara ili kujipatia kipato kwa njia isiyo halali.
Aidha, polisi wamewakamata baadhi ya wafanyabiashara wanaodaiwa kushirikiana na watuhumiwa hao kwa kununua na kuuza mifugo au nyama hiyo kinyume cha sheria.
Kamanda Hyera alisisitiza kuwa watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.