Mixx by Yas, KCB ‘kuwabustisha’ mawakala wao

Dar es Salaam. Benki ya KCB Tanzania imeingia ubia na Mixx by Yas kutoa mikopo ya kidijitali kwa mawakala wake ikiwa ni jitihada za kujenga mfumo jumuishi wa kifedha kidijitali na kuwafikia Watanzania wengi zaidi.

Ushirikiano huo, ujulikanao kama Bustisha Wakala, ni suluhisho la kimkakati la mkopo wa muda mfupi linalolenga kuhakikisha upatikanaji wa ukwasi kwa mawakala, ili waweze kutoa huduma za kifedha kwa wananchi bila kukwama.

Mbali na hilo, mpango huo unakusudia kubadilisha na kupanua huduma za kifedha nchini kote kwa kuwafikia zaidi ya wanachama 200,000 kupitia mtandao wa mawakala wa taasisi hizo.

Uzinduzi wa huduma hiyo ulifanyika Machi 31, 2026 katika Makao Makuu ya Benki ya KCB jijini Dar es Salaam, ambapo pande zote zilisema mawakala ni kiungo muhimu kinachounganisha mamilioni ya Watanzania na huduma za kifedha.

Akizungumza katika hafla hiyo Aprili 1, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya KCB Tanzania, Cosmas Kimario alisema kupitia mpango huo mawakala watapata fedha kwa wakati wanapozihitaji. Hali hiyo itasaidia kuhakikisha huduma zinaendelea bila kukatika na kuongeza fursa za kiuchumi.

Alisema tangu kuanza kwa majaribio ya huduma hiyo Februari 27, 2026, zaidi ya mawakala 7,000 wamefaidika na mpango huo.

Alisema programu hiyo inatarajiwa kukua kwa kasi kupitia mtandao wa Mixx by Yas, hatua itakayochochea ushirikishwaji wa kifedha na kuimarisha biashara za ndani.

“Tunapomwezesha wakala mmoja, tunawawezesha mamia ya wateja. Tunapouimarisha mfumo, tunaiimarisha pia uchumi,” alisema Kimario.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mixx by Yas, Angelica Pesha amesema ushirikiano huo una lengo la kuwapatia mawakala zana sahihi za kifedha ili kukuza shughuli zao.

Alisema kupitia mikopo ya papo hapo ya kidijitali, taasisi hiyo inaimarisha dhamira ya kuchochea uwezeshaji wa kiuchumi, kuongeza uaminifu wa mawakala na kuimarisha imani ya wateja katika huduma za kifedha za kidijitali.

“Tumejizatiti kujenga suluhisho zinazowawezesha mawakala wetu, ambao ni nguzo ya ushirikishwaji wa kifedha nchini. Bustisha Wakala ni zaidi ya bidhaa; ni kichocheo cha ustahimilivu wa kiuchumi na fursa kwa ngazi ya chini,” alisema.