Dar es Salaam. Wagombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, wamekutana na Rais Samia Suluhu Hassan, kujadili kuhusu namna ya kuimarisha maridhiano ya kisiasa, demokrasia ya vyama, amani na mshikamano wa kitaifa.
Hatua hiyo, imekuja miezi mitano tangu uchaguzi huo ufanyike na kumpata Rais Samia aliyegombea kwa tiketi ya CCM ushindi wa zaidi ya asilimia 96 na baadaye akaapishwa kuiongoza Tanzania kwa muhula wa pili.
Katika uchaguzi huo, Samia alishindana na wagombea 16 kutoka vyama mbalimbali vya siasa, ambao wote ndio waliohudhuria kikao hicho na mkuu huyo wa nchi kujadili kuhusu mustakabali wa Taifa.
Taarifa ya kikao hicho, imetolewa leo, Jumatano Aprili 1, 2026 na kutiwa saini na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Shaaban Kissu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanasiasa hao, walitumia nafasi hiyo kuwasilisha maoni yao kuhusu namna ya kuimarisha maridhiano ya kisiasa, demokrasia ya vyama, amani na mshikamano wa kitaifa baada ya uchaguzi mkuu.
Pia, wametoa maoni kuhusu namna ya kuimarisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo na kudumisha tunu za umoja wa kitaifa.
Taarifa hiyo inaeleza, majadiliano hayo pia yaligusia umuhimu wa kuendeleza maadili ya uongozi, uwajibikaji na siasa zenye staha, kama msingi wa kujenga Taifa lenye utulivu wa kisiasa na maendeleo endelevu.
Katika kukuza demokrasia jumuishi, taarifa inaeleza viongozi hao walisisitiza ushirikishwaji wa wadau mbalimbali katika masuala ya kitaifa na mchakato wa maendeleo.
Pia, imeeleza wanasiasa hao wametaka kulindwa kwa utulivu wa kisiasa wakati wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo, kwa kutambua kuwa mazingira ya amani na umoja ni msingi wa ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.
“Sambamba na hilo, walielezea umuhimu wa kuimarisha utamaduni wa uvumilivu wa kisiasa, kuheshimiana na kujenga uaminifu miongoni mwa wadau wa kisiasa, kama njia ya kuendelea kudumisha utulivu wa nchi,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa inaeleza, wanasiasa hao walieleza haja ya kuendeleza mazungumzo ya mara kwa mara baina ya viongozi wa kisiasa ili kujenga maelewano ya pamoja na kushughulikia changamoto za kitaifa kwa njia ya mazungumzo na ushirikiano.
“Mazungumzo hayo yanaakisi dhamira ya Rais Samia ya kuendeleza mawasiliano ya wazi na ya kujenga miongoni mwa viongozi wa kisiasa, kwa lengo la kuimarisha maridhiano na mshikamano wa kitaifa,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
