Geita. Hofu imetanda kwa wakazi wa Kijiji cha Nyakagwe, Kata ya Butobela wilayani Geita baada ya ng’ombe 13 kufa ghafla wakidaiwa kunywa maji yanayotiririka kutoka eneo la mradi wa uchenjuaji wa dhahabu, hali iliyomlazimu Mkuu wa Wilaya hiyo kuagiza uchunguzi wa kina wa sampuli za maji katika eneo hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, ametoa agizo hilo leo Aprili 1, 2026 wakati alipotembelea eneo la tukio akiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya pamoja na maofisa wa mazingira, madini, Mamlaka ya Maji na usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) na wataalamu wa Bonde la Ziwa Victoria.
Akizungumza katika ziara hiyo, Komba ameagiza taasisi hizo kushirikiana kuchukua sampuli za maji katika mto unaozunguka mradi wa uchenjuaji wa dhahabu unaomilikiwa na Simon Kiganga, ili kubaini kama maji hayo yana kemikali hatarishi kwa binadamu na mifugo.
“Ni vyema wenzetu wa Tume ya Madini mkashirikiana na Ruwasa pamoja na Bonde la Ziwa Victoria kuchukua sampuli za maji katika maeneo haya na hata sehemu ambazo maji haya yanaelekea, ili kujiridhisha kuhusu usalama wake kwa wananchi wanaoyatumia,” amesema Komba.
Mbali na uchunguzi huo, ameagiza ukaguzi wa mara kwa mara katika miradi ya uchenjuaji wa madini huku akiwataka maofisa mifugo kutoa elimu kwa wafugaji kuchukua tahadhari wanapochunga mifugo yao karibu na machimbo.
Akieleza kuhusu tukio hilo, Kaimu Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini Geita, Hussein Nzima, amesema ng’ombe hao walibainika wakiwa wamekufa Machi 23, 2026 katika mwalo wa dhahabu uliopo karibu na eneo la mradi huo.
Amesema baada ya ukaguzi uliohusisha ofisi ya madini, viongozi wa eneo hilo pamoja na ofisa mifugo, walibaini kuwa mifugo hiyo huenda ilikufa kutokana na sumu ya cyanide, kemikali inayotumika katika shughuli za uchakataji madini ya dhahabu.
“Baada ya kufuatilia tuligundua kulikuwa na dalili za maji kutiririka kutoka kwenye shimo la kuhifadhia maji yenye kemikali katika mradi huo, hali iliyosababisha maji hayo kufika eneo ambalo mifugo ilikuwa ikinywa,” amesema Nzima.
Ameongeza kuwa mmiliki wa ng’ombe hao alilipwa fidia ya Sh20 milioni baada ya makubaliano maalumu kufikiwa, huku mifugo hiyo ikifukiwa chini ya usimamizi wa daktari wa mifugo ili kuzuia madhara kwa binadamu.
Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Proches Norbert, amesema baada ya kupokea taarifa za tukio hilo walifika eneo la tukio Machi 24, 2026 na kuchukua hatua za kisheria ikiwamo kumpiga faini mwekezaji huyo ya Sh10 milioni kwa mujibu wa kanuni za mazingira.
Naye Diwani wa Kata ya Butobela, PaschalMapungo, amemtaka mwekezaji huyo kutumia miundombinu ya kisasa katika kupitisha maji yenye kemikali badala ya mifereji inayochimbwa kwa mikono.
“Tunalenga kuona wawekezaji wanafanya kazi zao kwa usalama huku wakilinda afya za wananchi na mazingira yanayowazunguka,” amesema Mapungo.
