Dar City ilivyopunguzwa kasi Sauzi

Timu ya kikapu ya Al Ahly Ly kutoka Libya jana iliipunguza kasi Dar City kwa kuifunga pointi 118-97 katika Ligi ya Kikapu Afrika (BAL), mchezo uliofanyika katika uwanja wa ndani wa Sun Bet Area mjini Pretoria, Afrika Kusini.

Kinachoelezwa ni kwamba Al Ahly Ly ilitumia michezo miwili ya awali ambayo Dar City ilishinda dhidi ya Johannesburg Giants na Nairobi City Thunder kuifanyia kazi kwa ajili ya mechi hiyo ambayo mabingwa hao wa Ligi ya Kikapu Dar es Salaam (BDL), walipasuka kwa tofauti ya pointi 21.

Katika mchezo huo, Al Ahly Ly iliongoza katika robo zote za mchezo zikimalizika kwa pointi 25-14, 26-20, 36-28 na 31-35. Takwimu za msimamo wa ligi zinaonyesha kuwa Dar City inatakiwa kushinda angalau mchezo mmoja ili iweze kucheza mchujo wa BAL yaani BAL Playoff itakayofanyika nchini Rwanda kuanzia Mei 22 hadi 31.

Mchezo wa nne kwa timu ya Dar City utachezwa kesho, Ijumaa, dhidi ya Petro De Luanda kutoka Angola, na Jumamosi itacheza dhidi ya RSSB Tigers kutoka Rwanda. Endapo Dar City itashinda angalau mchezo mmoja, itakuwa imeshinda michezo 3-1. Ushindi huo utaiweka katika nafasi ya miongoni mwa timu nne zitakazocheza Ligi ya BAL Playoff, zikitoka katika kundi la Kalahari Conference.

Kundi la Kalahari Conference lina timu za Petro de Luanda (Angola), Al Ahly Ly (Libya), RSSB (Rwanda), Nairobi City Thunder (Kenya), Dar City (Tanzania), na Johannesburg Giants (Afrika Kusini).

Mashindano ya BAL Playoff yatajumlisha timu nane, nne kutoka Kalahari Conference na nne kutoka Sahara Conference, ambayo itachezwa nchini Morocco. Kundi la Sahara Conference linaundwa na FUS de Rabat (Morocco), Al Ahly (Misri), ASC Ville de Dakar (Senegal), Club African (Tunisia), JCA Kings (Ivory Coast), na Maktown Flyers (Nigeria). Michezo ya kundi hili itaanza kuchezwa Aprili 24.