Singida, Azam ni bato ya nafasi NBC PL

PALE Uwanja wa Airtel, Singida, kuna patashika ya ubora ambapo wenyeji, Singida Black Stars, wataikaribisha Azam FC katika mchezo utakaobeba vita ya ubora wa wachezaji na ufundi wa makocha wa timu hizo mbili.

Mchezo huo wa Ligi Kuu Bara utakaoanza saa 10:00 jioni utakuwa na dakika 90 ngumu kutokana na ubora wa vikosi hivyo ambavyo havijaachana sana kwenye msimamo wa ligi.

Azam inatambua ugumu wa mchezo huo, ambapo haraka imewasafirisha mastaa wake watano waliokuwa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, wakiwemo makipa Zuber Foba na Aishi Manula, mabeki Lameck Lawi na Twalib Nuhu, pamoja na viungo Idd Seleman ‘Nado’ na Feisal Salum ‘Fei Toto’, kuwahi mchezo huo.

Taarifa mbaya kwa Azam ni kwamba itamkosa mshambuliaji wake Mkongomani, Jaque Ngita, ambaye alikwenda kuitumikia timu ya taifa ya vijana ya nchi yake na kushindwa kurejea kwa wakati tayari kwa mchezo huo.

Azam haina rekodi nzuri sana msimu huu ikiwa ugenini, ambapo katika michezo yake mitano iliyopita imetoa sare tatu na kushinda mmoja pekee ilipoifunga Dodoma Jiji mabao 3-0, huku ikiwa na matokeo mazuri zaidi nyumbani.

Rekodi zinaonyesha kuwa matajiri hao wa Chamazi, katika mechi saba za ligi zilizopita dhidi ya Singida, wameshinda nne huku wenyeji wao wakishinda mbili, na timu hizo zikitoka sare mchezo mmoja, ambao ni wa mwisho kwao kukutana uliomalizika kwa sare ya 0-0 pale Azam Complex, uliopigwa Desemba 3, 2025.

Kocha wa Azam, Florent Ibenge, akizungumzia mchezo huo, amekiri kwamba timu yake inakwenda kucheza mechi ngumu dhidi ya Singida yenye kikosi kizuri, lakini anaamini maandalizi yao yatawabeba kupata ushindi.

“Hatujapata muda wa kutosha kujiandaa na mchezo huu kutokana na ratiba ya mechi za kimataifa, lakini jambo zuri ni kwamba wachezaji wetu wamefika kwa wakati. Tumepata vipindi viwili vya mazoezi, nadhani itakuwa mechi nzuri tukijua kwamba tunakwenda kukutana na moja ya timu bora kwenye ligi,” alisema Ibenge.

Azam, iliyopo nafasi ya tatu kwenye msimamo, itategemea ubora wa mastaa wao wawili, Fei Toto aliye kwenye kiwango kizuri akiwa na mabao sita na asisti tano, huku akifuatiwa na Nado aliyefunga mabao matano.

Singida si wanyonge wakiwa nyumbani, ambapo katika mechi zake tano zilizopita za ligi imeshinda tatu na kupoteza mbili, ikipoteza pointi sita zilizochukuliwa na Simba na Yanga waliopata ushindi kwenye uwanja huo mpya.

Singida itawategemea mastaa wao wawili, Ibrahim Imoro mwenye mabao matatu na asisti nne, pamoja na mshambuliaji Mrundi, Mosi Nduwumwe, mwenye mabao matatu, anayetarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.

Singida, iliyopo nafasi ya sita kwenye msimamo, itakuwa na mtihani wa kutafuta namna ya kuzuia ubabe wa Azam chini ya Ibenge, ambayo haijapoteza mchezo wowote wa ligi msimu huu.

Kocha wa Singida, David Ouma, alisema mchezo dhidi ya Azam hautakuwa rahisi kutokana na ubora wa kikosi chao, na kwamba wamejiandaa vyema kuwazuia matajiri hao.

“Tumejiandaa vizuri na mechi hii. Ninachoweza kusema ni kwamba wachezaji wako tayari, wanatambua kuwa mpinzani wetu ni timu nzuri yenye wachezaji bora kama walivyo waliopo kwenye timu yetu. Tunataka kupanda juu kwenye msimamo, hivyo tutazitaka pointi hizi tatu,” alisema Ouma.