Dar es Salaam. Mfumuko wa bei ya mafuta duniani unaotokana na vita na mzozo wa kisiasa Mashariki ya Kati umeanza kulazimisha baadhi ya mataifa ya Afrika kuchukua hatua za dharura za kiuchumi ili kulinda wananchi wake.
Wakati Tanzania ikitangaza bei mpya za mafuta ya petroli na dizeli, Zambia, Namibia na Afrika Kusini tayari zimeanza kupunguza kodi na ushuru wa mafuta kwa muda, hatua inayolenga kupunguza mzigo kwa wananchi pamoja na sekta za uchukuzi.
Leo Jumatano, Aprili 1, 2026, bei mpya za mafuta ya petroli na dizeli zimetangazwa Tanzania, ambapo nishati hiyo imepanda kwa Sh950 kwa lita na baadhi ya maeneo sasa lita moja ni zaidi ya Sh3,900, hali inayohofiwa kuongeza gharama za maisha kwa wananchi.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaketi ili kuangalia uwezekano wa kuleta unafuu kwa Watanzania.
Akiwasilisha makadirio ya bajeti ya ofisi yake kwa mwaka 2026/27, Dk Mwigulu amesema: “Tumeona bei zimeshaanza kupanda, tutakaa ndani ya Serikali kuhakikisha tunakabiliana nalo vipi suala hili ili wananchi waendelee kupata mafuta kwa bei nzuri na kudhibiti kupanda kwa gharama za maisha.”
Hata hivyo, Dk Mwigulu amewahakikishia Watanzania kuwa licha ya changamoto zinazoendelea Mashariki ya Kati, Serikali itaendelea kusimamia upatikanaji wa petroli na dizeli ili kuhakikisha bei zinaendelea kuwa himilivu.
Taarifa kutoka Zambia zinaeleza taifa hilo limepunguza kodi za mafuta kwa kipindi cha miezi mitatu baada ya bei za petroli kufikia takriban Sh3,763 kwa lita na dizeli kufikia Sh4,134 kwa lita.
Vyombo vya habari, kikiwemo Iharare, vimeripoti Bodi ya Usimamizi wa Nishati ya Zambia (ERB) imetangaza uamuzi huo katika taarifa kwa vyombo vya habari ya Machi 31, 2026, ikieleza hatua hiyo ni ya muda na inalenga kulinda wananchi dhidi ya ongezeko la bei za mafuta duniani.
Katika taarifa hiyo, ERB imeeleza serikali imeamua kuingilia kati kwa kusitisha ushuru na kodi za VAT kwa petroli na dizeli kuanzia Aprili hadi Juni 2026, hatua inayolenga kupunguza athari za ongezeko kubwa la bei huku ikihakikisha upatikanaji wa mafuta unaendelea kuwa wa uhakika.
Hatua hiyo inadaiwa kupunguza hofu ya kupanda zaidi kwa bei za nishati, huku ongezeko lililopo likiwa la wastani ukilinganisha na matarajio ya awali.
ERB imebainisha kuwa ongezeko la bei limechangiwa kwa kiasi kikubwa na mzozo wa kisiasa Mashariki ya Kati pamoja na kuporomoka kwa thamani ya sarafu ya Kwacha dhidi ya dola ya Marekani, hali iliyoongeza shinikizo katika soko la mafuta.
Kwa upande wa Namibia, taifa hilo linaripotiwa kupunguza kodi ya mafuta kwa asilimia 50 kwa muda wa miezi mitatu kuanzia Aprili 1, 2026.
Iharare imemnukuu Waziri wa Viwanda, Madini na Nishati, Modestus Amutse, akieleza hatua hiyo imechukuliwa kutokana na mabadiliko makubwa ya bei za bidhaa za petroli yanayotokana na mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati.
Baada ya hatua hiyo, bei ya petroli nchini Namibia inakadiriwa kufikia Sh3,180 kwa lita, huku hatua zinazochukuliwa zikidaiwa kupunguza mzigo kwa watumiaji pamoja na sekta ya uchukuzi.
Shirika la Ecofin Agency limeripoti Afrika Kusini pia imechukua hatua za dharura kwa kupunguza kodi ya mafuta kwa muda wa mwezi mmoja kuanzia Machi 31, 2026.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Waziri wa Fedha, Enoch Godongwana, pamoja na Waziri wa Madini na Rasilimali za Petroli, Gwede Mantashe, wameeleza mzozo wa Mashariki ya Kati umeongeza hatari katika masoko ya nishati duniani na kuongeza shinikizo la bei ndani ya nchi hiyo.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Serikali ya Afrika Kusini imesema imeanza utekelezaji wa hatua hiyo kuanzia Aprili Mosi hadi Mei 5, 2026.
Wakati mataifa hayo yakichukua hatua, kupanda kwa bei ya mafuta kumeripotiwa kuathiri pia nchi nyingine barani Afrika, ikiwemo Zimbabwe ambako hali inaelezwa kuwa ya wasiwasi.
Taarifa zinaeleza nchini humo, bei ya petroli imefikia Sh5,750 kwa lita huku dizeli ikiuzwa kwa Sh5,433 kwa lita, hali inayoonyesha ukubwa wa changamoto inayolikabili bara hilo.
